Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tukiwathamini walimu, ubora wa elimu utakua

Walimu wakiwajibika shuleni.Wadau wanaeleza za kuwa moja  ya mbinu za kukuza ubora wa elimu shuleni, kuwathamini walimu. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Alisema; “….Elimu ni kitu cha kumkuza binadamu tu. Kumwezesha kupanua uwezo wake. Anawiri….elimu kazi yake ya kwanza na kubwa zaidi ni hii ya kupambana na mazingira yanayomzuia binadamu kushamiri”

Siyo vibaya tukijiuliza tena, elimu ni nini? Majibu ni mengi ila Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kueleza maana ya elimu wakati akizungumza na wakuu wa shule za sekondari mwaka 1975.

Alisema; “….Elimu ni kitu cha kumkuza binadamu tu. Kumwezesha kupanua uwezo wake. Anawiri….elimu kazi yake ya kwanza na kubwa zaidi ni hii ya kupambana na mazingira yanayomzuia binadamu kushamiri”

Mwalimu alisisitiza kuwa elimu ni kitu cha kutusaidia katika mapambano ya maisha. Elimu lazima impatie mhitimu uwezo wa kupambana na mazingira yanayomzuia kuchanua au kuendelea katika harakati za kujipatia maisha bora.

Ndiyo maana kila ngazi ya elimu iwe ni msingi, sekondari au elimu ya juu, ina malengo mahususi ambayo lazima mhitimu ayafikie.

Kwa kuzingatia tafsiri hii ya elimu, tujiulize ni kwa kiasi gani elimu inayotolewa hapa nchini inaakisi maana ya elimu? Je, wahitimu katika ngazi mbalimbali za elimu kweli wana uwezo wa kupambana na mazingira halisi wanayokwenda kuishi?

Bila shaka wengi tunakubaliana kuwa, kwa muda mrefu elimu yetu imekuwa ikilalamikiwa kwa kushindwa kuzalisha wahitimu wenye sifa za kuajiriwa au kujiajiri. Je, ni wapi tulipoanguka?

Tunawezaje kutoka hapa tulipo?

Changamoto za elimu Tanzania ni nyingi na zinafahamika wazi kwa wadau wote kuanzia wanafunzi mpaka Serikali.

Changamoto hizi zimekuwa zikisemwa kwa muda mrefu sasa wadau mbalimbali wamekuwa wakifanya jitihada kukabilina nazo, lakini bado hali ilivyo ni kama hatujajua mahala pa kuanzia.

Kwa mazingira ya utoaji elimu nchini yalivyo, lazima tukubali kuanzia mahali fulani; lazima tuanze kupambana na mzizi wa tatizo kwanza. Tukishafanikiwa kung’oa mzizi wa tatizo ni rahisi kupambana na changamoto nyingine.

Kwa mtazamo wangu, walimu bora walioandaliwa vizuri, wenye morali ya kufundisha na moyo wa kujitoa kwa dhati kwa kazi yao, ndiyo kiini cha kupatikana kwa elimu bora Tanzania.

Ni kweli kuna changamoto nyingine nyingi lakini tukianzia na walimu ambao ndio kiungo muhimu, tutakuwa tumepiga hatua kubwa katika kupambana na changamoto za elimu.

Kwa nini nasisitiza walimu ndio mwarobaini wa elimu yetu? Historia inatuambia kuwa baadhi ya wazazi wetu walisomea chini ya miti lakini walikuwa na walimu waliowafundisha kwa moyo.

Siyo kwamba hakukuwa na changamoto kwenye sekta ya elimu.. Oktoba 22 Oktoba, mwaka 1984 wakati Mwalimu Nyerere akizungumzia kuhusu hali na changamoto za elimu Tanzania, alisema,

“ Walimu wapo kila mahali Tanzania –kwenye vijiji vyetu vyote na mijini. Malipo yao ni madogo sana, mazingira wanayoishi na wanayofanyia kazi ni magumu sana na mahitaji yao ni mengi…”

Tujikumbushe zamani

Changamoto zinazowakabili walimu zimekuwepo tangu enzi za utawala wa awamu ya kwanza pamoja na juhudi alizofanya kuboresha elimu; walau walimu wa enzi hizo waliheshimika kuanzia kwa jamii mpaka serikalini. Hii iliwapa walimu motisha na ari ya kufanya kazi kwa bidii.

Miaka ya hivi karibuni hali hii imetoweka kabisa; taaluma ya ualimu imekuwa haina mvuto mkubwa, tumesahau walimu ndio kitovu cha elimu, ndio msingi wa taaluma nyingine zote.

Tumefanya jitihada kadhaa kushughulika na changamoto nyingine, hata hivyo, bidii hizo hazijatupa suluhisho la kudumu. Madawati, madarasa, vitabu, maabara ni muhimu lakini kama hatuna walimu bora, wenye ari na moyo wa dhati wa kufundisha, bado tutabaki palepale.

Kuendelea kufanya vibaya kwa shule za umma kwenye mitihani ya taifa mwaka huu kumetajwa na wananchi wengi kuwa kunatokana na mazingira magumu wanayoishi walimu.

Utafiti uliofanywa na shirika la HakiElimu mwaka 2016 uliolenga kuangalia motisha kwa walimu na namna wanavyoridhika na taaluma hiyo, ulibaini wazi kuwa kiwango cha motisha kwa walimu na moyo wa kuridhia kufanya kazi ya ualimu, viko chini sana .

Mapendekezo yaliyotolewa kutokana na matokeo ya utafiti huo yanatoa wito kwa Serikali kuwekeza nguvu zaidi katika kushughulikia masuala ya walimu ikiwa ni pamoja na kuongeza kiwango cha mishahara yao, kutoa motisha kwa walimu ili waifanye kazi yao kwa ufanisi.

Mengine ni kuwajengea walimu mazingira rafiki ya kufanya kazi yao hasa walimu wanaofundisha shule za pembezoni, ikiwamo nyumba, posho ya kufanya kazi katika mazingira magumu,upatikanaji wa huduma muhimu hasa maji na umeme.

Serikali ya Awamu ya Tano imeanza kutekeleza kwa vitendo baadhi ya mapendekezo hayo kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu, kama alivyosema Naibu Waziri wa nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) Selemani Jafo hivi karibuni bungeni.

Alisema katika mwaka wa fedha 2016/2017, Serikali imetenga Sh3.9 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu 1,157 kwa shule za msingi na Sh11.14 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu 661 wa shule za sekondari. Pia italipa deni la Sh26.04 bilioni kwa walimu walioko kazini na wastaafu. Hata hivyo swali la kujiuliza; je, ahadi hizi zitatimizwa?

Ikumbukwe kuwa kuyapa kipaumbele masuala haya kutasaidia kutarejesha hadhi ya mwalimu na kuifanya taaluma hii mama kuthaminiwa na kuheshimika tena.

Benedicta Mrema ni Ofisa programu kutoka Idara ya Habari na Utetezi, HakiElimu na anapatikana kwa baruapepe: [email protected]