Mazingira yanavyochangia ufaulu shule binafsi

Hiki ni chumba kinachotumiwa na wanafunzi wa bweni katika Shule ya Sekondari ya Feza ya jijini Dar es Salaam
Muktasari:
Lilikuwa jambo gumu kwa Congcong Wang kutambua walichokuwa wakimaanisha wazazi wake walipokuwa wakijadiliana kuhusu shule ya kumpeleka kusoma.
Lilikuwa jambo gumu kwa Congcong Wang kutambua walichokuwa wakimaanisha wazazi wake walipokuwa wakijadiliana kuhusu shule ya kumpeleka kusoma.
Alichoshindwa kukielewa kipindi hicho ni maneno; shule yenye mazingira mazuri. Ni mpaka alipoandikishwa katika moja ya shule zenye mazingira mazuri nchini, ndipo ufahamu ulipomjia wa nini hasa wazazi wake walimaanisha.
Anasema ufahamu huo ulimjia baada ya kutazama picha za shule mbalimbali nchini na kuzilinganisha na Shule ya Wasichana ya Feza aliyokuwa akisoma kwa ngazi ya sekondari.
Kwa sababu ya kuwa katika shule ya aina hiyo, Congcong, aliyeshika nafasi ya pili kitaifa katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne yaliyotoka hivi karibuni, anasema hakuwa na sababu ya kutofanya vizuri katika mazingira mazuri ya kitaaluma yaliyomzunguka.
“Tangu nilipokuwa Feza shule ya msingi mazingira yalikuwa mazuri, nilipokuja huku (sekondari) ndiyo usiseme kuna kila kitu, Sikumbuki mara ya mwisho kufua ni lini, nakula chakula kizuri nafurahi, ndiyo maana nasoma kwa bidii na kuelewa masomo, ”anasema.
Kwa hakika Shule ya Wasichana ya Feza iliyopo mkoani Dar es Salaam, ina sababu zote za kuwa katika orodha ya shule zenye mazingira bora ya kujifunzia nchini.
Hivi ndivyo zilivyo shule nyingi binafsi zikiwamo zilizoingia katika orodha ya shule 10 bora katika matokeo hayo. Pamoja na wazazi kulipa mamilioni ya fedha kama ada, kiwango hicho kikubwa cha ada kinarandana na mazingira na huduma zinazotolewa katika shule hizo.
Mwanafunzi aliyeshika nafasi ya tatu, Innocent Lawrence anasema kwa kiasi kikubwa utulivu wa mazingira ya kusomea katika shule aliyokuwa akisoma umemsaidia kufikia mafanikio aliyopata.
Lawrence aliyehitimu kutoka Shule ya Wavulana ya Feza, pia ya mkoani Dar es Salaam, anasema; “Napenda mpira wa miguu tangu nikiwa mdogo, hivyo nilipofika hapa na kukuta kuna kiwanja na kuna siku maalumu ya michezo, nilifurahi. Napata muda wa kujisomea, kucheza, nakula vizuri, nalala pazuri, sina sababu ya kufeli hata moja.’’
Anaongeza: “Mazingira mazuri ndiyo kila kitu asikuambie mtu, kama chakula kibovu, huna uhakika wa kukipata kwa maana mnagombania, sehemu ya kulala siyo ya kuridhisha, akili itakuwa inawaza vitu vingi kwa wakati mmoja. Lakini hapa ninaposoma ninawaza masomo tu, kila kitu kipo na siyo jukumu langu, kufahamu ninakula nini kwa sababu napata kila kitu.
Wasemavyo wadau wa elimu
Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, John Kalaghe anasema wingi wa shule hausaidii kama hazitokuwa na mazingira rafiki ya kufundishia na kujifunzia.
Anasema baadhi ya masomo yanahitaji kuwapo kwa vitu tofauti vya kujifunzia kama maabara za kisasa na kwa wanafunzi wanaoishi bweni, lazima wawe na uhakika na mazingira yanayowazunguka, kitu anachosema kinakosekana katika shule nyingi nchini.
“Kama mazingira ya kusomea na ya shule kwa jumla ni utulivu, kila kitu muhimu kwa masomo kinapatikana kama malazi bora, chakula bora, kila mtu anatumia kitabu chake, kompyuta yake, walimu wanalipwa vizuri, naamini hakutakuwa na anguko la ufaulu, anaeleza.