Kusoma, kuhesabu kunavyowasumbua wanafunzi shule za msingi

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Kwetui iliyopo wilayani Lushoto wakijisomea katika Maktaba ya kijamii. Picha na Maktaba
Muktasari:
- Miaka mitatu ya kufanya utafiti kuhusu uwezo wa wanafunzi wa shule za msingi katika stadi za kusoma na kuhesabu, matokeo yanaonyesha wanafunzi wengi wakiwamo wahitimu wa darasa la saba hawamudu kusoma na kufanya hesabu kwa ukamilifu
Tangu mwaka 2010, taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Twaweza kupitia mradi wake wa Uwezo, imekuwa ikifanya tafiti katika nchi za Afrika Mashariki zinazolenga kubaini uwezo wa watoto wa shule za msingi katika stadi za kusoma na kuhesabu.
Majaribio haya, yamekuwa yakihusisha masomo ya Hesabu na lugha za Kiswahili na Kiingereza kwa ngazi ya darasa la pili. Sampuli hujumuisha wanafunzi wa darasa la tatu na darasa la saba.
Sampuli ya washiriki
Takwimu zinaonyesha kuwa, mwaka 2010 watoto walioshirikishwa kwenye utafii huo walikuwa 37,683 mwaka 2011 wanafunzi 114,761 na mwaka 2012 wanafunzi walioshiriki ni 104,568.
Kwa upande wa kaya, mwaka 2010 zilishiriki kaya 18,952 mwaka 2011 zilikuwa kaya 59,992 na mwaka 2012 kaya. 55,191. Kwa wilaya, mwaka 2010 zilishiriki Wilaya 38, mwaka 2011 zilikuwa wilaya 119 na mwaka 2012 wilaya 126.
Shule zilizoshiriki kwenye utafiti uliofanyika mwaka 2010 zilikuwa ni 1,010 mwaka 2011 zilikuwa 3,709 na mwaka jana zikawa 3,624.
Mratibu wa Uwezo upande wa Tanzania, Zaida Mgalla anasema aghlabu majaribio hayo hutayarishwa kwa pamoja na wataalamu wa masomo kutoka vyuo vikuu, Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na walimu wa masomo husika wa darasa la pili.
Matokeo 2010
Utafiti huu ulipofanywa mwaka 2010 ulionyesha kuwa, japo Kiswahili ni lugha inayozungumzwa kwa upana zaidi nchini, idadi kubwa ya watoto hawawezi kusoma kupitia lugha hiyo.
“Kwenye sampuli zetu, chini ya nusu (42.2 asilimia) ya watoto waliofanyiwa uchunguzi waliweza kusoma kwa hatua ya hadithi. Wakati watoto wote katika darasa la tatu wanapaswa kuweza kusoma hadithi ya ngazi ya darasa la pili, watoto chini ya mmoja kati ya watatu (32.7 asilimia) ndio wanaweza.
‘’Hata hivyo, hadi wanamaliza shule ya msingi, mtoto mmoja kati ya 5 hawezi kusoma hadithi ya ngazi ya darasa la pili, licha ya kumaliza miaka saba ya elimu ya msingi,”inasema sehemu ya utafiti huo.
Kwa upande wa Kiingereza, ripoti hiyo ya mwaka 2010 inaonyesha kuwa chini ya mwanafunzi mmoja kati ya 10 (7.7 asilimia) ndio anayeweza kusoma hadhithi ya Kiingereza ya ngazi ya darasa la pili.
Inasema kuwa, watoto wengi wanafika darasa la saba bila kuwa na stadi zozote za Kiingereza, kama ripoti inavyofafanua:
“Hadi wanamaliza shule ya msingi, nusu ya wanafunzi (49.1 asilimia) bado hawawezi kusoma hadithi ya kiwango cha darasa la pili ya Kiingereza,”
Kwa upande wa hesabu, ripoti inasema kuwa, zaidi ya nusu ya wanafunzi hawawezi hata kufanya hesabu rahisi za kujumlisha.
“Hadi kipindi wanafika darasa la tano, watoto wengi wanaweza kutoa na kujumlisha, wengi bado hawawezi kuzidisha,” inasema.
Inaeleza kuwa, watoto watatu kati 10 (31.5 asilimia) wa darasa la saba hawawezi kufanya hesabu za kuzidisha za ngazi ya darasa la pili.
Matokeo 2011
Kwa utafiti wa mwaka 2011, unaonyesha kuwa ni watoto watatu tu kati ya 10 wa darasa la tatu, wanaoweza kusoma hadhithi fupi za darasa la pili.
Kwa somo la Kiingereza, ripoti hiyo inasema kuwa ni mtoto mmoja tu kati ya 10 wa darasa la tatu anayeweza kusoma hadithi ya darasa la pili.
Kuhusu hesabu, ripoti ya utafiti huo inaonyesha kwamba, ni watoto watatu tu kati ya 10 wa darasa la tatu wanaoweza kufanya hesabu ya darasa la pili.
Matokeo 2012
Aidha, ripoti ilibaini asilimia 24 ya wanafunzi wa darasa la saba hawawezi kusoma hadithi ya Kiswahili ya darasa la pili, huku asilimia 50 ya wanafunzi hao, wakiwa hawawezi kusoma hadithi ya rahisi ya Kingereza ya darasa la pili.
Inaeleza kuwa, asilimia 11 ya wanafunzi wa darasa la saba hawawezi kufanya hesabu rahisi ya darasa la pili.
Kwa upande wa darasa la tatu, utafiti huo unaonyesha kuwa, ni mtoto mmoja tu kati ya wanne wa darasa la tatu sawa na asilimia 26 aliwezi kusoma hadithi ya darasa la pili ya somo la Kiswahili.
Kwa upande wa somo la Kingereza, ripoti hiyo inaonyesha kuwa ni mtoto mmoja tu kati ya 10 sawa na asilimia 13 ndiyo aliyeweza kusoma hadithi ya Kingereza ya darasa la pili.
Kwa upande wa hesabu, utafiti huo unaonyesha kuwa ni watoto wanne tu kati ya 10 wa darasa la tatu ambao ni sawa na asilimia 44, walioweza kufanya hesabu ya darasa la pili.
Mkuu wa Twaweza, Rakesh Rajani, anasema kuwa wameamua kutumia kigezo cha majaribio ya darasa la pili kwa sababu, mtalaa wa elimu unaelekeza kuwa, mtoto akivuka darasa la pili awe na misingi ya stadi za kuhesabu, kuandika na kusoma (KKK).
Sehemu ya muhtasari wa ripoti ya utafiti huo, inasema ingawa kila mtoto nchini anayesoma darasa la tatu au zaidi anapaswa kuwa na uwezo wa kusoma na kuandika vitu vya darasa la pili, ukweli ni kuwa lengo hili halifikiwi.
“Katika miaka mitatu iliyopita, uwezo wa kusoma na kuandika umebaki chini na kwa kiasi kikubwa haujabadilika ingawa uwezo wao wa hesabu umeonyesha kuboreka kidogo,” inasema sehemu ya ripoti hiyo.