Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Unaogopa kumwambia mwenza ananuka kwapa, kinywa?

Umewahi kuwa kwenye uhusiano na mtu anayetoa harufu mbaya ya kinywa au mwili? Mara nyingi watu wanaokutana na adha hizo kwa wenza wao, hujikuta wakipitia wakati mgumu, kwa kuogopa kusema wakihofia maneno yao yatachukuliwaje.

Licha ya kuwepo kwa baadhi ya wanaovumilia harufu hizo, pia wapo ambao hufikia hatua ya kukimbia uhusiano wao kwa kuchoshwa na harufu mbaya kutoka kwa wenza wao, bila kufahamu kuwa zipo njia sahihi za kuzungumzia tatizo hilo.

Akizungumza na Mwananchi, Emmanuel Samwel, mkazi wa Tabata Kimanga jijini Dar es Salaam anasema hawezi kumwambia mwenza wake udhaifu huo, kwani unaweza kumwathiri kisaikolojia.

"Aisee siwezi kumwambia mpenzi wangu kuwa anatoa harufu mbaya, yaani siwezi kwa sababu ataanza kuniogopa. Kwanza ni aibu, siwezi, ni bora niachane naye," anasema Emmanuel.

Naye Beatrice Sebastian, mkazi wa Makongo Juu jijini humo, anasema hiyo ni changamoto anayopitia sasa, lakini hajui njia zipi za kumsaidia mwenza wake.

"Hili suala limekuja wakati sahihi, mimi mpenzi wangu anasumbuliwa na tatizo la kutoa harufu kwenye kinywa. Lakini naogopa kumwambia nawaza atanifikiriaje. Nahofia isijekuwa ndiyo mwisho wa uhusiano wetu, kwa kweli napitia wakati mgumu," anasema Beatrice.

Kwa upande wake, Erick Marwa anasema ni vyema kuzungumza kuliko kukalia kimya matatizo kama hayo.

"Mimi siwezi kuvumilia, kwanza ni bora kuzungumza. Kwa upande wangu siyo tu harufu, hata kitu chochote ninaweza kumwambia. Lakini kwa lengo la kumsaidia na siyo kumuaibisha. Kikubwa ni kuangalia njia nzuri ambazo ninaweza kuzitumia bila kumfanya aniogope,"anasema.


Wanachosema wanasaikolojia

Akizungumza na Mwananchi, mtaalamu wa saikolojia, Modesta Kimonga anasema vitendo ni njia sahihi ya kufikisha ujumbe bila kuharibu hisia za mwingine.

"Kuna njia mbili, ya maneno na matendo, zote hizo ni tiba na zinasaidia. Kwa hiyo kisaikolojia kama mtu atakuwa na uwezo wa kumfanyia mtu matendo, ni bora afanye hivyo. Kwa sababu yanaweza kuashiria maneno. Kama mpenzi wake ana changamoto ya kinywa anaweza akamnunulia dawa za kinywa nzuri, anazojua akitumia anaweza akasaidika.

"Mwanzo afanye hivyo, naamini hicho ni kitu kinachosaidia sana. Kama changamoto ni harufu ya mwili, anaweza kumnunulia vitu ambavyo vinaweza kusaidia kutatua shida hiyo. Kama vile sabuni, 'deodorant' na hata manukato mazuri badala ya kutumia maneno makali,"anasema.

Anasema lengo la uhusiano ni kujenga, ni vizuri watu wakatafuta kauli nzuri, njema za upole na unyenyekevu bila kuumiza hisia za wenza wao.

Dk Magolanga Shagembe, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais wa Chama cha Wanasaikolojia Tanzania (TAPA), anasema kabla ya kumwambia mwenza kwa maneno, ni vizuri kutengeneza mazingira ya kuonekana yupo sehemu ya suluhisho.

“Kama inahusiana na harufu mbaya ya kinywa, anaweza kufikisha ujumbe kwa vitendo. Kupitia matendo, majadiliano yanaweza yakaanzia hapo, wakati mwenza anashukuru mnaweza mkaanza kuambiana.

“Ili asijisikie vibaya mnaweza mkawa mnatumia wote, ili mhusika anayetoa harufu asijihisi kutengwa. Unapolazimika kumweleza, usiku ni muda mzuri, ambapo mpo katika mazingira ya upendo na furaha, msijadili nyakati za ugomvi au mbele za watu,” anasema Dk Magolanga.


Sababu za harufu mbaya mwilini

Dk Happiness Biyengo anasema harufu mbaya mwilini ambayo huhusiana na jasho la mwili, ni tatizo ambalo kitaalamu hufahamika kwa jina la ‘Bromhidrosis’ au ‘Osmidrosis’.

Anasema ngozi ya binadamu ina aina mbili za tezi zinazohusika na kutoa jasho, ambazo huitwa ‘apocrine’ na ‘eccrine’ na tezi hizi huhusishwa na harufu mbaya mwilini, ingawa apocrine huchukua nafasi kubwa zaidi.

“Tezi za ‘apocrine’ hupatikana sehemu za kwapani, chini ya matiti na sehemu za siri. Jasho inapotoka kwenye tezi hii haina rangi wala harufu hadi pale inapoingiliwa na bakteria waishio kwenye ngozi. Tezi hizi huanza kufanya kazi hasa katika umri wa kubalehe na hii ndiyo sababu tatizo la harufu mbaya husumbua zaidi kundi la vijana,” anasema na kuongeza:

“Eccrine hupatikana sehemu zote za mwili, pia zenyewe hutoa jasho lisilo na rangi wala harufu, na mara nyingine hutoa jasho la harufu ya vyakula ambavyo mtu anaweza akawa amekula kama vitunguu swaumu, pombe, sigara na baadhi ya dawa.’’

Dk Happiness anaeleza mtu kutokuwa na usafi binafsi kama kusafisha mwili mara kwa mara, kuvaa nguo chafu, maambukizi ya vijidudu kwenye ngozi au vinyweleo vya ngozi, ni sababu ya kuwepo kwa tatizo hilo.


Chanzo cha harufu mbaya kinywani

Daktari wa kinywa, Gillberth Lema anasema magonjwa ya kinywa yanasababishwa na mabaki ya chakula kwa kuwa mwili wa binadamu una bakteria ambao hutoa tindikali inayosababisha magonjwa ya fizi na kinywa.

“Vitu vyenye sukari, ikiwemo sukari ya kawaida pia huchochea tatizo hili, lakini mpangilio wa meno katika kinywa huhifadhi mabaki na kuleta harufu mbaya," anaeleza.

Anaeleza kuwa tatizo hili pia huchangiwa na bakteria wanaojificha kati ya jino na jino na mwingine kama ana jino lililotoboka, vijidudu hivi hutumia nafasi ya kujificha humo.

“Lakini wale ambao wana tabia ya kulala mdomo wazi, tabaka la juu la ngozi ya mdomo huoza na kutoa harufu mbaya. Chanzo kingine kikuu cha harufu mbaya ya kinywa ni pale ambapo chakula kingi kinabaki mdomoni, hasa nyama,’’ anasema.


Usafi kwa wenza

Usafi ni jambo la msingi katika maisha ya ndoa na uhusiano wa kimapenzi, na unaweza kuwa na athari kubwa kwa furaha, ustawi, na uimara wa uhusiano huo.

Kwa wenza, kuzingatia usafi siyo tu suala la mwonekano wa nje, bali pia linaathiri hisia, afya ya kihisia, na mawasiliano kati yao.

Usafi unajumuisha mambo mengi, ikiwemo usafi wa mwili na mazingira ya nyumbani. Hivyo, ni muhimu kwa wenza kuwa na tabia ya kujali usafi ili kuimarisha uhusiano wao na kuhakikisha kuwa wanakuwa na ndoa yenye furaha, afya na utulivu.

Usafi wa mwili ni kipengele muhimu katika kudumisha mvuto na heshima kati ya wenza. Wakati mpenzi wako anapojali usafi wake wa mwili, inatoa ishara ya kujitunza na kujali mwenzake.

Kwa mfano, kuoga mara kwa mara, kuvaa mavazi safi, na kutumia manukato ni njia za kuonyesha kujali kwa mwenzako. Hii inajenga mvuto wa kimapenzi na kuleta hisia nzuri kati ya wenza. Pia, usafi wa mwili huchangia katika afya ya mwili na kupunguza uwezekano wa magonjwa ya ngozi au maambukizi, jambo ambalo ni muhimu kwa kudumisha uhusiano wenye afya.

Usafi wa mazingira ni kipengele kingine cha muhimu katika maisha ya wenza. Nyumba inayokuwa safi na inayoshughulikiwa vizuri inajenga mazingira ya amani na starehe kwa wanandoa.

Wenza wanapoishi katika mazingira yasiyo na uchafu au mikusanyiko ya vichafu, huwa na uhuru wa kuzungumza na kuungana kwa utulivu.

 Mazingira safi pia yanaathiri hali ya akili, kwani uchafu mara nyingi huleta hisia za msongo na uchovu wa kiakili. Hivyo, kuzingatia usafi wa nyumba ni muhimu kwa uhusiano mzuri na ushirikiano wa kila siku.

Ikumbukwe usafi ni muhimu sana kwa wenza kwa sababu unahusiana na afya ya mwili, akili, na mazingira.

Uhusiano wenye usafi wa mwili na mazingira unachangia katika kujenga mazingira mazuri kwa furaha, mapenzi na ushirikiano.

Vilevile, usafi wa kiakili na kihisia unasaidia wenza kuwa na ndoa yenye afya, utulivu na uwezo wa kushinda changamoto.

Kwa hiyo, wenza wanapaswa kuzingatia na kujali usafi katika nyanja zote ili kuimarisha uhusiano wao na kuleta furaha ya kudumu.