Prime
Unalea au unawafuga watoto?

Muktasari:
- Ingawa silengi kubeza umuhimu wa nidhamu na utii katika malezi, nafikiri ipo haja ya kuwaruhusu watoto kuwa na kiasi fulani cha uhuru wa kufikiri, kuchagua na hata kufanya makosa.
Kila siku saa 12 jioni, Mah’mood mwenye miaka 12 hutoka shule anakosoma moja kwa moja kwenda nyumbani.
Mah’mood anawajua wazazi. Hawawezi kuthubutu kumruhusu kuchelewa nyumbani hata dakika tano. Jaribio lolote la kuchelewa litakaribisha matusi, ukali, na ikibidi kiboko bila maelezo yoyote.
Mah’mood anatamani kuwa mchezaji hodari wa mpira. Ndoto hii imekatishwa baba yake alimwambia, “Hutakula mpira, soma uwe mwanasheria. Hutaki acha shule.
Kila Mah’mood anapouliza swali, jibu huwa ni kama limerekodiwa mahali, “nyamaza, wewe ni mtoto.” Kadiri miaka inavyoenda, Mah’mood alizidi kuwa mnyonge na kujiamini kwake. Ukiongea na Mah’mood unaweza kuhisi ni jasiri. Lakini ukisikiliza vizuri unagundua ana unyonge unaoua utu wake, ndoto zake, na uhuru wa kuwa yeye.
Je, haya ni malezi au ufugaji? Je, Mah’mood analelewa au anaishi na wazazi wake kama mfugo? Jamii zetu zinaamini mno katika utii na nidhamu.
Tunafikiri bila nidhamu iliyopindukia, utii usiohoji basi mtoto hawezi kufanikiwa. Ingawa silengi kubeza umuhimu wa nidhamu na utii katika malezi, nafikiri ipo haja ya kuwaruhusu watoto kuwa na kiasi fulani cha uhuru wa kufikiri, kuchagua na hata kufanya makosa. Kulea maana yake ni kulinda uhuru huo, na kufuga, kama ilivyo kwa Mah’mood ni kumnyima mtoto nafasi ya kufikiri, kujieleza, kuchagua, na hata kufanya makosa ili ajifunze. Hebu tutazame tofauti ya malezi na ufugaji wa watoto katika maneno matano makubwa.
Uhuru wa fikra
Uhuru wa mtu kufikiri ndio utu wake. Malezi bora hulenga kukuza uwezo wa mtoto kufikiri bila utegemezi uliopitiliza kwa mzazi. Ufugaji, tofauti na malezi, ni kumnyima mtoto uhuru wa kufikiri hali inayomnyang’anya na kutweza utu wake.
“Unajua unaongea na nani?”
“Unataka kuniongoza?”
“Ondoka hapa haraka!” Hii ni mifano ya kauli za mzazi anayeamini katika ufugaji wa watoto. Ukiendekeza ufugaji wa hivi watoto hukua wakiwa na hofu, wanyonge wasiojiamini.
Utii bila nidhamu
Nidhamu sio kuogopa adhabu. Unaweza kumwogopa mtu usiyemheshimu. Mzazi anayefuga watoto huridhika mtoto anapokuwa mtii kupitiliza.
“Nimekuambia fanya!”
“Sitaki maswali hapa.” Unaweza kuona namna kauli hizi zinavyomchukulia mtoto kama mfugo usio na uwezo wa kudadisi chochote.
Mtoto hukua bila uwezo wa kupambanua mambo au kufanya uamuzi wa kina. Ukimlea mtoto kuwa na nidhamu, anakuwa na uwezo wa kuelewa anachopaswa kufanya na kujiepusha na chochote kinachomtoa kwenye mstari bila woga wa adhabu.
Kumtumia mtoto kutimiza ndoto
Namfahamu mzazi mmoja aliyekuwa na ndoto ya kuwa daktari lakini kwa bahati mbaya hakufanikiwa. Mzazi huyu alimshinikiza kijana wake kusomea udaktari kama namna ya kufidia ombwe la kutotimiza ndoto zake.
Huu sasa ndio ufugaji. Unapima mafanikio ya mtoto kwa viwango vyako mwenyewe. Mtoto mwenye kipaji cha sanaa analazimishwa kuwa mwanasheria.
Tunaathiri mno afya ya akili ya watoto wengi kwa tabia hii. Malezi ni kumuongoza mtoto kujua anataka nini na kumwekea mazingira ya kufikia ndoto alizonazo.
Kumuamulia mtoto
Hili ni gumu lakini acha niliseme. Unajisikiaje mtoto akiamua kuwa na dini tofauti na dini yako wewe mzazi? Mzazi mfugaji hawezi kutambua haki ya mtoto kufanya uamuzi ikiwa pamoja na dini anayoitaka. Huamini anachokichagua yeye ndicho kinachopaswa kuchaguliwa na mtoto.
Ingawa ni kweli tunatamani watoto wafuate njia zetu kiimani lakini ni muhimu kuelewa kuwa mtoto naye kadri anavyokua hufikia pahala akafanya uamuzi unaokidhi itikadi zake, mazingira yake, ufahamu wake, uelewa wake ambayo si lazima iwe ‘kopi’ ya misimamo ya mzazi.
Kumdhibiti kupitiliza
Unapokuwa na misimamo mikali sana unamweka mtoto kwenye hatari ya kutengeneza sura mbili wakati mwingine zinazokinzana.
Mtoto anakuwa na sura bandia ya kumuonesha mzazi, lakini pia anakuwa na sura yake halisi anayokuwa nayo akiwa na wenzake mitaani. Huu sasa ndio unaitwa ufugaji wa watoto kwa maana ya kuwanyima watoto raha ya kuishi uhalisia wao.
Malezi, tofauti na ufugaji, yanalenga kumsaidia mtoto kujitambua, kufurahia utoto wake, kufanya uamuzi wenye kiwango fulani cha uhuru bila kuogopa wengine wanasemaje.
Hitimisho
Kulea ni kumsaidia mtoto akue akiwa mtu kamili — mwenye akili, hisia, na sauti yake. Kufuga ni kumbana mtoto kwa hofu, ukimya, na utii wa lazima.
Tofauti hii ni ndogo kwa nje, lakini ina athari kubwa sana kwa maisha ya mtoto kwa muda mrefu.
Mah’mood tuliyeanza naye angeweza kuwa mchezaji mkubwa leo, kama angetunzwa, kuelekezwa na kusikilizwa.
Haitakuwa ajabu Mah’mood kuishia kuishi maisha yasiyo na amani yenye shinikizo kubwa la kuwafurahisha watu.