Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Umejiuliza ulionao ni watoto au mitoto?

Muktasari:

  • Kuna tofauti kubwa kati ya kuwa na watoto na kuwachukulia kama watoto na kuwa na mitoto. Watoto ni binadamu — wenye utu, mahitaji ya kihisia, na uwezo wa kufanya kitu.



“Wenzangu nyie mnafanyaje watoto wawasikilize?” analalamika mama Rehema.

“Hata sijui nilimkosea nini Mungu! Hii niliyonayo ni mitoto.”

Namuuliza kwa nini?

Kama mtu asiyeamini anaulizwa swali la kijinga ananijibu: “Haina akli, mijinga, mitundu, mikorofi, pasua kichwa kazi kunitia hasara tu,” anasema kwa hasira.

Kanisimulia juzi kwenye mtihani wa nusu muhula mwanae mkubwa kawa wa 38 kati ya watoto 40 darasani.

“Huwezi amini hata sijashangaa. Mtoto wa Asha kapata A anawaongozea darasani!”

Kwa muda mfupi niliokaa pale kwake, watoto ni kama watumwa ni mwendo wa kelele na amri  kwenda mbele.

“Mama Rehema si ungerekodi tu amri ziwe zinatokea kwenye spika?” namwambia kwa kejeli baada ya kuona anatumia nguvu kubwa kutoa amri zile zile.

“Rehema! Unafanya nini?”

“Samweli? Hujanisikia?”

“We Rehema uko wapi hebu njoo nipe rimoti”

Mama Rehema anawakilisha tabia zetu wazazi wengi. Ingawa tunawaita ‘watoto’ lakini kiuhalisia tunawatazama watoto kama mitoto kama anavyofanya mama Rehema.

Kuna tofauti kubwa kati ya kuwa na watoto na kuwachukulia kama watoto na kuwa na mitoto. Watoto ni binadamu — wenye utu, mahitaji ya kihisia, na uwezo wa kufanya kitu.

Mitoto, tofauti na watoto, ni dharau tunayokuwa nayo kwa watoto, tukiamini hawana uwezo, hawajielewi na hakuna kitu wanaweza kufanya tukatambua.

Je, unawachukulia ulionao kama watoto au mitoto? Hapa nakupa dalili tano kuwa unawachukulia kama mitoto.


Unawalalamikia muda wote

Ukiona kila siku unawatukana, kuwaona kero, unawasema, unawalalamikia huenda unaamini una mitoto.

Malalamiko maana yake huridhishwi na wanachokifanya. Muda wote unawachukulia kama wakosaji. Je, ni kweli kuwa watoto wako hawana jema?

Ukmheshimu mtoto kama binadamu kamili anayestahili heshima, unaweza kushangaa akakusikiiliza na kukuelewa a hutolazimika kupiga kelele, kuwarushia maneno na kuwanyanyasa kihisia.


Unawaamrisha muda wote

Unapokuwa mtu wa kutoa amri muda wote maana yake huamini mnaweza kuzungumza na mtoto mkakubaliana jambo nna likafanyika.

Muda wote, “Fanya hivi”, “Acha hiki”, “Kalale,” “Amka!”

Badala ya kuwa mlezi, unakuwa dikteta. Hakuna nafasi ya kushauriana, kuelewana au kujenga mahusiano ya karibu — ni amri tu na adhabu.

Unaweza kutengeneza mfumo mzuri unaomkumbusha mtoto wajibu wake bila muda wote kufoka na kutoa maagizo yasiyoisha.


Unawalinganisha

Sijui kama kuna asiyejua watoto hawa wako tofauti. Kwa nini unampima mtoto kwa kutumia kigezo cha mtoto mwingine? Unafoka muda wote kwa vile unatarajia wote watafikiri sawa, wataona sawa, wataamua sawa na watafaya sawa.  Je, hili linawezekana?

Mitoto inafanana. Watoto wanatofautiana. Kauli kama “tazama fulani alivyofanikiwa, wewe uko tu hapa!” humuumiza mtoto na kumpa hisia kuwa hana thamani.


Unawachukulia kama vifaa

Kuna suala la mtoto kuwajibika lakini kuna tatizo la kumchukulia mtoto kama nyenzo ya kazi. Ukishaamini thamani ya mtoto ni kazi anazofanya maana yake hiyo uliyonayo ni mitoto. Itakusumbua na hutokaa uridhike kama mama Rehema.


Hatuzai wafanyakazi wa kufua, kupika, kulima, kusaidia biashara na shughuli nyinginezo. Tunawafundisha kazi lakini watoto sio vyenzo za uzalishaji mali. Unaweza kumfundisha mtoto kuwajibika pasipo kumfanya ajione hana maana asipoweza kazi.



Huna muda nao


Huwezi kuwa na muda na mitoto. Si haisikii? Unakaa nayo mfanye nini? Ukishaamini una mitoto, ukirudi nyumbani huna haja ya kujua shuleni wamekutana na nini, siku iliendaje, kipi kilienda vyema na kipi hakikwenda sawa na walijisikiaje.


Watoto wanahitaji kupendwa, kukumbatiwa, kusikiilizwa, kucheza nao na kuwa na muda na wazazi wao. Ukishaona una watoto, utawaheshimu, utawachukulia kama watu wa maana wanaohitaji muda wako, wanaohitaji kufurahia utoto wao wakiwa na mzazi wao. Kejeli, dharau, kupuuzwa, kusimangwa ni mambo tunayoifanyia mitoto.


Hitimisho

Wazazi na walezi, watoto tulionao si mitambo ya kufanya kazi wala si viumbe vya kufurahisha nafsi zetu. Tumezaa binadamu na wao pia wanahitaji kulelewa kwa heshima, mapenzi, na uelewa.

Kabla hujasema “mitoto yangu,” jiulize: Je, unawalea kwa utu? Unawawekea mazingira ya kuaminii nao ni watu? Ulionao si mitoto. Mungu alikupa watoto na wanastahili kulelewa kwa staha wawe watu wazima wanaojiheshimu.