Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Unafahamu masaibu anayopitia mwanao na hakuambii wewe mzazi?

Kama sehemu ya wajibu wangu wa kitaaluma, huwa ninaandaa, kuendesha na kutathmini mafunzo ya ulinzi wa mtoto kwa walimu, wanafunzi na wazazi kwenye shule mbalimbali.

Nimeendesha mafunzo hayo kwa shule nyingi, hususan za binafsi na zile zinazoendeshwa na mashirika binafsi na kidini.

Hivi karibuni nilipata bahati hiyo kwenye shule kubwa inayoendeshwa na shirika la kitawa.

 Imani tuliyonayo wazazi wengi kwa shule hizi ni mfumo madhubuti wa malezi unaowahakikishia watoto usalama wao.

Ingawa ni kweli matarajio ya wazazi wengi ni ufaulu mzuri, hili la malezi yenye kumjenga mtoto kimaadili ni kubwa zaidi.

Siku hiyo, Ijumaa, kabla ya kuzungumza na wazazi Jumamosi yake, nilipata wasaa wa kusema na watoto wa kidato cha kwanza na cha pili.

Madhumuni ya kuanza na watoto ni kupata uzoefu halisi ninaoweza kuutumia kama rejea kwenye mazungumzo na wazazi.

Nafahamu sisi wazazi huwa hatupokei jambo kirahisi, hasa linapoonekana halina uhalisia. Ninapokuwa na mifano halisi ya uzoefu wa watoto mapokeo yanakuwa makubwa.

Basi mazungumzo yangu na watoto Ijumaa hiyo yalichukua takribani saa nne. Kwa kawaida, mazungumzo haya huwa shirikishi kwa utaratibu unaolinda faragha ya mtoto na pale inapowezekana tunazungumza kwa uwazi kama mjadala.

Niligawa vikaratasi vidogo vyenye rangi mbalimbali vinavyofahamika kama ‘sticky notes.’ Rangi tofauti zilikuwa alama ya siri kuwakilisha darasa la mwanafunzi. Swali mojawapo nililouliza ni: “Ukiwa na jambo linalokusumbua, huwa unakwenda kwa nani ukiwa hapa shuleni?”

Nikafafanua kuweka muktadha kidogo, “Unapohitaji msaada kwa jambo la faragha na linakunyima amani, unamwamini nani anayeweza kukusaidia?” Hapa mtoto alipaswa kutaja jina (kama angependa) au kutoa maelezo ya jumla tu.

Swali lililofuata ni kumtaja mtu wanayeweza kumwamini katika mazingira ya nyumbani. Nilibashiri kuwa wangemtaja mzazi mmojawapo kuonesha ukaribu walionao na wazazi. Kinyume na matarajio uchambuzi wa taarifa hizi ulinishtua.

Katika watoto 10, kwa mfano, ni mmoja tu alimtaja mwalimu na wawili tu walimtaja mzazi kwa mazingira ya nyumbani. Watoto wengi walisema wanakimbilia kwa rafiki au mtu mwingine yeyote asiye sehemu ya familia.


Siri za watoto

Aidha, niliuliza swali jingine nyeti. “Una siri gani inayokusumbua na kukunyima amani na hujawahi kumwambia mtu na hutarajii kumwambia mtu kirahisi?”

Hapa nililenga kujua watoto wamehifadhi nini kwenye mioyo yao? Uchambuzi wa vikaratasi vile ulinitia simanzi. Naomba kunukuu vichache.

“Sijawahi kumwambia mtu yeyote kuwa nilifanyiwa ukatili wa kingono na kaka yangu wa damu miaka miwili iliyopita.”

“Niliwahi kufanya ngono na dada yangu na kaka yangu mdogo niliozaliwa nao.”

“Huwa kuna kitu kinaniambia kuwa niliwahi kulala na mpwa wangu lakini huwa najikatalia. Wazo hili huwa linanisumbua sana na kuna wakati natamani nirudi utotoni ili nipate ukweli nyuma ya hisia hizi.”

“Kushikwa matiti na baba. Kulazimishwa kumbusu mjomba na kukatazwa kusema kwa mama.”

“Siwezi kumwambia mtu kuhusu vitendo nilivyofanyiwia na dada wa kazi (housegirl) nilipokuwa mdogo.”

“Kupoteza usichana wangu nilipokuwa na miaka sita. Manyanyaso, masumbuko ya familia yangu kutokana na kutengana kwa familia na sisi watoto kutokupata malezi bora kama watoto.”

Haya, kwa hakika, ni mambo mazito na mikono inatetemeka ninapoyaandika. Najua naingilia faragha ya watoto hawa kuyasema haya, lakini niliwaomba nitumie mifano nitakayokutana nayo kwenye mazungumzo yangu na wazazi. Ukweli ni kwamba watoto wanapitia masaibu mazito.

Kesho yake tulizungumza na wazazi. Mazungumzo yalianza na baadhi ya nukuu nilizowaambia nimezitoa kwa watoto wao wenyewe.

“Huenda ni mwanangu masikini!” alisema mzazi mmoja kwa hofu kubwa.

“Tunafanya nini kuwalinda watoto wetu?” Hicho kikawa ndio kiini cha mazungumzo yetu yaliyotawaliwa na hisia kali. Kikao kiliibua mengi kuhusu usalama wa mtoto.

Tulihitimisha kuwa ukatili mkubwa wa kingono unafanyikia kwenye mazingira ya nyumbani. Ukitizama mifano hiyo niliyoitaja, watu ambao tungetarajia wawe walinzi wa mtoto, ndio hao hao, wanaweza kugeuka kuwa shubiri kwa usalama wa mtoto.

Tunayo kila sababu ya kuchukua hatua.

Pamoja na kuwa karibu na watoto kadri inavyowezekana, kwa maana ya kuwa na muda nao ili watuamini, ni muhimu kuondoa mazingira hatarishi yanayoweza kuwafanya watoto wakafanyiwa (na hata kufanyiana) vitendo hatarishi.