TUONGEE KIUME: Maisha katikati ya ujana na uzee yanavyopasua kichwa

Kuna wakati kwenye maisha ambapo mwanaume anajikuta katikati ya kujiona kijana na mzee. Kipindi hiki, nafsi na moyo unatamani kuishi maisha ya ujana lakini mwili, akili yako na hali ya maisha inakukumbusha wewe ni mtu mzima. Leo tuongee kiume kuhusu hii hali ya kushindwa kuchagua kati ya kuchomekea kwa kuulambia mkanda nje au kuvaa suruali za kubana na mlegezo.
Wanaume wengi tunakumbwa na hali hii kwenye miaka 30 au 40. Wakati huu, baadhi yetu tunaanza kuona nywele nyeupe zikijipenyeza kichwani kama wageni waliovamia shughuli. Unakimbilia saluni, unapiga kipara ili kuzificha, lakini wapi, unaona kama vile kipara ndo kinakuzeesha zaidi, mwisho wa siku unaamua kunyoa mitindo ya ujana na kuweka super black nyingiiiii ili imradi tu nafsi yako ijisikie ujana.
Hali hii pia inakuja na hamu ya ghafla ya kupenda kwenda ‘gym’. Ghafla unajikuta unaanza kuruka kamba, kupiga push up, kufanya jogging na kubeba vyuma utadhani unajiandaa na kushiriki mashindano ya Mr. Tanzania huku lengo lako likiwa sio kuwa na afya bora bali kuonekana kijana.
Unataka kuwa na six pack, kifua kizuri, mikono mikubwa ili tu ukivaa t-shirt zikupendeze. Lakini wakati nafsi na moyo wako unakwambia kwamba wewe ni kijana na unahitaji kuonekana hivyo, mwili wako unakukumbusha kuwa wewe ni mzee kwa kukupa maumivu ya mgongo na kiuno kuliko kawaida.
Si ajabu ukajikuta dukani unatafuta suruali za jeans za kubana na za kuchanikachanika, nafsi na moyo wako ukikuaminisha kwa umri wako unatakiwa kuvaa hivi. Lakini ukishanunua nguo hizo, unaanza kukosa kujiamini unapozivaa, unahisi kama watu wanakutazama na kukujadili wakisema, ‘muone yule naye mtu mzima hovyo. Mzee mzima kuvaa nguo suruali modo za kuchanika ndio nini?”
Kuna pia wanaume ambao nafsi na roho zao zinawaambia wao vijana hivyo wanatakiwa kusikiliza muziki wa ujana. Singeli, bongofleva za kisasa na kadhalika. Lakini wakati unasikiliza nyimbo za kisasa, mistari ya ujana kama vile ‘Nakupenda, unasema una bwana wako.
Sasa nakupenda wewe na uyo bwana ako.’ inakufanya ujiulize hivi nisingekuwa natumia earphone ningeweza kusikiliza wimbo kama huu mbele za watu. Hiyo sio wewe, ni mwili wako unajaribu kukupa taarifa kwamba pengine upo katika hatua ya maisha ambayo hutakiwi tena kusikiliza muziki wa aina hii.
Kusema ukweli kipindi hiki kinachanganya sana. Kinatunyima amani wanaume wengi. Kuwa kijana unataka, na sio kutaka tu, nafsi na moyo wako unakwambia wewe ni kijana lakini uzee na utu uzima nao unakutaka. Unajikuta uko njia panda, unachanganyikiwa. Ni muhimu kuelewa kuwa hii hali ya kuwa katikati ya ujana na uzee inaweza kuwa faida kubwa kama ukiikubali na kuamua kuikumbatia kwa moyo mmoja. Kwa sababu unapoishi maisha haya ya katikati, unapata nafasi ya kufurahia vyote viwili – ujana na uzee kwa namna ya kipekee.