Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ANTI BETTIE: Mke wangu ni mlevi, ananitia aibu nifanyeje?

Habari. Sina mengi, shida yangu unisaidie nimwambie nini mwenza wangu aache pombe, maana nimetumia kila aina ya vitisho, maneno na hanisikilizi.

Ukimkataza anajitetea kuwa tangu awali tulipokutana alikuwa anakunywa. Sikatai, lakini haikuwa katika kiwango cha sasa, kwani kwenye jokofu unaweza kukosa kitoweo siyo pombe.

Akipata mshahara anachofikiria ni kununua pombe na kuweka ndani, mwisho wa juma ukikataa kutoka naye anatoka mwenyewe na haoni aibu kukaa baa peke yake akinywa pombe hata mchana kweupe.


Nifanyeje Anti?

Kosa ulilifanya mlipokutana, alikuwa akinywa na pengine ulikuwa ukitoka naye. Ulichotakiwa kufanya ni kuonyesha kuzichukia tangu wakati ule lakini ulizikubali, kuzichukia sasa kunamshangaza.

Unasema amekuwa mlevi zaidi ya umjuavyo, pengine wakati ule alikuwa anakunywa kwa kujificha ficha hakutaka umjue kama mlevi mapema labda usingemuoa, ungezikataa pengine kwa sababu ya huba angeacha. Ninachokushauri kwa kuwa ulizikubali tangu mwanzo, cha kufanya mwambie apunguze taratibu na asiziweke ndani, ikiwezekana anywe mwisho wa juma pekee, badala ya kufanya hivyo kila siku.

Pia onyesha kukasirishwa kabisa pindi anapokunywa, mpunguzie baadhi ya huduma ili fedha zake ziwe na kazi ya ziada, inaonekana anazo nyingi hazina kazi ndiyo maana anazipeleka kwenye pombe.

Ila usitumie nguvu, mtakuwa mnashindana, nenda naye taratibu na kama wewe ulikuwa unakunywa acha ili umuonyeshe mfano.




Nina mpenzi muongo kupindukia


Anti ukistaajabu ya Mussa, utaona ya Firauni. Nina mpenzi wangu tunapendana sana na kila kitu ananitimizia, shida yake ni moja, uongo.

Ni mwanamume lakini muongo na kwa asili na tulivyozoea wanaume si waongo, ila huyu wangu amefuzu.

Kibaya zaidi hachagui wa kumueleza uzandiki wake, hadi watu wa familia yangu akiwapatia nafasi anawaeleza, tena mwingine wa uchonganishi.

Alianza taratibu kujisifia vitu asivyovifanya, nikaona anatamani labda kuwa na maisha fulani acha nimuache ajiotee ndoto njema, matokeo yake amekuwa sugu sasa hadi anachonganisha watu.

Nifanyeje na ninampenda na ananitimizia kila kitu.

Mapenzi siyo jambo geni kwa kila mtu mzima aliyefikisha umri wa miaka 18 na kuendelea.

Vipo vitu vingi wanandoa au wenza wanavikosea kwenye mapenzi, ninasema wanavikosea bila sababu ikiwamo uwongo. Wengi wameachika, kunusurika kuachana kwa sababu ya kusema uwongo.

Wakiulizwa sababu ya kufanya hivyo hawana, ingawa wapo baadhi hulazimika kufanya hivyo kutokana na kuwa na maasi katika mahusiano yao.

Kwa vyovyote iwavyo, uwongo haustahili katika uhusiano, ni sumu, nyoka kwenye ndimi mbili. Uongo ni miongoni mwa vitu wapendanao wanafanya kwenye mapenzi bila kujua athari zake na kusababisha wenza kuchokana au mmoja kati yao kumchoka mwenzake.

Inashangaza sana tabia hiyo, tena hakuna watu wanaonikera kama wanaume waongo, wanaowadanganya wake zao hata kwa vitu vilivyo wazi.

Nimeamua kukujibu jumla kwa sababu kumeingia ugonjwa wa wanaume kuwa waongo kwa wapenzi, wenza wao bila sababu ya msingi.

Tena ukipanda daladala ndiyo utajua jinsi gani ugonjwa huo umepamba moto, mtu hata akiulizwa upo wapi na yumo ndani ya usafiri wa umma, lakini atajibu Sinza, ilihali upo naye ndani ya gari Temeke.

Wanawake wengi wamekuwa wakiwapuuza wanaume wa namna hiyo katika hatua za awali, lakini unapozidi huchoka na huchukulia kama dharau.

Kuhusu huyo mwanaume wako nakushauri washirikishe watu wake wa karibu kwani kwa hatua aliyofikia hutoweza kumdhibiti tena.

Ameshavuka viwango vya uwongo maana anawadanganya hadi wakwe na shemeji zake.

Husisha watu wengine mzungumze naye, ikishindikana kubadili tabia yake fikiria vinginevyo, sumu ya ulimi ni kali kuliko ya nyoka. Kwa uwongo huo anaweza kuja kukusababishia matatizo mbele ya safari.

Wengi wanasema uzandiki wa mwanamume ni mbaya kuliko wa mwanamke kwa sababu anaaminiwa kiasili hawezi kusema uwongo.