Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ONGEA NA AUNT BETTIE: Tukiwa faragha sinogewi, hanogewi kama zamani nifanyeje?

Swali: Tukiwa faragha sinogewi, hanogewi kama zamani nifanyeje?

Nimejitahidi kila njia lakini mwenza wangu ni kama simridhishi faragha, kiasi imefikia hata mimi naona haniridhishi.

Kila nikifikiria ninakosea au tulikosea wapi ninashindwa kupata jibu la moja kwa moja.

Nimefikia muafaka sitaki kuumiza kichwa sana, nataka nianze upya kuhakikisha kila kitu kinakuwa sawa. Lakini sina mbinu tena kama nilipokuwa kijana, naona nishauri nifanye nini kuhakikisha mimi na mwenza wangu niliyeishi naye miaka mingi tunaridhishana faraghani.

Jibu: Kabla sijasahau ni muhimu muwe na mawasiliano mazuri, uelewa na kila mmoja kujali hisia za mwenzake.

Zungumza naye kwa uwazi kuhusu azma yako hii ukilenga kueleza matamanio yako, yaani unachotamani kitokee kuhusu kuridhishana naye mkiwa faragha.

Mkizungumza usijikite tu kwenye nini unataka, bali pia elewa nini mpenzi wako anataka.

Mkijadili kwa pamoja utapata mwanga wapi pa kuanzia, ikiwamo kukubaliana nini kitawafanya mjisikie vizuri mkiwa faraghani na hatimaye kufurahi nyote kupata mlichokikosa kwa muda mrefu.

Inawezekana kuna vitu kila mmoja wenu anavifanya mkiwa faragha havimfurahishi mwingine, lakini mnashindwa kuambiana, hapa ndipo mahali pa kuvisema, pia mnaweza kushirikisha wataalamu wa mahusiano.

Mjiruhusu kuonyeshana ujuzi wa tendo la ndoa, kama unaona inaweza kuleta shida, mshirikishe kuwa unataka kumuonyesha manjonjo mapya. Hii itamfanya kuwa na hamu na hayo majonjo na mwili, akili na roho vitakuwa tayari kushiriki vikijua kuna mazuri yanakuja. Hii isiwe ya kupita, bali ya kudumu, kila mara ukijifunza kitu kipya unampa mshawasha wa kukijua na yeye pia halikadhalika.

Si vibaya siku moja moja mkibadilisha mazingira ya kufanyia tendo, simaanishi yawe ya gharama kubwa, ila nasisitiza jitahidini kubadili eneo mnalofanyia mambo yenu kwa kadiri mtakavyojaaliwa.

Muombe maoni siku utakayohisi amefurahia zaidi ujue ulifanya nini hadi kufikia hali hiyo, nawe pia siku ukifurahi zaidi mweleze ashikilie hapo hapo, kwani amekukuna mtima.

Usijipunje, hili suala halitakiwi kusinyaa, linatakiwa kuchanua siku zote, jifunze, tafuta mbinu. Watu wanapojadili masuala hayo hakikisha unakuwa msikilizaji ili ujifunze vitu vipya. Usisahau kumpa nyama ya ulimi, ukimkemea hata ukiwa na mbinu mpya milioni moja, hatofurahia tendo na asipofurahi nawe hutopata unachokitaka kutoka kwake.


Swali: Sijui ana shida gani huyu shemeji yako Anti, kwani naishi naye huu mwaka wa nane, lakini hanishirikishi suala lolote kuhusu mambo ya familia yetu. Huwezi kuamini hata nyumba tunayoishi alijenga hadi akamaliza akaniambia nijiandae tunahamia kwenye nyumba yetu.

Nilifurahia kwa sababu tumepiga hatua, ila ilinifikirisha sana, yaani mtu ananunua kiwanja, anakusanya fedha mpaja anajenga na kumaliza nyumba sijui chochote. Hata watoto anaweza kuwahamisha shule bila kunishirikisha mpaka wanaporudi likizo ndiyo ninajua.

Hiyo ni mifano michache, yapo mambo mengi anafanya siyajui, nayajua kwa bahati mbaya kama hayawezi kutimia bila mimi kujua, mfano hilo la kuhama nyumba.

Jibu: Siku anapokuwa na furaha zungumza naye kuhusu jambo hili. Umewezaje kulivumilia kwa miaka minane, huoni kama umelifuga na linaweza kuwa limeota mizizi?

Unapozungumza naye kuhusu hilo, hakikisha mazungumzo yako yanajikita kwenye hisia zako na si kwenye lawama.

Toa sababu kwa nini ni muhimu kwako kushirikishwa kwenye mambo ya familia. Hii inaweza kusaidia mwenza wako kuelewa hisia zako na athari za kutoshirikishwa kwenye mambo yanayohusu familia yenu. Hakikisha una mambo muhimu ya kumwambia. Nasisitiza usilalamike, eleza kwa kujiamini bila jazba wala papara. Inawezekana kwamba mwenza wako hajui unavyohisi au hata hajui jinsi ya kushirikisha. Kwa hiyo unaweza kumchomekea iwapo kuna jambo lolote la kifamilia analifanya kwa wakati huo unapaswa kulijua ili mlijadili kwa pamoja.

Akikueleza analolifanya usifanye makosa, hakikisha unaonyesha msaada wako. Wakati mwingine, mwenza anaweza kuacha kukushirikisha kwa namna ulivyojiweka anaona huwezi kumsaidia chochote, hapo muonyeshe uwezo wako.

Ukiijua sababu kwa nini alikuwa hakushirikishi pia itakusaidia kukabiliana nayo. Pengine alikuwa anaona aibu kukuambia mambo yake au mila na desturi za alikolelewa ni mwiko mwanamke kushirikishwa mambo ya familia, hapo utamsaidia kubadilika pia.

Mabadiliko hayaji mara moja. Endelea kuwa mvumilivu na uwe tayari kwa mabadiliko madogomadogo. Inawezekana mwenza wako atahitaji muda kujifunza jinsi ya kukushirikisha zaidi.

Usisahau kumshirikisha na yeye pia, ikiwamo mambo yako binafsi ya kazini au kwenye biashara, hii inaweza kumtia moyo yeye pia afanye vivyo hivyo kwako.

Kama hali haibadiliki hata baada ya kutumia mbinu hizi na kujipa muda wa uvumilivu, mshirikishe mtaalamu wa mahusiano awaite pamoja na kumuelimisha zaidi kwa nini anapaswa kukushirikisha kwenye mambo ya familia yenu.