Shule zimefungwa, kazi kwenu wazazi, walezi

Muktasari:
- Tunaambiwa kuwa mbali ya kupumzika, likizo pia ni fursa muhimu kwa wazazi na walezi kuwasaidia watoto wao, hasa wale wanaosoma shule za bweni kujifunza stadi mbalimbali za maisha.
Baada ya muhula wa kwanza wa masomo kufungwa Juni hii, ni dhahiri kuwa watoto wako nyumbani kwa mapumziko ya likizo.
Huu ni wakati mwafaka kwa wazazi kuwa karibu nao, kuzungumza nao kuhusu waliyojifunza shuleni na pia kupanga kwa pamoja namna ya kujiandaa kwa muhula wa pili wa mwaka wa masomo 2025.
Tunaambiwa kuwa mbali ya kupumzika, likizo pia ni fursa muhimu kwa wazazi na walezi kuwasaidia watoto wao, hasa wale wanaosoma shule za bweni kujifunza stadi mbalimbali za maisha.
Miongoni mwazo ni pamoja na maarifa ya jamii ambayo watoto wa enzi hizo walikuwa wakiita maarifa ya nyumbani, yatakayowasaidia kuendesha maisha yao ya kila siku kwa hekima, busara na heshima hasa akiwa anajitambua.
Katika maisha ya kila siku, mara nyingi watu wazima huwa wanafuata utaratibu wa namna ya kuishi kijamaa kwa kujuliana hali, kushirikiana katika shughuli mbalimbali.
Hivyo hata watoto pia wanapaswa kufundishwa mambo haya mapema, na ikibidi, mzazi mfundishe vema mwanao namna ya kuomba radhi kukumbuka kuomba radhi mara moja kama amekosea.
Kuna baadhi ya makabila hutumia wasaa wa likizo wakikutana kuombana radhi kama walikoseana siku za nyuma.
Changamoto za kukoseana zipo hata kwa watoto, ama kwa kujua ama kutokujua, lakini tofauti ni kuwa wao bado hawajafikia uwezo wa kuzimudu. Hapa sasa ndipo mzazi anapaswa kuchukua nafasi ya kuwa mlezi na mwalimu wa maisha ya mtoto wake.
Wataalamu wa masuala ya malezi, husisitiza umuhimu wa wazazi na walezi kuwafundisha watoto kufuata maelekezo tangu wakiwa wadogo.
Wanasema ni vema kuanza kuwaelekeza kufanya kazi ndogo kama kuweka vitu vyao vya kuchezea mahali pake, kupanga viatu, begi la shule na vitu vingine vya nyumbani. Wakumbushe mara kwa mara kwamba wanapopewa maelekezo, ni vyema kumtazama anayezungumza nao usoni na kumsikiliza kwa makini. Mbali na kuwa dalili ya heshima, hulinda mawasiliano bora, haya yote wazazi mnapaswa kuyarudia na kuyasisitiza hasa kipindi hiki ambacho wako nyumbani kwa mapumziko.
Mzazi kumbuka kuwa kukosea ni sehemu ya maisha ya binadamu. Hivyo mtoto wako pia anatakiwa afundishwe namna ya kuomba msamaha kwa dhati bila visingizio.
Hii itamsaidia katika kujenga uhusiano mzuri na wanafunzi wenzake awapo shuleni nan je ya shule.
Upo mtazamo miongoni mwa wazazi kuwa shule za bweni hutoa mazingira bora ya kujifunza na kumfanya mtoto kuwa na nidhamu ya kitaaluma.
Wengine huamua kuwapeleka watoto bweni kwa sababu tu hana msaidizi wa kazi nyumbani au ratiba zake kuwa ngumu.
Lakini, je, ufaulu pekee unatosha kuwa kipimo cha makuzi bora? Je, mafanikio ya kitaaluma yasiyozingatia tabia njema yanasaidia nini iwapo yamekosa msingi wa utu na stadi za maisha?
Ukweli ni kwamba watoto wanaolelewa na kusoma wakiwa nyumbani mara nyingi hujifunza zaidi kuhusu maisha ya kawaida kama ushirikiano, kuwajibika, kujisaidia na kuwa sehemu ya familia.
Kwa mfano, kuna mwanafunzi mmoja aliyeniambia kuwa licha ya kumaliza shule za bweni, hajui hata kupika. Nilipomuhoji ataishije bila msaada, alijibu kuwa ataajiri mfanyakazi wa ndani.
Lakini hili si suluhisho la msingi. Kuna hatari kubwa ya watoto wanaolelewa katika mazingira haya kukosa makuzi ya msingi ya kujitegemea na kuishi vizuri na watu wengine.
Hivyo wakati huu wa likizo, familia zinapaswa kuwa mahali pa kujifunzia na kujengea misingi ya maisha.
Na hili litafanikiwa tuiwapoa mzazi au mlezi utaweka utaratibu mzuri wa maisha nyumbani watoto wanapokuwa likizo.
Lakini suala la ukaribu wa wazazi na watoto pia linasaidia kuwafundishana kwa vitendo mambp mbalimbali ya uwajibikaji kama mtoto wa kike au wa kiume.
Labda niwakumbushe tu wazazi wenzangu, hatupaswi kuwalea watoto wetu kwa kufuata mkumbo au kwa mazoea au kwa mitazamo iliyopitwa na wakati.
Tukumbuke dunia imebadilika, lakini misingi ya malezi mema haibadiliki. Tukitumia muda huu wa likizo kuwalea watoto wetu kwa busara, tutawajengea msingi bora wa maisha yao ya baadaye. Kwa sababu malezi si jukumu la shule pekee. Ni jukumu letu kama wazazi na walezi, mnapaswa kuwajibika katika hili.