Kinababa mpo? Malezi si ya kinamama pekee

Muktasari:
- Kwa mujibu wa tafiti na wataalamu mbalimbali wa malezi, ushiriki wa baba katika malezi ya mtoto si hiari tena, bali ni jambo la lazima kwa ukuaji bora wa mtoto.
Dar es Salaam. Ikiwa leo Juni 15, 2025 ni maadhimisho Siku ya Baba duniani, ushiriki wake katika malezi unatajwa kuchochea ustawi bora wa watoto na jamii kwa ujumla.
Hata hivyo, katika jamii nyingi za Kiafrika, jukumu la kulea watoto limekuwa likihusishwa zaidi na mama, huku baba akionekana kama mtoaji wa mahitaji ya familia pekee.
Kwa mujibu wa tafiti na wataalamu mbalimbali wa malezi, ushiriki wa baba katika malezi ya mtoto si hiari tena, bali ni jambo la lazima kwa ukuaji bora wa mtoto.
Katika utafiti uliochapishwa katika tovuti inayozungumzia masuala ya malezi ya watoto ya ‘Zero to Three’ umeeleza kuwa watoto ambao hupata muda wa kula, kucheza na kuzungumza na baba zao huwajengea kujiamini, furaha na tabia ya kupenda kujumuika na watu wengine katika jamii inayowazunguka.

Mdau wa masuala ya afya ya akili na malezi, Vannesser Mkagilage ameeleza kuwa ukuaji bora wa mtoto kimwili, kiakili na kuwa na tabia njema zinazokubalika na jamii, unahitaji ushiriki wa baba na mama katika malezi na hutakiwa kuanza mara tu mtoto anapozaliwa.
Mkagilage amesema mtoto anapozaliwa anakuwa hana uelewa juu ya jambo lolote linaloendelea duniani lakini mwalimu wake wa kwanza ambaye anakutana nae na kujifunza ni familia anayoishi.
Amesema katika maisha ya kila siku, watoto huwatazama wazazi wao kama kioo cha kujifunza.
Ameeleza kuwa baba anaposhiriki katika shughuli mbalimbali za malezi ya mtoto, kunamfanya kujenga ukaribu na mtoto pamoja na familia kwa ujumla.
Pia humjenga mtoto kukua huku akiamini kuwa suala la malezi ya mtoto si la mama pekee bali ni la wote hivyo kumjenga katika misingi ya usawa na maadili mema.
“Ushiriki wa baba katika malezi huanza mara tu mtoto anapozaliwa, Uwepo wa baba katika maisha ya mtoto unaongeza usalama wa kihisia kwa mtoto na hujenga uhusiano wa karibu baina yao “ameeleza.
Akizungumza na gazeti hili Athumani Shomari ambaye ni baba wa watoto watatu, amesema japokuwa ni muhimu baba kuwepo katika malezi ya mtoto, mila na desturi, ugomvi kati ya wazazi, ratiba za kazi zisizotabirika, au hata kutoelimika kuhusu umuhimu wa nafasi yao kwenye malezi, vinachangia kukosekana kwa ushiriki wao.
Nini kifanyike?
Ameshauri elimu zaidi kuendelea kutolewa kuhusu umuhimu wa baba kushiriki kikamilifu katika malezi ya watoto hasa katika kizazi cha sasa.
“Mtoto anahitaji zaidi ya mahitaji ya msingi, anahitaji uwepo wa wazazi wote wawili katika ukuaji wake”
“Ni wakati sasa kwa baba wa Kitanzania kuacha dhana ya "mlezi ni mama" na kila mmoja kuchukua nafasi yake ipasavyo katika kulea taifa la kesho”amesema.