Mwenza wako ana gubu, mpenda lawama?

Muktasari:
- Gubu ni hali au tabia ya mtu kuonyesha hasira, kinyongo, au kukasirika kimya kimya bila kueleza sababu ya wazi.
Maisha ya uhusiano yanahitaji uvumilivu, uelewa na mawasiliano ya wazi ili yadumu.
Hata hivyo, kuna changamoto zinazojitokeza, mojawapo ikiwa ni kuwa na mwenza au mpenzi anayelalamika sana na mwenye gubu.
Kila unalomfanyia haoni dhamira ndani yake. Ni mtu wa madai na lawama zisizo na ukomo.
Katika hali kama hii, furaha ya uhusiano unaweza kuwa sawa na ndoto ya mchana, na kibaya zaidi ni pale inapoweza kusababisha hata tatizo la afya ya akili.
Hili linaweza kuathiri sana furaha ya uhusiano na hata afya ya kiakili ya wahusika.
Gubu ni nini?
Gubu ni hali au tabia ya mtu kuonyesha hasira, kinyongo, au kukasirika kimya kimya bila kueleza sababu ya wazi.
Ni namna ya mtu kuonesha kutoridhika au kukwazika kwa njia ya kimya, kutoa kejeli au maneno yenye kuuma lakini yasiyoeleza tatizo moja kwa moja.
Mtu mwenye gubu mara nyingi huwa na tabia ya kujitenga, kununa, kujibu kwa hasira, au kutoa kauli zinazoumiza kihisia bila kueleza kilichomsumbua.
Gubu linaweza kuonekana kwa njia kama kunyamaza na kutojibu maswali kwa makusudi, kutomjali mwenza au kuonyesha ukatili wa kimya, kutoa kauli zenye dhihaka au matusi ya chini chini na kujibu kwa kejeli.
Kwa mfano mwenza anapokwambia: “Wewe ni malaika siyo? Hutendi makosa kabisa.”
Gubu ni tofauti na hasira ya wazi, kwani mtu mwenye gubu huwa hajafunguka kueleza hasira yake moja kwa moja.
Hii mara nyingi huleta ugumu kwa mwenza kuelewa tatizo na kutafuta suluhisho.
Tabia hii inaweza kuharibu mawasiliano, kuleta migogoro ya mara kwa mara, na kusababisha maumivu ya kihisia kwa mpenzi au mwenza wake.
Sababu za mtu kuwa na gubu ni nyingi. Inaweza kuwa matokeo ya majeraha ya kihisia ya zamani, msongo wa mawazo, hofu ya kuumizwa tena, au tabia waliyojifunza katika malezi yao. Mara nyingine, gubu hutumika kama njia ya kujilinda au kudhibiti uhusiano.
Lawama kwenye uhusiano
Katika muktadha wa makala haya, lawama ni hali ya kumtupia mwenza au mpenzi mzigo wa makosa, matatizo au hali mbaya inayojitokeza katika ndoa au uhusiano.
Katika uhusiano wa kimapenzi, lawama zinaweza kuharibu mawasiliano, kupunguza upendo, na kusababisha migogoro ya mara kwa mara.
Lawama hufanya mtu ahisi kutoshughulikiwa kwa haki, kulaumiwa bila kusikilizwa, au kukosolewa bila kusaidiwa.
Mara nyingi, lawama hutokea pale ambapo wenza hawajifunzi kuwasiliana kwa njia chanya. Badala ya kueleza hisia zao kwa utulivu, mmoja anakuwa mwepesi wa kusema kama vile:
"Wewe ndiyo unaharibu kila kitu,"
"Kama si wewe, haya yote yasingetokea,"
"Najuta kukuoa/ kuolewa’’
Kauli kama hizi huumiza, hujenga ukuta wa kihisia na huzuia maelewano. Mwenza anayelaumiwa mara kwa mara anaweza kujenga chuki au kuanza kujitetea kila wakati, hali inayosababisha mawasiliano ya mivutano badala ya maelewano.
Sababu za lawama zinaweza kuwa kama vile kutoridhika katika uhusiano, msongo wa mawazo, kutoaminiana au maumivu ya kihisia yaliyowahi kutokea.
Mara nyingine, lawama hutumika kama njia ya kuficha udhaifu binafsi kwa kumgeuzia mwenza lawama zote.
Kwa ujumla, kuepuka lawama kunahitaji uvumilivu, uelewa, na mawasiliano ya wazi. Ndoa au uhusiano wenye afya hujengwa kwa kuelewana, si kulaumiana.
Sababu ya gubu, lawama
Maswali makuu hapa ni mambo gani yanayosababisha mtu kuwa na gubu na kupenda lawama? Na je unawezaje kuishi na mwenza wa aina hiyo?
Watu wengine huonyesha tabia hizi kutokana msongo wa mawazo au matatizo ya kiakili, kwani mtu anapokuwa na msongo, hasira au huzuni, huweza kuonyesha gubu au kutoa lawama bila sababu ya msingi.
Sababu nyingine ni historia ya maisha. Watu waliokulia katika mazingira ya ukosoaji au matatizo ya kifamilia, hujifunza gubu na lawama kama njia ya kuwasiliana.
Pia hali hiyo unaweza kutokea pale mwenza anaposhindwa kutimiziwa mahitaji yake ya kihisia.
Kama mwenza anahisi kupuuzwa au kutothaminiwa, anaweza kuonyesha hali ya kukosa furaha kwa malalamiko au gubu.
Kwa mfano, mume anapokuja nyumbani na kukuta chakula hakijaandaliwa, badala ya kuuliza kwa utulivu, anaanza kulalamika na kusema, “Kila siku nalazimika kula chakula kibaya, kama huna muda wa kupika nambie mapema.”
Fanya haya
Katika mazingira haya ya uhusiano, wataalamu wanashauri mambo mbalimbali kunusuru maisha ya wenza ikiwamo kuweka mawasiliano ya wazi na yenye heshima
Mawasiliano ni msingi wa kila uhusiano. Unapokuwa na mwenza mwenye tabia ya kulalamika au kuwa na gubu, epuka kurudisha maneno au kuonyesha hasira. Badala yake, zungumza kwa upole lakini kwa uthabiti.
Tumia sentensi za “mimi” badala ya “wewe” ili kuepuka lawama na ili ujifanye kuwa wewe ndiye mkosaji.
Kwa mfano, badala ya kusema, “Wewe kila siku ni mtu wa kulalamika tu,” unaweza kusema: “Ninajisikia vibaya ninapohisi kuwa hauoni mazuri ninayojaribu kufanya.”
Mara nyingi watu wenye tabia ya kulalamika wanahitaji kusikilizwa. Badala ya kumkatisha au kumkwepa, mpe nafasi ya kuzungumza huku ukimsikiliza kwa makini. Wakati mwingine watu wa aina hii wanapomaliza kujieleza, hupunguza gubu na hasira.
Kwa mfano, mpenzi wako anapolalamika kuwa hujali, badala ya kumwambia anasumbua, muulize kwa utulivu, “Nieleze, ni nini kimekufanya uhisi hivyo?”
Njia nyingine ni kutafuta suluhisho. Badala ya kugeuza lawama kuwa ugomvi, ni vyema kuangalia suluhisho. Tambua suala analolalamikia na tafuteni njia za pamoja za kulitatua.
Kwa mfano, mwenza analalamika kila mara kuwa unachelewa kurudi nyumbani. Badala ya kubishana, panga muda utakaomridhisha na pia usiathiri kazi zako.
Afya yako muhimu. Kama malalamiko au gubu vinaanza kuathiri afya yako ya kiakili, ni muhimu kuweka mipaka. Hii inamaanisha pia kuchukua muda wa kupumzika au kutafuta usaidizi kutoka kwa wataalamu wa uhusiano, saikolojia na hata afya ya akili.
Mfano wa kuweka miaka ni kama kumwambia: “Ninathamini kile unachosema, lakini tukizungumza kwa hasira, sitoweza kusaidia. Hebu tuchukulie dakika kumi kutulia kisha tuzungumze tena.”
Kumbuka watu wanaolalamika mara nyingi hujiona hawatambuliwi au hawapendwi.
Kwa hiyo, ongeza juhudi za kuonyesha mapenzi, kushukuru, na kumpongeza mwenza wako hata kwa mambo madogo. Hili linaweza kupunguza malalamiko na hali ya kuwa na gubu.
Mfano, kumwambia, “Nashukuru kwa jinsi unavyohakikisha watoto wanakula vizuri kila siku,” kunaweza kumfanya ajihisi kuthaminiwa na kupunguza hali ya kulalamika.
Hata hivyo, ikiwa hali inazidi kuwa mbaya, dawa si kila mmoja kushika hamsini zake.
Ni muhimu kuwashirikisha wataalamu wa uhusiano na wanasaikolojia. Ushauri wa pamoja unaweza kusaidia kuelewa kiini cha tatizo na kuimarisha mawasiliano.
Kuishi na mwenza anayelalamika sana na mwenye gubu si rahisi, lakini kwa kutumia mbinu sahihi, uhusiano unaweza kuboreshwa.
Uvumilivu, mawasiliano ya wazi, huruma na usaidizi wa kitaalamu vinaweza kusaidia kubadilisha mwenendo huu. Kumbuka kwamba kila mtu ana upungufu, na mara nyingi malalamiko ni kilio cha mtu anayetafuta kueleweka au kupendwa zaidi. Kwa hiyo, badala ya kupambana, chagua kuelewa na kujenga.