Msanii wa filamu aliyeamua kufanya kweli kwenye uchungaji

Pastor Myamba
Muktasari:
Anaongeza kuwa kanisa hilo tayari limeshakamilika na maandalizi yanaendelea kwa ajili ya kuanza kwa ibaada za kiroho kila siku ya jumapili.
Tabia hujenga mazoea, au mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Hii yote ni misemo ya wahenga , na kwa upande mwingine baadhi ya watu hufikia kuamini kuwa kazi anayoifanya mtu fulani huweza kuathiri utamaduni wake katika maisha yake ya kila siku.
Katika upande wa sanaa hususani ya uigizaji, wasanii wamekuwa wakikutana na changamoto kadhaa ya kutafsiriwa nafasi zao za uigizaji na maisha yao halisi ya mitaani.
Kwa hapa nchini, jamii imekuwa ikikosa majibu sahihi juu ya mcheza filamu wa Bongo Movie Emanuel Myamba au maarufu kama Pastor Myamba kutokana na nafasi yake moja tu katika maisha ya uigizaji kama mchungaji kanisani.
Tangu alipoanza kuonekana katika filamu mwaka 2005 kupitia filamu ya Johari , Myamba amekuwa amekuwa akicheza nafasi hiyo mara kwa mara na hadi sasa ni miaka tisa.
Ameshacheza filamu za kibongo (38) ambapo 10 kati ya hizo ni za kwake mwenyewe kupitia Kampuni yake ya ‘Bornagain films.
Hata hivyo, Myamba kwa sasa ameamua kuonyesha hisia zake za kiroho katika uhalisia wa maisha yake, huku akiwa katika maandalizi ya mwisho ya kufungua kanisa lake kwa ajili ya uponyaji.
“Kuigiza kwangu katika filamu Watanzania watambue kuwa ni sehemu ya maisha yangu ya kiroho duniani,sichezi filamu tu kwa sababu ya kipato na kuonyesha maisha ya imani lakini ninafanya hivyo kwa utashi nilionao,” anasema Pastor Myamba na kuongeza:
“Kanisa langu litakuwa nyuma ya jengo la Ubungo Plaza jijini Dar es Salaam , nafanya hivyo kwa sababu nimekuwa nikitamani kuona watu wakibadili tabia zao, hivyo nimeamua kufungua kanisa ili kuonyesha niko makini,”
Anaongeza kuwa kanisa hilo tayari limeshakamilika na maandalizi yanaendelea kwa ajili ya kuanza kwa ibaada za kiroho kila siku ya jumapili.
Kazi yake inapigwa vita
Wakati akijiandaa kufungua kanisa hilo siku chache baadaye, Myamba anabainisha kupigwa vita na kundi la baadhi ya viongozi wa makanisa kupitia kazi mpya aliyoandaa.
“Kuna filamu mpya inayoitwa ‘Toba halisi’, ambayo inazungumzia maisha ya unafiki unaofanywa na baadhi ya viongozi wa makanisa kuhubiri dini wakati wakionyesha vitendo viovu,” anasema na kuongeza:
“Filamu hiyo msingi wake ni mawazo ya viongozi wa makanisa kadhaa ya kiroho, ambayo nisingependa kuyataja majina, waliniita mwanzoni mwa mwaka huu na kunieleza kanisa linavyokwenda kwa sasa ni tofauti na agizo la Mungu.”
Pastor Myamba anasema viongozi hao walimshawishi kuandaa filamu ya kukemea, lakini mpaka sasa kuna baadhi ya viongozi wa makanisa kadhaa ambao walikuwa wanapinga filamu hiyo isiingie sokoni kwa madai ya kuchafua kanisa.
“Baada ya kuona mvutano huo nikasema ujumbe umegusa wengi kwa hivyo sikuahirisha.Filamu hiyo ilikuwa ni maombi ya wengi na imeshaingia sokoni siku chache zilizopita,” anasema Myamba.
Baadhi ya filamu zilizompatia umaarufu ni pamoja ‘Pastor Myamba Trial, God’s Kingdom na nyingine nyingi.
Kuhusu Chuo cha filamu:
Mwaka 2009 aliamua kufungua kampuni hiyo ya filamu kabla ya kuanzisha chuo cha sanaa ya uigizaji.
Myamba ni Mkurugenzi mtendaji wa Chuo kinachotoa taaluma katika sanaa ya uigizaji kwa lengo la kukuza vipaji nchini ambapo kwa sasa chuo hicho kina zaidi ya wanafunzi 2000
Chuo hicho kinafahamika kama ‘Tanzania Film Training Center (TFTC), kinafundisha masomo manne ambayo ni pamoja na kuigiza,kupiga picha,kuandika na kipngele cha maadili katika uigizaji ambacho amekuwa akiwekea mkazo zaid,i ili kuleta mabadiliko katika maadili ya sanaa hii.
“Kwa sasa kimetimiza miaka mitatu tangu nimekianzisha, kina wanafunzi wapatao 2000 na tayari wahitimu zaidi ya 150 ambao wameshaingia kwenye soko la filamu za hapa Bongo,” anasema na kuongeza:
“Nafarijika sana kwa sababu nimekuwa nikiwaona wakitumika kwenye filamu za wasanii wakubwa kama vile Tino, JB, Ray,Odama na hata mimi mwenyewe huwatumia katika kampuni yangu.”