Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Malengo ya Ibada ya Hija katika Uislamu

Muktasari:

  • Katika ibada ya Hijja, watu hukusanyika kutoka pande zote za dunia wakitofautiana kwa mazingira yao, lugha, jinsia na rangi, wakielekea mahali pamoja.

Dar es Salaam. Hijja ni nguzo ya tano katika Uislamu, ibada hii inabeba maana na malengo makubwa yanayowafanya Waislamu kuwa na shauku kubwa ya kuitekeleza. Miongoni mwa malengo hayo ni yafuatayo:

Mojawapo ya malengo ya kwanza yanayodhihirika wazi, ni vazi la Ihramu, ambalo huvaa hujaji, kupitia vazi hilo humkumbusha makazi ya mwanzo ya kuelekea Akhera, na kuachana na anasa za kidunia.

Vazi la Ihramu ni ukumbusho kuhusu maisha ya kaburini,. Kama ambavyo maiti huondoka duniani bila mavazi ya anasa na starehe, ndivyo ilivyo kwa Hujaji anapovua nguo za kifahari na kuvaa vazi la Hijja ihramu.

Hili ni fundisho kwamba safari ya Hijja ni mfano wa safari ya mwisho ya mwanadamu kuelekea kwa Mola wake.

Katika ibada ya Hijja, watu hukusanyika kutoka pande zote za dunia wakitofautiana kwa mazingira yao, lugha, jinsia na rangi, wakielekea mahali pamoja, yaani uwanja wa Arafa.

Katika siku hiyo, hawamiliki chochote cha dunia isipokuwa mavazi ya kuweza kufunika miili yao.

Hufika wakiwa wamechafuka kwa vumbi na nywele timtim, wakiwa wameacha mali, watoto, vyeo na mamlaka yao kwa hiari, kwa lengo la kutekeleza ibada hii tukufu na kutafuta msamaha wa Allah Mtukufu.

Tofauti iliyopo kati ya mkusanyiko huu na Siku ya Kiyama ni kwamba. Hija ni mkusanyiko wa hiari wenye matumaini ya kupata msamaha wa Mola Mlezi. Kiyama ni mkusanyiko wa lazima, wa hesabu na malipo.

Hili pia, ni miongoni mwa malengo makuu ya Hijja, linalodhihirika wazi katika kujenga subira na juhudi kubwa anazozifanya Hujaji tangu aondoke nyumbani kwake hadi kufika katika mji mtakatifu wa Makka, kisha kuingia kwenye Nyumba ya Allah Tukufu (Al-Kaaba).

Katika mzunguko huo, Hujaji hukumbana na msongamano mkubwa wakati wa kutufu, kusai kati ya Safa na Marwa, kurusha mawe kwenye jamarat, na ibada za siku ya kuchinja (ya’um An-Nahr) ambazo ni pamoja na kurusha mawe, kunyoa au kupunguza nywele, kuchinja mnyama, kutufu nyumba ya Allah Tukufu Haya yote yanamhitaji Hujaji kuwa na nguvu na subira ya kweli.

Ni mfano wa wazi wa kujipamba na roho ya jihad, ambayo inapaswa kubaki hai katika Umma wa Kiislamu, kwani jihad ni kilele cha Uislamu, na chanzo cha utukufu na nguvu ya Waislamu.

Katika utekelezaji wa ibada ya Hijja, watu huja kutoka maeneo mbalimbali wakiwa na tabia tofauti. Wapo wapole na wapo wakali na wagumu wa tabia.

Kadhalika wapo wanyonge, wazee dhaifu, vijana wenye nguvu, watoto wadogo, na hata watoto wachanga. Hivyo, Hujaji anapaswa kujifunza subira na kuwapa wengine nafasi, hasa wakati wa kutufu, kurusha mawe, au kubusu Jiwe Jeusi (Hajar Al-As’wad). Asimsukume mzee wala kumsumbua mtoto mdogo.

Daima akumbuke kauli ya Allah Mtukufu:". Hija ni miezi maalumu. Na anaye kusudia kufanya Hija katika miezi hiyo, basi asiseme maneno machafu wala asifanye vitendo vichafu wala asibishane katika Hija..."
 (2: 197)

Waislamu kutoka mataifa mbalimbali hukusanyika mahali pamoja kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Hijja, bila kubaguliwa kwa sababu ya utajiri, lugha au kabila.

Wanamwabudu Allah Mungu mmoja, wanafuata Mtume mmoja, wanaelekea kwenye Qibla kimoja, na lengo lao ni moja. Huu ni udugu wa Kiislamu, ambao huwafanya wawe kitu kimoja.

Mahujaji huja kutoka kila pembe ya dunia, wakielekea lengo moja—kutafuta msamaha wa Allah Mtukufu na kujikurubisha Naye kwa kutekeleza wajibu wa Hijja. Wote wapo chini ya bendera moja ambayo ni Uislamu, na wanapaza kauli moja ya kumpwekesha Allah Mtukufu: "Labbayka Allahumma Labbayk, Labbayka laa sharika laka Labbayk. Inna al-hamda wan-ni‘mata laka wal-mulk, laa sharika lak."

Mahujaji wanakusanyika kutoka mataifa na makabila tofauti. Wote wanakutana katika eneo moja, kwa muda mrefu, chini ya udugu wa Kiislamu. Katika mazingira haya, wanajitambulisha na kufahamiana, hata kama wanatoka nchi moja.

Kwa kupitia utangamano huu: Udugu na mapenzi huimarika, uhusiano huendelea hata baada ya kurejea makwao. Hii ni sehemu ya malengo ya Uislamu, kama alivyosema Allah Mtukufu:

"Enyi watu! Hakika Sisi tumewaumba kutokana na mwanamume na mwanamke, na tumewafanya kuwa mataifa na makabila ili mfahamiane." (49: 13)

Hijja hutufundisha kuwa ibada ni maamrisho ya Allah ambayo hayaruhusiwi kubadilishwa, kupunguzwa au kuongezwa kwa akili ya mwanadamu.

Allah ndiye aliyepanga ibada ya Hijja kwa hekima Anayoijua Yeye peke Yake. Muislamu hapaswi kujishughulisha kutafuta sababu za kubusu Jiwe Jeusi, kukaa Mina bila kufanya shughuli nyingine zaidi ya swala, kutufu upande wa kushoto wa Kaaba, na kadhalika.

Anachopaswa kufanya ni kukubali na kutii, huku akiamini kuwa utii huu ni sehemu ya ukamilifu wa imani yake.