Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mbinu kumuandaa mtoto wa kiume kuwa baba mwema

Muktasari:

  • Mzazi anapaswa kutambua kwamba kumlea mtoto wa kiume,  ni zaidi ya kumfundisha elimu au kumkadiria anachokipata kimaisha.

Dar es Salaam. Malezi bora ni msingi wa familia bora. Mara nyingi tumekuwa tukizungumza kuhusu nafasi ya mzazi kumlea mtoto wa kike, lakini nafasi ya kumsaidia mtoto wa kiume aje kuwa baba bora, imekuwa ikipuuzwa au kutozungumziwa kwa mapana.

Hata hivyo, mzazi anapaswa kutambua kwamba kumlea mwanaume ni zaidi ya kumfundisha elimu au kumkadiria anachokipata kimaisha.

Ni kumwandaa kuwa mtu mzima kamili, mume bora na hatimaye baba bora kwa watoto wake  baadaye.

Mara zote watoto hujifunza kwa kuona zaidi kuliko kusikiliza tu.

Hivyo baba au mama anapokuwa mfano bora wa upendo, heshima, uvumilivu na usawa, mtoto wa kiume atakua akijua kwamba hayo ndiyo msingi wa familia bora.

Hii inamaanisha kwamba mzazi anapaswa kuwa makini katika matendo yake, lugha anayotumia, na jinsi anavyoshughulika na changamoto mbalimbali.

Mtoto wa kiume anayeona baba yake anamsaidia mama kazi za nyumbani, anaheshimu nafasi ya mama na kudumisha mawasiliano bora, atakua akiamini kwamba hivyo ndivyo mwanaume bora anavyopaswa kuwa.

Kumfundisha umuhimu wa uwajibikaji, hiyo ni moja ya sifa kubwa ya baba bora. Hivyo mzazi anapaswa kumsaidia mtoto wa kiume kutambua kwamba kila tendo lina matokeo na kwamba, ni jukumu lake kubeba matokeo hayo.

Hii inaweza kuanzia kwa kumfundisha kumaliza kazi ndogo anazopewa nyumbani, kuheshimu wakati na kushughulikia changamoto bila kukata tamaa.

Mtoto anapokuzwa katika mazingira yanayosisitiza uwajibikaji, atakuwa mwanaume anayeweza kutimiza majukumu yake kama mume na baba bila visingizio.

Lakini pia suala la kujenga maadili kwenye familia ni jambo sahihi zaidi. Kwa sababu maadili mema humsaidia mwanaume kuwa mwaminifu, mwenye huruma na anayeaminika.

Hivyo, mzazi anapaswa kumsaidia mtoto wa kiume kutambua umuhimu wa ukweli, uadilifu, na heshima kwa wengine.

Hii inaweza kufanikishwa kwa kumshirikisha kwenye mazungumzo muhimu, kumwelimisha kuhusu matokeo ya matendo yasiyofaa na kumtia moyo atumie busara wakati wa kufanya uamuzi.

Malezi yenye msingi wa maadili humsaidia mtoto kuwa mtu mzima anayeishi kwa uaminifu, anayeweza kuongoza familia yake kwa busara.
Mara nyingi, wavulana wanakuzwa kwa mtazamo kwamba mwanaume hatakiwi kuonesha hisia zake.

Hili ni kosa kubwa linaloweza kumfanya mtoto wa kiume ashindwe kudhibiti hisia au kukabiliana na changamoto za kiakili wakati wa utu uzima.

Badala yake, mzazi anapaswa kumsaidia mtoto kutambua hisia zake, kuzieleza kwa usahihi na kuzishughulikia kwa amani.

Hii inamsaidia mwanaume atakayekuwa baba ajaye kuelewa hisia zake mwenyewe na zile za familia yake, hivyo kudumisha ukaribu na mshikamano wa kifamilia.
kwa sababu baba bora ni yule anayeweza kumudu majukumu ya kifamilia, ikiwa ni pamoja na kukidhi mahitaji ya kiuchumi.

Mzazi anapaswa kumsaidia mtoto wa kiume kuthamini elimu, ujuzi na nidhamu kazini. Anapokuzwa katika hali hii, atakuwa mwanaume anayeweza kutafuta fursa na kuzitumia ipasavyo, jambo ambalo ni muhimu kwa uhai wa familia anayoikusudia kuijenga.

Lakini pia baba bora ni yule anayeweza kuwasiliana na familia yake kwa busara na uwazi. Katika hili pia mzazi anapaswa kumzoesha mtoto wake wa kiume kushiriki katika mazungumzo ya familia, kutoa maoni yake na kuheshimu mawazo ya wengine. Anapokua katika mazingira hayo, atajua thamani ya ushirikiano na namna ya kutumia busara katika mawasiliano jambo litakalomsaidia kuwa baba anayesikiliza, anayeaminika na anayeongoza kwa mifano bora.

Na bila shaka, mwanaume bora anayeandaliwa kwa nafasi ya ubaba ni yule anayeishi kwa kumjua Mungu na kumheshimu.

Katika hilo, mzazi pia anapaswa kumfundisha mtoto wake huyo wa kiume kumtegemea Mungu, kuheshimu utu wa kila mtu na kuthamini upendo wa kweli.

Haya yote humjengea msingi imara wa utu wema, ukarimu, uvumilivu na busara zinazotakiwa kwa kila baba.
kwa hiyo kila mzazi anapaswa kuzingatia kuwa kumlea mtoto wa kiume ni zaidi ya kumfanya akue kimwili au kumwezesha kupata elimu bora. Ni kumjenga kuwa mwanaume kamili, anayeweza kudhibiti hisia zake, kutenda kwa uwajibikaji, kumheshimu mkewe, kuwalea watoto wake kwa busara na kumtegemea Mungu.

Ni mchakato unaohitaji muda, uvumilivu na upendo usio na kikomo. Lakini matunda yake ni makuu kwa fanilia ambayo ni pamoja na kwamba itakuwa imepata mwanaume anayeweza kuwa baba bora, mume bora na raia mwema katika jamii.