Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mapenzi ni hatua tano, wewe uko ya ngapi?

Muktasari:

  • Tafiti za kisaikolojia kwenye eneo la uhusiano pamoja na yale mengi tunayokutana nayo tunapowashauri wapenzi na wanandoa wengi, yametufanya kufikia hitimisho kwamba mapenzi huwa yana hatua zake tano.

“Inawezekana hakuwa wa kwangu. Yumkini Mungu hakupanga tuwe pamoja. Labda Mungu ameniepushia mengi”.

Mara kwa mara wengi tumesikia sentensi zinazofanana na hizi hususani kwenye vinywa vya watu, marafiki au ndugu zetu ambao wamewahi kuachana, kutengana au kuvunja uhusiano.

Tafiti za kisaikolojia kwenye eneo la uhusiano pamoja na yale mengi tunayokutana nayo tunapowashauri wapenzi na wanandoa wengi,  yametufanya kufikia hitimisho kwamba mapenzi huwa yana hatua zake tano, na kwa bahati mbaya wapenzi wengi wanashindwa kuziendea hatua hizo moja baada ya nyingine.

Katika hatua tano kama tutakavyoona wengi huishia hatua ya tatu.


Hatua ya kwanza: Kuingia katika penzi

Hii ni hatua ya mwanzoni kabisa wakati umekutana na mtu ambaye unaona kama ni ndoto yako imekuwa dhahiri. Mtu uliyemtamani kwa muda mrefu sana.

 Hapa unajihisi mwenye furaha kuliko mtu yeyote yule. Hisia zako zote zinatawaliwa na mihemko ya kuwa na huyo unayemfia. Kila wakati na kila sehemu unatamani kuwa na huyo. Unamwona na kumhisi yeye kuwa vyote katika vyote kwenye maisha yako.

Hii ndio hatua ambayo binti huambiwa kwamba huyo kijana anayekuchumbia ni mwizi au ana wanawake wengi na akajibu “kwani hata mimi si mwanamke?” na wengine ukiwaambia mabaya ya kweli ya wapenzi wao wanakwambia Mungu atambadilisha.

 Katika hatua hii hauko tayari kurudishwa nyuma na mtu yeyote hata akiwa mzazi wako.


Hatua ya pili: Kuwa wawili

Katika hatua hii, mapenzi yamepevuka sana na ile mikutano ya hotelini, kwenye migahawa au kutembeleana mara kwa mara, inabadilishwa kwa kuamua kuanza kuishi pamoja.

Sasa hapa kama ni watu wa dini ndio watafunga ndoa za makanisani au misikitini, wengine bomani, wengine za mila na nyinginezo ili mradi waanze kuishi pamoja kama mke na mume. Kufahamiana kunazidi na unaanza kumjua mwenzako kwa kina zaidi hususani baadhi ya vitu ambavyo mwanzoni ulishindwa kuvijua kuhusu yeye.

 Uwepo wako unaanza kuwa na umuhimu mkubwa kwenye maisha ya mwenzako. Ndani yenu mnaanza kuhisi umoja na furaha ya kipekee. Kila kitu kikienda sawa, baada ya miezi au miaka michache kipindi hiki kinaweza kuwaleteeni mtoto ambaye anaweza kuiongeza furaha baina yenu.

Hapa mwanamke anajihisi salama zaidi ya wakati akiwa hana mtoto na mwanaume anajiona ana jukumu la kuwalinda mama na mtoto.


Hatua ya tatu: Machungu ya kuhisi ulikosea

Katika hali ya kushangaza kabisa, katika kipindi hiki upepo unaanza kubadilika na kama ni safari ya baharini basi mnaanza kuona mawimbi yakivuma kwenye chombo chenu.

Ndani yako unaanza kuona yale matumaini uliyokuwa nayo kwenye hatua ya kwanza na ya pili yanaanza kuzama. Kuna vitu zamani ulikuwa ukiviona vidogo tu kwenye tabia za mwenzako, ulikuwa ukiviona kama njiti, sikuhizi unaanza kuviona vikubwa kama misumari na vinakuchoma kama moto.

Vipindi vya hasira, kelele na kufokeana vinaanza kuingia kwenye uhusiano wenu. Katika kipindi hiki wengi wanatoa sentensi za “tuachane kama tumeshindwana”, “kama umenishindwa nirudishe kwetu”, “nikirudi nisikukute” Kiukweli katika hali na upepo huu ndani yako unahisi kabisa kwamba ulikosea kumchagua yeye, na wengine wanajutia kabisa uamuzi wao.

Zile hisia za kumpenda, kumlinda, kumfurahisha na kumtetea mpenzi wako zinaenda na maji mbali kabisa, tena hutaki kabisa kumsikia, unatamani hata asirudi nyumbani kwa jinsi anavyokuudhi.

Kama mwanzoni mlikuwa mnafurahia tendo la ndoa basi sasa ndio tendo hilo linaingia shubiri. Hutaki akuguse wala akusogelee.

Katika kipindi hiki kiu ya kuwa pamoja imekufa na kuzikwa kabisa, wengine wanatafuta maeneo ya kupumulia ilimradi asiwe nyumbani, wa kushinda baa ndio anapotelea huko kabisa, wa kushinda kazini ndio atakaa huko hadi usiku wa manane. 


Hatua ya nne: Kutengeneza penzi la kweli linalodumu

Kwa bahati mbaya ndoa za wengi huishia hatua ya tatu. Kama uliweza kuvumilia na kufumba macho ukikabiliana na kila upepo kwenye hatua ya tatu.

 Ukavumilia matusi, kupigwa na kudharauliwa. Ukastahimili aibu ya kukalishwa vikao mbele ya ndugu, wasimamizi wa ndoa, marafiki na hata viongozi wa dini.

Kama ulipenya kote huko basi unaingia kwenye hatua ya nne. Hatua ya kulitengeneza penzi la kweli na linalodumu.

 Katika hatua hii moyo wako unaondokana na zile hisia hasi za kujiona ulikosea kuwa na huyo mwenza wako. Huyo mpenzi unayemwona mbele yako unajutia kumtendea kila hiana miezi au miaka michache iliyopita maana sasa ukimtazama unamwona kama malaika kwako.

Sasa unaanza kumwelewa sana na kuukubali upungufu wake. Huu unakuwa wakati wa kuponya majeraha na kuingia kwenye hatua ya mwisho.


Hatua ya tano: Nguvu ya wawili inatumika kubadili ulimwengu

Sasa umeshaweza kumfahamu vema mwenzako na hakuna kinachokuyumbisha kwa urahisi  maana tayari misuli yako ya uvumilivu, ustahimilivu umetanuka.

Sasa unaweza kabisa kustahimili kutofautiana, na hata kuwepo na hisia hasi bado unaweza kupenyeza upendo kwa mwenzako na akauona dhahiri upendo huo.

Hapa mnajisikia huru zaidi, kuhitajiana zaidi na kuhusiana zaidi. Mnaihisi nguvu ya kuleta mabadiliko makubwa sio tu baina yenu bali na kwa wengine wengi wanaowazunguka.

Kuhusiana kwenu sasa hakuwi tu kwasababu ya kuzifurahisha hisia zenu bali kwasababu ya kusudi kubwa ambalo mnahisi Mungu ameliweka ndani yenu. Maranyingi wengi kwenye muda huu wanafanya kazi nyingi pamoja, wanalima pamoja, wanaandika pamoja, wanafundisha pamoja, wanahubiri pamoja au kufanya mengi mengine kwa pamoja.

 Ile nadharia ya mwili mmoja ndio inakuja kuwa dhahiri wakati huu na baada ya kupita kwenye hatua zote nne za nyuma, sasa una ujasiri usiofichika ndani ya moyo na kinywa kutamka kwamba “Huyu ndiye Mungu aliyenipa”.