Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Inawezekana kuwa wenza bila mapenzi ya mwili

Muktasari:

  • Wengi wanagundua kuwa urafiki wa kweli, wa kuaminiana na kuhimiliana, unaweza kuwa wa kudumu na wa kuridhisha zaidi kuliko mapenzi ya kawaida.

Katika jamii nyingi, upendo umezoeleka kuhusishwa moja kwa moja na uhusiano wa kimapenzi.

Filamu, nyimbo, vitabu na mitandao ya kijamii huonyesha mapenzi ya wapenzi kama kilele cha mafanikio ya kihisia.

Lakini miongoni mwa vijana wa kizazi cha sasa, upo mtazamo mpya unaochipuka — upendo wa ‘kiplatoniki’, yaani, ule wa kirafiki wa kina usiohusisha uhusiano wa kimapenzi au kingono, unazidi kupewa thamani.

Wengi wanagundua kuwa urafiki wa kweli, wa kuaminiana na kuhimiliana, unaweza kuwa wa kudumu na wa kuridhisha zaidi kuliko mapenzi ya kawaida.

Upendo wa kiplatoniki ni aina ya uhusiano wa karibu ya kihisia kati ya watu wawili, bila ya kuwapo kwa hisia za kimapenzi au mvuto wa kimwili.

Hili ni jina lililotokana na mwanafalsafa wa Kigiriki, Plato, ambaye alielezea aina ya upendo unaozingatia kiroho, maadili, na ushirikiano wa kina wa mawazo. Marafiki wa kiplatoniki hushirikiana kwa kiwango kikubwa cha uaminifu, msaada, na uelewano,  hali ambayo huleta amani na utulivu wa ndani.


Sababu za uhusiano huu

Kwanini upendo wa kiplatoniki unapewa kipaumbele siku hizi? Tuone sababu:

Mosi, kuchoshwa na visa vya uhusiano. Katika zama za  mapenzi ya mitandaoni na mizunguko isiyoisha ya uhusiano wa kimapenzi, watu wengi wamechoka kuvunjwa moyo, kutokuwa na uhakika wa uaminifu, na mahitaji ya kimapenzi yasiyo na uwiano.

Hivyo watu hawa wanaelekeza nguvu zao kwa marafiki wa kweli,  wanaowapa faraja bila masharti au matarajio ya kimwili.

Pili, mahitaji ya kihisia yasiyohusiana na ngono. Binadamu wote tunahitaji kusikilizwa, kueleweka, na kuwa na mtu wa kushiriki naye maisha.

Si lazima hili lifanyike kwenye uhusiano wa kimapenzi. Marafiki wa ‘kiplatoniki’ wanaweza kutimiza nafasi hii kwa namna ya kipekee isiyohitaji kugeuka kuwa wapenzi.

Tatu, ushirikiano wa kudumu. Utafiti umeonyesha kuwa baadhi ya marafiki wa muda mrefu hushinda hata wapenzi katika suala la msaada wa kihisia.

Urafiki hujengwa kwenye msingi wa kufahamiana kwa kina, kuvumiliana, na kupitia changamoto pamoja, hali ambayo hujenga uhusiano thabiti  na wa kudumu.

Nne, kupungua kwa msukumo wa ndoa au uhusiano wa lazima. Kizazi cha leo kinavunjilia mbali matarajio ya kijamii ya kuwa katika ndoa au uhusiano wa kimapenzi ili kuwa “kamili.”

Watu wanajifunza kuwa furaha haihitaji mpenzi, bali inaweza kupatikana kupitia marafiki walioko tayari kwa hali zote.


Nguvu ya marafiki hawa maishani

Marafiki wa kweli hutoa msaada mkubwa wakati wa huzuni, matatizo ya kifamilia, changamoto kazini, au hata katika kipindi cha mafanikio.

Wanaweza kuwa watu wa kwanza kufika hospitali unapougua, au wa kwanza kukupongeza unapopata kazi mpya.

Tofauti na wapenzi, marafiki hawa hawana hofu ya kupoteza nafasi yao kwa sababu ya tofauti ndogo.

Amina Swedi anayesoma chuo kikuu mkoani Mwanza anasema: "Rafiki yangu wa kiplatoniki ni zaidi ya dada kwangu. Nimempigia simu nikiwa na wasiwasi saa nane  usiku na hakuwahi kunikataa. Tumevumiliana katika misukosuko mingi ambayo wapenzi wangu hata hawakufahamu nayo."


Changamoto zake

Ingawa urafiki huu una nguvu kubwa, si rahisi kuuelewa na kuuheshimu katika jamii inayoweka mapenzi ya kimapenzi mbele.

Wapo wanaoshindwa kuelewa kuwa wanaume na wanawake, au watu wawili wa jinsi moja, wanaweza kuwa karibu sana bila kuvuka mipaka ya mapenzi.

Wakati mwingine, jamii huwatazama marafiki wa kiplatoniki kwa shaka. Watu baki husema lazima kuna jambo linaloendelea kisiri kwa watu hao.

Mitazamo hii isiyo sahihi huleta presha kwa uhusiano wa aina hiimna wakati mwingine,  huharibu kabisa urafiki uliokuwa mzuri.

Unawezaje kudumisha urafiki huu?

Moja, weka mipaka iliyo wazi. Eleza kwa uwazi nia ya urafiki huo ili kuepuka mivutano ya kihisia.

Mbili, thamini nafasi ya rafiki yako. Onyesha shukrani kwa uwepo wake, msaada, na usikivu wake.

Tatu, jali uaminifu na uadilifu, ukikumbuka kuwa kama ilivyo katika uhusiano wowote, usaliti wa kihisia au kusema uongo, unaweza kuharibu kila kitu.

Nne, usikubali presha ya jamii. Kama urafiki huo unakupa furaha na kutosheka, usiruhusu watu wa nje kukuvuruga.

Katika dunia iliyojaa mapenzi ya kupita, kutokuaminiana na mashinikizo ya kijamii, upendo wa kiplatoniki unatoa nafasi ya pumziko.

Ni aina ya uhusiano unaojengwa kwa misingi ya uaminifu, msaada na uelewano wa kina. Ni muhimu kutambua kuwa si kila uhusiano wa karibu unahitaji kugeuka kuwa wa kimapenzi.

Marafiki wa kweli ni hazina ya thamani ambayo haipaswi kupuuzwa. Katika ulimwengu unaobadilika kila siku, huenda wao ndio wapenzi wa kweli tuliowasahau.