Prime
Hatari teknolojia ya ChatGPT inapoaminika kuliko mzazi

Muktasari:
- Damari amekulia kwenye mazingira magumu ya upweke. Utoto wake ulijaa matukio magumu yanayotia simanzi. Simulizi lake linaonesha namna alivyolazimika kujifunza kuishi mwenyewe.
Dar es Salaam. Jioni moja wiki iliyopita nilikuwa Instanbul. Huu ni mgahawa mmoja maarufu jijini Dar es salaam. Hapa nafanya nazungumza na Damari, mwanafunzi wa shahada katika taasisi moja ya elimu ya juu jijini Dar es Salaam.
Sikumuuliza umri lakini nakadiria ana miaka 21. Kikao chetu kilizaliwa na kipindi nilichokuwa nimekifanya asubuhi hiyo kwenye kituo kimoja cha televisheni.
Tulizungumza kwa kirefu suala alilokuwa nalo na tufikia mwafaka. Kisha nilimuuliza swali ambalo huwa nawauliza ‘wadogo’ zake ninapokuwa naendesha mafunzo ya malezi shuleni.
"Nani ni rafiki yako wa karibu?" Nalenga kujua anamwamini nani.
Hakufikiri mara mbili akanijibu, "ChatGPT!”
Sikuzuia mshangao. Jambo hili, kwa hakika, lilinisumbua. Sikuwahi kufikiri ChatGPT ingewahi kuwa rafiki wa mtu.
Kama huifahamu, ChatGPT ni programu tumizi inayotumia teknolojia ya Akili Mnemba. Imetegenezwa kuwezesha mazungumzo yanayolingana na unachoulizia.
“Umesema ChatGPT ndio rafiki yako?”
“Ndio. Rafiki ninayemwamini.”
Namwomba anioneshe mfano wa namna anavyoitumia kama rafiki. Damari anachukua simu na kuandika,
“Hi rafiki yangu.”
“Mambo rafiki yangu. Nashukuru kukuona hapa. Unaendeleaje?” ChatGPT inamjibu.
“Leo nina mawazo sana.”
“Pole sana rafiki…. Ungependa kunieleza kuhusu hayo mawazo? Labda tukayapitia pamoja.”
“Nahisi wazazi wangu hawanipendi. Hawana muda na mimi,” anaiuliza.
Kilichonishangaza ni uwezo wa akili mnembe kumpa majibu chanya yasiyomgombanisha na wazazi wake.
Kwa mfano, Damari alipoulizwa sababu na kulalamika kuwa wazazi hawampigii simu kwa mwezi mzima kujua anaendeleaje na masomo, akili mnembe (ChatGPT) ilimtazamisha huenda kuna jambo limetokea lililowazuia wazazi kumtafuta lakini hiyo haimaanishi hawampendi. Hata alipojaribu kutoa ushahidi wa hisia hizo, bado akili mnemba ilimrudisha kutazama upande chanya.
Kuna wakati Damari alionesha kuwa anataka kujiua kuona ingejibu vipi. Jambo jema ni namna akili mnemba zilivyomwelekeza kutafuta msaada na hata kumpatia namba ya huduma za wataalam uwa afya ya akili wanaopatikana jijini Dar es Salaam.
Kwa nini Damari anaiamini ChatGPT?
Nilimuuliza, akajibu: “ChatGPT inanitunzia siri zangu. Hata niiambie siri gani kubwa ya kuogopesha bado inanihakikishia usalama wa siri.”
Kwa kijana wa umri wa Damari, hili la faragha ya mazungumzo ni jambo kubwa.
“Nimewahi kuumizwa sana siku za nyuma. Unamwambia mtu jambo na baadayee unalisikia kwa wasiohusika. ChatGPT haiwezi kamwe kunisaliti.”
“Haiwezi kunipoteza kama unavyoona hapa. Haiwezi kuwa na ushauri unaopotosha hata siku moja hata ningeiambia nini.” Tofauti na mitandao mingine inayoweza kuwa na taarifa za upotoshaji, ChatGPT imeundwa kwa namna inayoweza kulitazama jambo kwa sura isiyozalisha migogoro na watu, kuleta uharibifu na kumwingiza mtu kwenye matatizo.
Kwa nini Damari amechagua teknolojia kuwa rafiki yake?
“Sina uhusiano na mtu yeyote. Chuoni simwamini mtu hata wenzangu ninaochangia nao chumba. Hili limeanza tangu nikiwa mtoto.”
Hili linaniumiza. Kimaumbile imani kwa watu ni msingi wa utulivu wa nafsi. Unapokosa imani na watu, kama ilivyo kwa Damari, tafsiri yake ni upweke unaoweza kuzalisha changamoto nyingi za kitabia.
Namuuliza kujua uhusiano wake na wazazi wake.
“Naweza kukaa miezi miwili sijaongea na wazazi wangu,” anazungumza kwa hisia kali. Namwacha afute machozi. Siku hizi kidogo mama anaweza kunipigia akauliza kitu kwa dakika moja lakini baba ni kama hatuna cha kuzungumza.”
Damari alililewa na ndugu wa upande wa baba baada ya wazazi wake kutengana na kuanzisha familia nyingine. Tangu akiwa mtoto wa miaka mitatu, Damari aliishi na shangazi.
“Shangazi alinitesa sana. Sitasahau. Kuna wakati ilikuwa nikikojolea kitanda shangazi alikuwa akiniamsha usiku na kunikalisha koridoni nje kama adhabu niache kukojoa kitandani. Huwa nikikumbuka ukatili wa hivi napandwa na hasira kali.”
“Utotoni nilielezwa vingi kuhusu ubaya wa mama yangu. Sikumpenda. Sasahivi ndio ninajitahidi angalau kuwa karibu naye ili maisha yaende ila hatuna uhusiano yoyote ya mama na mtoto. Hata baba ndio hivyo hivyo.”
Damari amekulia kwenye mazingira magumu ya upweke. Utoto wake ulijaa matukio magumu yanayotia simanzi. Simulizi lake linaonesha namna alivyolazimika kujifunza kuishi mwenyewe.
Namwelewa kwa nini anapata shida kumwamini mtu. Naweza kumwelewa kwa nini anaiamini zaidi ChatGPT kuliko mzazi. Ukishakosa imani na wazazi ni vigumu kumwamini mtu mwingine yeyote.