Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hakuna mtoto anayezaliwa na ukorofi

Juzi nimepokea taarifa za kusikitisha. Baraka mtoto wa jirani yetu enzi hizo amekuwa kilema. Jicho lake moja limeng’olewa, hana mkono moja, uso umejawa makovu shauri ya vipigo vya ‘wananchi wenye hasira kali.’ Sikushangaa kusikia Baraka anadaiwa kuwa jambazi sugu, anayetishia usalama wa watu na mali zao. 

Inadaiwa, kwa miaka mingi tangu awe mtu mzima, Baraka amekuwa akishiriki matukio mengi ya kihalifu ikiwa ni pamoja na ubakaji, unyang’anyi wa kutumia mabavu na matumizi makubwa ya madawa ya kulevya.

Kwa nini Baraka amefikia hapo? Tumbebeshe Baraka lawama zote? Kwa jicho la ‘haki’ tunaweza kusema Baraka alichagua maisha ya ukatili na kutokuwa na huruma na watu. Kwamba Baraka alikuwa na uhuru wa kuchagua kuwa mtu mwema, muungwana kama walivyo wengine. Lakini je, ni kweli mazingira ya malezi yalimpa Baraka uhuru huo?

Tafiti zinaonesha kuwa majambazi wengi na watu walioshiriki kufanya matukio ya kikatili hawakuzaliwa na ukatili huo. Hakuna mtoto anayezaliwa kibaka, mhuni, mkorofi na jambazi. Sote tunazaliwa na wema ndani yetu. Nini kimeuondoa wema aliozaliwa nao Baraka?

Nilimfahamu Baraka kama jirani yetu. Maisha yake ya nyumbani yalitawaliwa na ghasia tupu. Mbali na kuwa mgomvi kwa karibu kila mtu, Baraka alikuwa na uwezo wa kujibizana na wazazi wake na hata ikibidi kukabiliana nao kibabe pale walipotaka kumuadhibu. Ilikuwa kawaida kumsikia Baraka akipiga mayowe saa za jioni. Wakati mwingine yalikuwa ni majibizano makali ya maneno kati yake na kaka zake, baba au mama.

Nakumbuka si mara moja Baraka alijikuta akilala barazani akiwa amefungwa mikono na miguu kwa kamba. Ilikuwa ni adhabu kali yenye udhalilishaji mkubwa kwa mtoto mwenye umri kama wake. Ingawa wazazi wake walifikiri wanatumia njia sahihi kumrekebisha, ni dhahiri walijeruhi moyo wake kuliko kumsaidia. Kadri walivyomdhalilisha, ndivyo Baraka alivyozidi kuwa ‘gaidi,’ ‘haambiliki’, ‘kichwa ngumu.’

Watalaam wa tabia wamebaini mchango wa mazingira ya kimalezi katika kuamua tabia ya mtoto. Mzazi mkali, mwenye mbavu, asiyejali hisia za mwanae, kama ilivyokuwa kwa baba yake Baraka, yana nafasi kubwa ya kukuza mtoto mwenye tabia zisizokubalika katika jamii.

Maumivu anayoyapata mtoto yana nguvu ya kuamua mustakabali wake atakavyokuwa mtu mzima. Ukorofi wa mtoto mara nyingi ni ujumbe. Ni muhimu wazazi kuuelewa ujumbe huu kabla hawajafanya maamuzi ya aina gani ya adhabu waitoe. Ukorofi, mathalani, ni lugha ya mtoto kusema ndani yake anajisikia utupu. Hisia zake hazijapata mtu wa kuzisikiliza. Anapofanya ukorofi wake, kimsingi anatuambia kwamba sisi tunaomzunguka hatujatambua hisia zake. Ndani yake mna sauti inayomwaminisha kuwa hatambuliki. Imani hiyo potofu huchochea jitihada za kutafuta kutambulika kwa namna isiyokubalika.

Ugomvi, udokozi na ghasia nyingine anazofanya –wakati mwingine bila hata yeye kuchagua kivile– ni namna ya kujirudishia mamlaka anayoamini hana. Anapobishana na mzazi, anapogombana na wenzake, kama alivyofanya Baraka, kimsingi anajaribu kujiliwaza kuwa na yeye bado anauwezo wa kupambana kama wengine.

Mtoto wa namna hii, kama ilivyokuwa Baraka, huishia kuwa na hisia zilizokufa hali inayoweza kumfanya awe tayari kufanya chochote bila kujali maumivu anayoyasababisha kwa wengine. Bahati mbaya, kadri anavyowaumiza wengine, ndivyo anavyojisikia unafuu ndani yake kwamba na wengine nao wanaumia kama anavyoumia yeye.

Matukio ya ukatili yanayoendelea kwenye jamii yetu, yanaweza kuwa na mzizi kwenye aina ya malezi tunayowapa watoto wetu. Matumizi ya mabavu kupita kiasi, adhabu kubwa zinazoumiza mno hisia za watoto, zinaweza kuwa mbegu mbaya itakayozalisha watu wasiojali hisia za wengine, watu watakaokuwa tayari kuumiza wengine na hata ikibidi, kuwatoa roho ili tu kuridhisha nafsi zao kwamba nao wana uwezo wa kufanya matendo ya ‘kishujaa’ yatakayowanyoosha wengine.

Tunahitaji kutambua kwamba watoto, bila kujali makosa yao, wanaelewa vizuri zaidi lugha ya upendo inayojali hisia zao kuliko adhabu kubwa tunazowapa. Tukijenga mazoea ya kuumiza hisia za mtoto, tunatengeneza kizazi cha watu watakaofurahia kuwaumiza watu wengine wakiamini kufanya hivyo ni ushujaa. Tusisubiri watu watafute ushujaa kwa kuumiza wengine. Tuchukue hatua.