Wanafunzi UDSM wabuni mfumo wa kutoa msaada wa kisheria kwa WhatsApp

Muktasari:
- Kupitia mfumo huo, mwananchi anaweza kuuliza jambo lolote linalohitaji ufafanuzi wa kisheria na kujibiwa ndani ya muda mfupi bila ya gharama zozote.
Dar es Salaam. Wanafunzi wa sheria katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wamebuni mfumo unaoweza kutoa huduma ya msaada wa kisheria kwa njia ya WhatsApp.
Kupitia mfumo huo walioupa jina la “CLC Legal Bridge Platform” ambao kwa sasa unapatikana kwa njia ya WhatsApp pekee kupitia namba 0745118253, mtu anaweza kuuliza jambo lolote linalohitaji ufafanuzi wa kisheria na kujibiwa ndani ya muda mfupi bila ya gharama zozote.
Pia, kupitia mfumo huo, anaweza kuunganishwa moja kwa moja na watoa huduma za kisheria.
Akizungumza leo Juni 5, 2025 wakati wa hafla ya ‘Carrier Day’ iliyoandaliwa na Shule Kuu ya Sheria, mmoja wa wanafunzi waliobuni mfumo huo, Possi Hamisi amesema kilichowasukuma kuanzisha mfumo huo ni baada ya kubaini ombwe lililopo kwa wananchi kuhusu masuala ya kisheria.
“Tuligundua kuwa watu wengi wanakumbwa na changamoto za kisheria lakini hawajui kabisa kuwa ni masuala ya kisheria. Mfano, mtu anaweza kubakwa lakini akaenda kanisani kuombewa badala ya kuripoti tukio hilo ili mamlaka husika ziweze kuchukua hatua,” amesema.
Kwa mujibu wa Hamisi, wazo la mfumo huu lilianza kwa kutengeneza video fupi zenye maudhui ya kisheria ili kuwafundisha watu kuhusu masuala ya kijamii na haki zao.
Amesema baadaye waliona haja ya kuja na mfumo rahisi wa kufikisha elimu na huduma mbalimbali za kisheria moja kwa moja kwa wananchi.
“Ndipo tulipata wazo la kuja na mfumo unaotumia WhatsApp, jukwaa ambalo linafahamika na kutumiwa na watu wengi nchini, mtu anaweza kuwasiliana na mfumo huo ambao umeunganishwa na ‘Chatbot’ inayojibu maswali ya kisheria papo kwa papo.
“Endapo shida ni kubwa au inahitaji msaada wa wakili, huduma kwa wateja huchukua nafasi na kumuunganisha mhitaji na wakili anayehusika na utatuzi wa changamoto husika,” ameeleza mwanafunzi huyo.
Mwitikio wa watumiaji
Hamisi amesema tangu mfumo huo ulipozinduliwa mwaka 2022 na kuanza rasmi kufanya kazi, mwaka 2023, tayari umeshahudumia zaidi ya watu 4,000 kwa njia hiyo ya WhatsApp.
Ameseme wanatarajia kuboresha zaidi huduma hizo ili zipatikane kupitia App maalumu ambayo itawasaidia wananchi hata kupata nyaraka mbalimbali kama mikataba na hati nyingine muhimu za kisheria.
Pia, wanakusudia kuwawezesha wananchi wasiotumia huduma za intanenti kupata elimu na msaada wa mambo mbalimbali ya kisheria kwa njia ya ujumbe mfupi (SMS).
“Tunataka kuwa daraja kati ya mwananchi wa kawaida na msaada wa kisheria. Mtu aweze kuelewa tatizo lake, ajue pa kwenda na afuatilie kwa urahisi. Tunaamini hakuna mtu anayepaswa kukosa haki yake kwa sababu tu ya kutojua,” amesisitiza
Akizungumza katika hafla hiyo akiwa mgeni rasmi, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson amesema ubunifu huo umelenga kusaidia wananchi wasiokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu huduma mbalimbali za kisheria, kwa kuwawezesha kueleza changamoto zao kupitia mfumo wa kidijitali na kupokea ushauri wa hatua za kuchukua.
“Kwa kweli nimefurahi kuona wanafunzi wetu wanatumia ujuzi wao kutatua changamoto za jamii. Wametengeneza mfumo mzuri ambapo mtu anaweza kuingia, kueleza tatizo lake na kupokea ushauri wa hatua za kuchukua au wapi anapotakiwa kwenda kupata msaada wa kisheria,” amesema Dk Tulia.
Amesema uwepo wa bunifu kama hizo zinazofanywa na wanafunzi au wahitimu, zinaongeza ushiriki wao katika kutatua changamoto za jamii na kuimarisha taaluma zao kwa vitendo.
Dk Tulia amewataka wanafunzi pamoja na wahitimu wa vyuo vikuu nchini kutumia maarifa wanayoyapata vyuoni kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii.
Awali, alipongeza utaratibu uliowekwa na chuo hicho wa kuandaa siku maalumu inayowakutanisha wanafunzi na wadau mbalimbali katika fani husika.
Ametoa wito kwa vyuo vingine vikuu nchini, hasa shule nyingine za taaluma mbalimbali, kuiga mfano huo, ili kuwajenga wanafunzi kuwa tayari kukabiliana na hali halisi ya ajira na mahitaji ya jamii.
“Tusisubiri hadi mwanafunzi amalize miaka minne au mitano ndipo aseme hakutayarishwa kwa ajili ya mazingira halisi ya ajira,” amesema.
Naye Naibu Makamu Mkuu wa Chuo- Taaluma, Profesa Bonaventure Rutinwa amesema ushirikiano kati ya vyuo, wadau mbalimbali wa fani husika na jamii ni muhimu katika kumuandaa mhitimu kuwa mahiri.