Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

UDSM kujenga jengo la kisasa la uwekezaji kwa Sh8.3 bilioni

Muktasari:

  • Katika mradi huo, kutajengwa majengo yenye urefu wa ghorofa mbili, katika eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 12,498.5 na unatarajiwa kugharimu Sh8.3 bilioni na utachukua miezi 18 hadi kukamilika kwake.

Dar es Salaam. Wakati Watanzania wakiendelea kufurahia uwekezaji katika mradi wa Mlimani City, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kinatarajia kuanzisha mradi mpya wa kisasa wa majengo utakaokiwezesha kuvuna mapato yanayokaribia Sh2 bilioni kwa mwaka.

Uwekezaji huo mpya utafanyika ndani ya chuo hicho na katika mradi huo utakaopewa jina la Hill Park, chuo hicho kitashirikiana na Shirika la Watumishi House Investment (WHI) kutekeleza mradi huo.

Katika mradi huo, kutajengwa majengo yenye urefu wa ghorofa mbili, katika eneo lenye ukubwa wa mita za mraba 12,498.5 na unatarajiwa kugharimu Sh8.3 bilioni na utachukua miezi 18 hadi kukamilika kwake.

Akizungumza leo Jumatatu Mei 26,2025 wakati wa kutiliana saini mkataba wa makubaliano hayo, Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa William Anangisye amesema mara baada ya kukamilika kwa jengo hilo kutakuwa na huduma mbalimbali ndani yake ikiwemo kumbi za mikutano, maduka makubwa na maeneo ya kuoshea magari.

“Huduma nyingine ni maeneo ya kufanyia mazoezi (gym), huduma za udobi, vyumba vya ofisi na michezo ya watoto,” amesema makamu huyo mkuu wa chuo.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa WHI, Sephania Solomon amesema wanaelewa chuo kinapata wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi, hivyo ni lazima kuwe na jengo la kisasa la kutoa huduma.

Akieleza namna walivyoshirikiana, Solomon amesema waliosanifu mchoro wa jengo ni chuo na wao walichofanya ni kuuboresha kidogo ili jengo lilete mapato makubwa.

Hata hivyo, amesema mbali na kujenga pia, WHI watauendesha mradi huo kwa miaka 15 kabla ya kuukabidhi kwa chuo moja kwa moja.

“Mbali ya kujenga, tutauendesha mradi kwa miaka 15 na tunaahidi kuendeleza ushirikiano katika miradi mingine ya miliki,” amesema.

Naye Mkurugenzi wa Mipango, Maendeleo na Uwekezaji wa UDSM, Profesa Siasa Mzenzi amesema hawatarajii ujenzi wa jengo hilo kuchukua muda zaidi ya uliopangwa.

“Tunaamini ujenzi huu utaisha ndani ya muda tuliokubaliana kwani ukiacha huu tuna miradi mingine mingi, hivyo niwahakikishie WHI huu hautakuwa wa mwisho kushirikiana nao,” amesema Profesa Mzenzi.

Pia, amesema kwa kuwa mradi huo ni wa P to P (Public to Public), haimaanishi kuwa hawatashirikiana na sekta binafsi, bali watafanya hivyo kila inapobidi,” amesema mkurugenzi huyo.

Awali, Mkurugenzi wa Fedha na Uwekezaji wa WHI, Paskali Massawe amesema mradi huo umebuniwa kwa ajili ya miaka 50 ijayo huku gharama za uendeshaji zitabebwa na mradi wenyewe.

Wakati kuhusu mapato amesema asilimia 40 yataenda UDSM na 60 iliyobaki watachukua WHI.