Veta Dar yawaita vijana kuchangamkia mafunzo bure
Muktasari:
- Mafunzo haya yatakayowanufaisha jumla ya vijana 5,000 kutoka halmashauri tano za Jiji la Dar es Salaam yanatolewa kupitia Programu ya Mama Samia.
Dar es Salaam. Ofisi ya Veta Kanda ya Dar es Salaam, Chuo cha Chang’ombe, imetangaza fursa za mafunzo bure kwa vijana kupitia Programu ya Mama Samia ya Utambuzi na Urasimishaji wa Ujuzi, hatua inayolenga kuwawezesha wananchi kupata stadi za kazi na kujiajiri.
Kwa mujibu wa tangazo lililotolewa na ofisi hiyo, jumla ya fani 10 zitahusika katika awamu ya kwanza ya programu hiyo huku kila wilaya ya Mkoa wa Dar es Salaam ikitakiwa kuwa na wanafunzi 1,000 watakaonufaika na mafunzo hayo.
Tangazo hilo limewataka wananchi wenye sifa kujitokeza mapema kuwasiliana kupitia namba zilizotolewa ili kupata taarifa zaidi kuhusu usajili na ratiba za mafunzo hayo.
Wilaya zitakazonufaika ni Kigamboni, Ubungo, Ilala, Temeke na Kinondoni.
Tangazo hilo limeeleza kuwa mafunzo hayo yatatolewa bila malipo ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan za kuwainua vijana kiuchumi kupitia elimu ya ufundi stadi.
Fani zilizotajwa katika programu hiyo ni pamoja na umeme, useremala, ushonaji na teknolojia ya nguo, ufundi magari, ufungaji na utandazaji bomba, pamoja na utengenezaji wa bodi za magari.
Fani nyingine ni uashi, uungaji na uundaji vyuma, uandaaji wa mapishi ya vyakula pamoja na mauzo ya huduma ya chakula na vinywaji.
Hatua hiyo inakuja wakati mahitaji ya ajira na ujuzi wa kazi yakiendelea kuongezeka nchini, huku wataalamu wa maendeleo wakisisitiza umuhimu wa vijana kupata stadi zinazoweza kuwasaidia kujiajiri badala ya kutegemea ajira rasmi pekee.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi wameeleza kuwa programu hiyo inaweza kuwa msaada mkubwa kwa vijana ambao hawakupata nafasi ya kuendelea na elimu ya juu.
“Kama hilo litafanyika itakuwa jambo jema kwa sababu vijana wengi wana vipaji lakini wanakosa nafasi za mafunzo kutokana na gharama. Mafunzo haya yatawasaidia kupata kipato,” amesema Hassan Mallya mkazi wa Temeke.
Kwa upande wake, Rehema Mushi, mkazi wa Ubungo, amesema hatua hiyo inaweza kusaidia kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana wengi waliomaliza shule lakini hawana ujuzi wa kazi.
“Wapo vijana wengi mtaani wamekaa nyumbani kwa muda mrefu bila kazi. Wakipata ujuzi wa ufundi wanaweza kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa,” amesema Rehema.
Naye Salum Khamis wa Kigamboni amesema mafunzo hayo yatawasaidia vijana wengi kujenga kujiamini na kuona thamani ya kazi za ufundi ambazo kwa muda mrefu zilionekana hazina hadhi kubwa katika jamii.
“Zamani watu wengi walikimbilia ajira za ofisini pekee, lakini sasa vijana wanaanza kuona hata kazi za mikono zinaweza kuwapa maisha mazuri,” amesema Khamis.
Akizungumzia hilo mchambuzi wa masuala ya ajira na maendeleo ya vijana, Bakari Mwinyi amesema hatua ya kutoa mafunzo bure ni muhimu lakini kuna haja ya kuhakikisha wahitimu wanapatiwa mazingira ya kuendeleza ujuzi wao baada ya mafunzo.
“Mafunzo pekee hayatoshi kama vijana hawatapata mitaji, vifaa au masoko ya kazi. Ni muhimu kuwe na mfumo wa kuwaunganisha na fursa za kiuchumi baada ya kuhitimu,” amesema Mwinyi.