Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TET yajitosa kuelimisha matumizi ya akili bandia

Mkurugenzi wa TET Aneth Komba kulia akiwa na Mkurugenzi wa Tanzania AI Community, Essa Mohamedali wakisaini mkataba wa ushirikiano wa kutoa mafunzo kwa walimu kwa njia ya akili mnemba.

Muktasari:

  • Makubaliano hayo yanayolenga kuimarisha matumizi ya majukwaa ya kidijitali katika shule za msingi na sekondari, yanatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya elimu kwa kuongeza ubunifu, ufanisi na usawa katika upatikanaji wa maarifa kwa walimu na wanafunzi.

Dar es Salaam. Walimu na wanafunzi nchini wanatarajia kunufaika na mkataba mpya uliosainiwa kati ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) na Kampuni ya Tanzania AI Community, wenye lengo la kuboresha mbinu za ufundishaji na ujifunzaji kwa kutumia teknolojia ya akili bandia (AI).

Makubaliano hayo yanayolenga kuimarisha matumizi ya majukwaa ya kidijitali katika shule za msingi na sekondari, yanatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika sekta ya elimu kwa kuongeza ubunifu, ufanisi na usawa katika upatikanaji wa maarifa kwa walimu na wanafunzi.

Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba huo leo Mei 9, 2025 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa TET, Dk Aneth Komba amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kitaifa wa kuhimiza matumizi ya teknolojia katika elimu.

“Lengo la makubaliano haya ni kuhakikisha tunaingiza matumizi ya akili mnemba katika ufundishaji na ujifunzaji. Tanzania AI Community kazi yao ni kutoa mafunzo kwa wakuza mitaala na walimu wote nchini kwa kutumia AI,” amesema Dk Komba.

Ameongeza kuwa TET itatoa nyenzo muhimu ikiwemo vitabu, mada na mitaala kwa kampuni hiyo ili kusaidia walimu kupata mafunzo stahiki kwa kutumia akili bandia, hatua aliyosema ni mapinduzi ya kweli katika elimu, hasa kwa kizazi kinachokua katika mazingira ya kidijitali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania AI Community, Essa Mohamedali amesema ushirikiano huo unaonyesha dhamira ya kweli ya serikali ya kuimarisha elimu kupitia teknolojia ya kisasa.

“Teknolojia ya AI itamrahisishia mwalimu kazi ya ufundishaji. Itawezesha hata kutunga maswali ya ubunifu na kutoa maudhui kwa wakati. Tunataka kuhakikisha walimu wote nchini, hata wa vijijini, wanapata fursa sawa ya kujifunza,” amesema Mohamedali.

Amesema pia kuwa kampuni hiyo itahakikisha elimu ya AI inafikishwa kwa walimu kwa njia rahisi, rafiki na inayozingatia mazingira halisi ya shule nyingi nchini.

Makubaliano hayo yanakuja wakati ambao dunia nzima inashuhudia mabadiliko ya haraka ya kiteknolojia na Tanzania kupitia TET imechukua hatua hiyo kama sehemu ya kujenga mfumo wa elimu unaokwenda sambamba na karne ya 21.

Kwa mujibu wa TET, utekelezaji wa mkataba huu utaanza mara moja kwa kufanya tathmini ya mahitaji ya walimu, kuandaa maudhui ya mafunzo, na kuweka mifumo ya ufuatiliaji ili kuhakikisha elimu inayotolewa kupitia AI ni bora, sahihi na jumuishi.