Mjadala elimu ya amali ulivyoteka Bunge

Muktasari:
- Wakichangia katika Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2025/2026, baadhi ya wabunge walionyesha shaka kuhusu uelewa wa wananchi kuhusu neno amali na namna Taifa linavyojiandaa kutoa wahitimu wenye ubora unaotarajiwa.
Dodoma. Elimu ya amali inatajwa kuwa ni nyenzo muhimu ya
kuwawezesha wanafunzi kupata ujuzi na hatimaye kumudu maisha yao.
Elimu hiyo itokanayo na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kutaka Tanzania kutoa mafunzo ya ujuzi, sio tu inajenga msingi wa kuwa na wahitimu walio tayari kuchangia maendeleo ya Taifa, bali kuandaa Watanzania katika soko la ajira la kimataifa.
Mpaka sasa Serikali imewezesha ujenzi wa shule mpya 103 za sekondari za amali ambazo zipo katika hatua mbalimbali za ujenzi.
Miongoni mwa shule hizo, 29 ni za amali za kihandisi na shule 74 ni za amali zisizo za kihandisi na kukamilika kwake kutafanya Tanzania kuongeza idadi ya shule za amali za sekondari kufikia 112.
Mkanganyiko
Hata hivyo, neno amali limeonekana kuwa na ukakasi na kuwatatiza baadhi ya watu wakiwamo wabunge.
Mkanganyiko upo katika tofauti yake na mafunzo ya ufundi ambayo kwa sasa yanatolewa na VETA karibu kila kona ya nchi.
Wakichangia katika Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka 2025/2026, baadhi ya wabunge walionyesha shaka kuhusu uelewa wa wananchi kuhusu neno amali na namna Taifa linavyojiandaa kutoa wahitimu wenye ubora unaotarajiwa.
Mbunge wa Singida Mjini, Mussa Sima anasema lazima Watanzania waelezwe na kupewa elimu juu ya elimu hiyo bila kufanya hivyo huenda wengi hawataona umuhimu wa elimu hiyo.
Sima ambaye kitaaluma ni mwalimu, anaonyesha shaka kuhusu watakapopatikana walimu wa kufundisha elimu hiyo.
Hofu yake inaungwa mkono na Mbunge wa Viti Maalum, Ng’wasi Kamani anayesema mfumo huo umechukuliwa kutoka mataifa ya Ujerunmani, Canada, Uswisi na China, ambayo hata hivyo yamefanikiwa kwa sababu yalijiandaa vema kwanza katika uwekezaji.
Kamani anasema kuwa mataifa hayo yamekuwa na mafanikio makubwa kwa sababu vijana wao wamefundishwa mambo mengi kuanzia katika viwanda vidogovidogo na hatimaye wakazifungua nchi zao kiuchumi.
“Kwa hiyo maandalizi yanatakiwa kwa maeneo mengi, kama tukiwekeza itasaidia nchi kufunguka kiuchumi lakini tunapaswa kuwa na angalau viwanda vidogo kwa kuanzia vijana wetu vinginevyo itakuwa ni ngumu kufikia malengo tarajiwa, kwani hakutakuwa na mafunzo stahiki ya vitendo," anasema na kuongeza:
" Kingine tuwatumie hata mafundi wabobezi kuwafundisha kwa vitendo wanafunzi wetu."
Mbunge huyo anashauri Taifa kujifunga mkanda kwenye bajeti zake kwani ikiwekeza vya kutosha katika Elimu hiyo, vijana wengi watakimbilia elimu hiyo.
Kwa upande wake Mbunge wa Tabora Kaskazini, anasema neno amali halieleweki kwani wengi wanachanganya elimu hiyo na ufundi mchundo au uhandisi, akisema bila kutoa elimu kwa umma, itakuwa kazi kubwa kuhamasisha jamii hata kama shule nyingi zitajengwa.
Kwa upande mwingine, aliishauri Serikali kuipa uzito elimu hiyo, kwa kuanza na shule chache inazoweza kuzimudu.
“Muhimu kuwa na karakana na vifaa vyote ndipo tuanze, lakini kuanza na shule nyingi kwa wakati mmoja tutajikuta tutatoa watu wasiokamilika. Tuanze na shule chache ili tujifunze na hizo ziwe na vifaa vya kutosha vyenye ubora kuliko kusubiri kuwa na wigo mpana, itatuharibia,”alisema Maige.
Profesa atamani walimu wa nje
Mbunge wa kuteuliwa, Profesa Shukrani Manya yeye alitaka Serikali kutoa walimu kutoka nje kwani ndiyo utakuwa mwanzo mwema katika elimu ya amali kwa vijana wa Tanzania.
Kwa hali ilivyo, Profesa Manya haoni mwanzo mwema katika shule hizo akitaja sababu moja ya ukosefu wa wahadhiri wabobezi wanaoweza kuwafundisha walimu.
“Tuanze kwa gharama kubwa ya kutafuta wahadhiri hata kwa kuazima kutoka nchi ambazo zilianza muda mrefu kwenye mpango huu, tuchukua watu waje kutusaidia na siyo aibu isipokuwa ni kwa Serikali kuamua kama inataka kuwa na kilicho bora,” alipendekeza.
Mwalimu wa Chuo cha Veta Agapiti Makata anasema elimu ya amali inawezekana isipokuwa lazima Serikali ianze kuwekeza kwa walimu.
Anasema kwa namna yoyote kuna ulazima wa kutafuta wataalamu ambao watakuja kuwekeza misingi ya ufundi lakini akaeleza Serikali isikwepe gharama hasa kwa wanafunzi wa mwanzo.
Waziri afafanua
Katika ufafanuzi wake kwa wabunge, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda anasema elimu hiyo itatolewa kwa kidato cha kwanza hadi cha nne cha sita.
Anasema kuna tofauti kati ya elimu ya amali na ufundi mwingine hasa kwa ngazi za juu.
Waziri anataja kuwa ufundi stadi siyo elimu ya ufundi japokuwa uhandisi ni sehemu ya ufundi amali ambapo Tanzania imeajiandaa kufundisha elimu hiyo katika kilimo, ukarimu na maeneo mengine.
“Katika maandalizi hayo tumejenga Polytecnicial katika mikoa ya Kigoma, Zanzibar, Mtwara, Mwanza,Morogoro na kingine cha Dodoma kimekamilika kwa sasa kimeunganishwa na taasisi ya ufundi Dar es Salaam,”alisema Profesa Mkenda.
Kuhusu wahadhiri kutoka nje, Waziri anasema Serikali haina tatizo kuingia mikataba na mataifa mengine ili kuwafapiga msasa walimu watakaofundisha elimu ya amali.
Kwa kuanza anakiri kuwa tayari Katibu mkuu wa Wizara hiyo alishakwenda nchi za India, Korea,China na Uswisi kwa ajili ya kujifunza zaidi namna ya kuanza mtalaa huo na kuufanyia maboresho.