Mambo sita kuboresha sekta ya elimu

Muktasari:
- Wadau wa elimu wamependekeza mambo sita kuboresha elimu, juma la elimu likizinduliwa mkoani Katavi.
Katavi. Wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine kuadhimisha juma la elimu, wadau wa elimu wamependekeza mambo kadhaa kufanyika kwenye sekta hiyo ikiwemo kuwekeza katika elimu inayolenga kujenga uwezo na stadi za maisha kwa vijana.
Wadau hao ambao wamekusanyika katika Halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi wakiadhimisha juma hilo wamesema Tanzania inahitaji mfumo wa elimu unaompa kijana uwezo wa kutumia maarifa yake kwa vitendo.
Akizungumza leo Mei 5,2025 wakati wa uzinduzi wa Juma la Kimataifa la Elimu (GAWE) lililoandaliwa na Mtandao wa Elimu Tanzania (Tenmet), Faraja Kota ambaye ni mwenyekiti wa mtandao huo, amesema katika dunia ya leo inayobadilika kwa kasi, maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila elimu yenye mwelekeo wa ujuzi.
Faraja amesema kauli mbiu ya maadhimisho hayo inayosema ‘Elimu na Ujuzi kwa Maendeleo ya Taifa’ inalenga kuangazia umuhimu wa kuwekeza katika elimu inayojenga uwezo na stadi za maisha kwa vijana, ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa uchumi wa taifa na maendeleo endelevu ya kijamii.
“Tunahitaji mfumo wa elimu unaompa kijana uwezo wa kutumia maarifa yake kwa vitendo, kuanzisha miradi ya kiuchumi, kushiriki katika ubunifu, na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya taifa,” amesema Faraja.
Amesema licha ya Tanzania kupiga hatua katika sekta hiyo na kupata mafanikio makubwa ikiwemo kuongezeka kwa uandikishaji wa watoto shule za msingi na sekondari, uboreshaji wa sera ya elimu na mafunzo, uboreshaji mitaala ili kuendana na mahitaji ya sasa, ujenzi wa miundombinu ya elimu, bado kuna changamoto mbalimbali.
Baadhi ya changamoto hizo ni ufinyu wa bajeti, ukosefu wa chakula shuleni, mimba za utotoni, ukatili dhidi ya wanafunzi, upungufu wa miundombinu, upungufu wa walimu.
Kukabiliana na changamoto hizo mtandao huo umependekeza kuimarishwa kwa elimu ya ujuzi na ufundi stadi (TVET).
“Serikali iongeze uwekezaji katika vyuo vya ufundi na programu za mafunzo kwa vitendo ili kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa wanapohitimu elimu ya sekondari.
“Pia tunapendekeza kuondolewa kwa adhabu ya viboko shuleni, tunashauri kuanzishwa kwa mbinu mbadala za malezi na udhibiti wa nidhamu zinazojali utu wa mtoto na kukuza mazingira salama ya kujifunzia,”amesema.
Mwenyekiti huyo amependekeza pia kuongezwa kwa bajeti ya elimu kufikia asilimia 20 ya bajeti kuu ili kuwezesha utekelezaji kikamilifu wa sera za elimu na kutoa huduma bora.
Lingine lililopendekezwa ni kufuatilia tathmini ya utekelezaji wa Mwongozo wa Kurudisha wanafunzi waliokatiza masomo na kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji ili kuhakikisha kila mtoto anapata nafasi ya kurejea shuleni na kuendelea na masomo yake.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa juma hilo, Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amekemea vikali mila ya chagulaga ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa watoto wa kike kukatisha masomo.
Mila hiyo inatekelezwa na kabila la Wasukuma walioweka makazi katika halmashauri ya Mpimbwe, ambapo wasichana hutekwa na kulazimishwa kuingia kwenye ndoa za utotoni.
“Kuna jambo linatusumbua hapa Mpimbwe hii mila chagulaga, ni wakati mwafaka wa kuikomesha mila hii ambayo inawatoa watoto wa kike kwenye mfumo wa elimu. Suala hili linaturudisha nyuma sana
“Tumeletewa shule sio kwa ajili ya kuangalia majengo, zimeletwa kumkomboa kifikra mtoto wa Kitanzania, kama tutaendekeza mambo ya chagulaga tutaendelea kugharimu maisha ya watoto wa kike,” amesema na kuongeza .
“Kuanzia sasa nataka uwepo mkakati wa kukabiliana na mila hii na wakati mkakati huo unatekelezwa kama wewe ni kijana kaoe mkubwa mwenzako usioe mwanafunzi.Tuache wanafunzi wapate elimu,”
Akizungumza hilo, Mwenyekiti wa mtandao wa wasichana wanaofadhiliwa na shirika la Camfed, Shamsa Mkurungo amesema kupitia programu mbalimbali zinazotekelezwa na shirika hilo kwa ajili ya wasichana, zinafanyika jitihada za kuhakikisha kundi hilo linabaki kwenye mfumo wa elimu.
“Tuna programu ya Dunia Yangu inayolenga kuwasaidia wanafunzi hasa kidato cha kwanza na cha pili kujifunza stadi za maisha zinazowasaidia kujitambua, kujijua wao ni nani na wanatakiwa kufanya nini, ili kufikia malengo yao waliyojiwekea,” amesema.