Kongole vyeti vya wahitimu kutumika kuombea mikopo
Muktasari:
- Kutambua vyeti kama dhamana ni sawa na kutambua kwamba akili na maarifa ni rasilimali muhimu kama zilivyo mali nyingine za kimwili.
Dar es Salaam. Katika hatua inayoweza kubadilisha maisha ya maelfu ya vijana nchini, tamko la serikali kuruhusu vyeti vya taaluma kutumika kama dhamana ya kupata mikopo linapaswa kupongezwa kwa dhati.
Hii ni hatua ya kihistoria inayogusa moja kwa moja wahitimu wa vyuo kama kundi ambalo kwa miaka mingi limekuwa likikumbana na vikwazo vikubwa katika jitihada za kujikwamua kiuchumi.
Kwa muda mrefu, mfumo wa kifedha nchini umekuwa na changamoto kubwa linapokuja suala la upatikanaji wa mikopo kwa watu wasio na dhamana kama vile nyumba, ardhi, au mali nyingine zisizohamishika.
Hali hii imekuwa kikwazo kikubwa hasa kwa vijana waliomaliza masomo yao lakini hawana ajira rasmi wala mali za kurithi au kumiliki.
Kwao, hata wazo la kuanzisha biashara au kampuni limekuwa ndoto ya mbali, si kwa sababu ya ukosefu wa ubunifu au maarifa, bali kwa sababu ya ukosefu wa mtaji.
Tatizo hili si la leo. Ni kero ya muda mrefu ambayo imekuwa ikirudiwa mara kwa mara katika mijadala ya kijamii na kiuchumi.
Wahitimu wengi wamejikuta wakibaki majumbani au kufanya kazi zisizoendana na taaluma zao kwa sababu tu hawana uwezo wa kupata mtaji wa kuanzisha miradi yao.
Benki na taasisi nyingi za kifedha zimekuwa zikisisitiza dhamana ngumu ambazo kwa kijana wa kawaida ni vigumu kabisa kuzipata.
Hivyo basi, mfumo huu uliwatenga vijana wengi waliokuwa na uwezo wa kuleta mabadiliko makubwa kiuchumi.
Kongole Serikali
Ndiyo maana uamuzi wa Serikali wa kuruhusu vyeti kutumika kama dhamana unapaswa kuonekana kama mwanga mpya.
Vyeti hivi ni ushahidi wa uwekezaji mkubwa ambao Taifa limeufanya kwa vijana wake yaani uwekezaji wa elimu, maarifa, na ujuzi.
Kutambua vyeti kama dhamana ni sawa na kutambua kwamba akili na maarifa ni rasilimali muhimu kama zilivyo mali nyingine za kimwili.
Hata hivyo, pamoja na pongezi hizi, kuna jambo moja muhimu ambalo haliwezi kupuuzwa: utekelezaji.
Mara nyingi tumeshuhudia sera nzuri zikishindwa kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa sababu ya utekelezaji dhaifu.
Taasisi za fedha zina jukumu kubwa katika kuhakikisha kuwa dhamira ya Serikali inafikiwa bila kuweka vikwazo vipya visivyo vya lazima.
Ni muhimu sana kuhakikisha kwamba benki na taasisi nyingine hazitengenezi masharti magumu yatakayofanya mpango huu ushindwe kufikiwa na walengwa.
Kama ilivyo, ajira ni changamoto kubwa nchini. Vijana wengi wanahitimu kila mwaka bila kuwa na uhakika wa kupata ajira rasmi.
Katika mazingira kama haya, mikopo inaweza kuwa chombo muhimu sana cha kuwawezesha kujiajiri kuanzisha biashara ndogo ndogo au hata kampuni zinazoweza kukua na kutoa ajira kwa wengine.
Hata hivyo, kama masharti ya mikopo yatakuwa magumu ikiwa ni pamoja na riba, ada nyingi au taratibu ndefu basi dhamira njema ya Serikali hii inaweza kupotea kabisa.
Vijana wataendelea kubaki nje ya mfumo wa kifedha, na tatizo litaendelea kama lilivyokuwa awali.
Elimu kwa walengwa na riba
Zaidi ya hayo, kuna haja ya elimu ya kifedha kwa wahitimu hawa. Kupata mkopo ni hatua moja tu; kuutumia kwa ufanisi ni hatua nyingine muhimu zaidi. Bila mwongozo sahihi, kuna hatari ya mikopo hii kutumika vibaya na kusababisha mzigo mkubwa wa madeni kwa vijana hawa.
Lakini pia kuna hoja nyeti na ya msingi ambayo haiwezi kupuuzwa: suala la riba. Mikopo inaweza kuwa na manufaa makubwa, lakini ikiwa itakuja na mzigo mkubwa wa riba, basi inaweza kugeuka kuwa mtego badala ya fursa.
Wahitimu wanaanza maisha yao ya kiuchumi; kuwabebesha mzigo mkubwa wa riba mapema kunaweza kuathiri uwezo wao wa kukua na kujiendeleza.
Ni vyema, ikiwezekana, mikopo hii ikatolewa kwa mfumo au masharti yasiyo na riba.
Hii itahakikisha kwamba lengo la kuwawezesha vijana linafikiwa bila kuwaweka katika hatari ya kudidimia kifedha.
Kwa ujumla, tamko la Serikali ni la kupongezwa na linapaswa kuungwa mkono na wadau wote.
Ni hatua inayoweza kufungua milango mipya ya fursa kwa vijana wa Tanzania. Lakini kama ilivyo kwa sera nyingi nzuri, mafanikio yake yatategemea utekelezaji wake.
Ikiwa utekelezaji utakuwa wa haki, wenye uwazi, na unaozingatia maslahi ya wahitimu, basi Taifa linaweza kushuhudia kizazi kipya cha vijana wabunifu, wajasiriamali, na wachangiaji wakubwa wa uchumi.
Hili si tamko tu la Serikali, ni nafasi ya kuandika upya hadithi ya ajira na uchumi wa vijana nchini.