Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Chahita: Walimu wa hisabati waongezewe malipo ya ziada

Muktasari:

  • Ufaulu wa somo la hisabati umekuwa hafifu miaka yote ikilinganishwa na masomo mengine katika mitihani ya Taifa ya kidato cha pili na cha nne, huku mzigo mkubwa wa ufundishwaji ukitajwa kuwa sababu.

Dar es Salaam. Wakati dunia ikitarajia kuadhimisha Siku ya Hisabati kesho Machi 14, Chama cha Hisabati Tanzania (Chahita) kimetaka walimu wa somo hilo waongezewe malipo ya ziada kutokana na mzigo wa kufundisha walionao.

Mbali na malipo, chama hicho kimeainisha changamoto saba ambazo bado ni mwiba kwa somo hilo, huku kikianisha mapendekezo yake ili kuimarisha ufaulu wa somo hilo.

Miongoni mwa changamoto hizo ni upungufu wa walimu kwa ngazi zote za elimu, hamasa ndogo kwa walimu na wanafunzi, kukatishwa tamaa kwa kauli, ubunifu mdogo kwa walimu katika ufundishwaji, na umahiri mdogo kwa walimu kwa baadhi ya mada.

Haya yameelezwa na Mwenyekiti wa Chahita, Dk Said Sima, alipozungumza na Mwananchi leo Alhamisi, Machi 13, 2025, ikiwa ni siku moja kabla ya maadhimisho hayo kufanyika.

Maadhimisho hayo yanafanyika wakati ambapo bado takwimu zinaonyesha kuwa ufaulu wa somo hilo katika mitihani ya Taifa ya kidato cha pili na cha nne umeendelea kuwa duni, jambo linaloonyesha kuwapo kwa haja ya kuwekwa nguvu ya ziada.


Hali ilivyo

Taarifa mbalimbali zilizowahi kutolewa na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), zimeonyesha kupanda na kushuka kwa ufaulu wa somo hilo katika miaka tofauti.

Katika mitihani ya kidato cha nne mwaka 2024, somo la hisabati, ufaulu wake wa alama A hadi C ulikuwa asilimia 11.71, ukiwa umeshuka kulinganisha na wa mwaka 2023 ambapo asilimia 12.75 walipata daraja A hadi C. Hii inamaanisha zaidi ya robo tatu ya wanafunzi 516,520 walipata alama D au F.

Kwa upande wa kidato cha pili, takwimu zinaonyesha kuwa ufaulu wake pia ni wa kusuasua. Hiyo ni baada ya waliopata F katika somo hilo kufikia asilimia 81.15, ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 78.92 iliyokuwapo mwaka 2023.

Hii inafanya waliopata daraja A hadi D kufikia asilimia 18.85 mwaka 2024, kutoka asilimia 21.08 iliyokuwapo mwaka uliotangulia.

Hata hivyo, uchambuzi unaonyesha kuwa kama wanaohesabiwa kufaulu wangekuwa ni wale wa daraja A hadi C, bado kwa mwaka 2023, ambao wangekuwa katika kundi hilo, ni asilimia 13.42 pekee ambayo ingekuwa ni ongezeko ikilinganishwa na asilimia 8.15 iliyokuwapo mwaka uliotangulia.

Kwa upande wa matokeo ya mtihani wa Taifa darasa la saba mwaka 2024, asilimia 55.12 ya watahiniwa 1,204,636 walipata daraja A hadi C, ikiwa ni ongezeko kutoka asilimia 48.83 iliyokuwapo mwaka uliotangulia.

Kwa upande wa matokeo ya upimaji darasa la nne, takwimu zinaonyesha kuwa asilimia 46.19 ya watahiniwa 1,530,456 waliofanya mtihani huo mwaka 2024 walipata daraja A hadi C, ikiwa ni ongezeko ikilinganishwa na asilimia 23.28 waliopata daraja hilo mwaka uliotangulia.


Changamoto

“Somo hili linakabiliwa na upungufu wa walimu kwa ngazi zote za elimu, jambo linalofanya wakabiliwe na idadi kubwa ya vipindi. Hali hii inawafanya washindwe kufundisha kwa ufanisi,” amesema Dk Sima.

Licha ya uchache wa walimu waliopo, bado kumekuwa na hamasa ndogo kwa walimu na wanafunzi katika somo la hisabati, huku kauli za kukatishwa tamaa zikisemwa juu yao.

“Miongoni mwa kauli hizi ni kusema hisabati ni somo gumu, jamii na makundi, hivyo kufanya watu kuwa na fikra hizi muda wote.”

Pia kumekuwapo na ubunifu mdogo kwa walimu katika ufundishwaji kutokana na kukosekana kwa mafunzo kazini, jambo linalowafanya wasiwe mahiri katika ufundishaji.

“Lakini pia kuna kukosekana kwa upendo na lugha nzuri kwa walimu. Hii inawafanya wanafunzi washindwe kulipenda somo.”

Umahiri mdogo wa ufundishaji unaofanya walimu kushindwa kumudu baadhi ya mada nao umetajwa kuwa changamoto inayofanya wanafunzi kushindwa kuelewa vyema somo hilo.

“Pia kuna changamoto za kijamii, ikiwa ni pamoja na mikopo mbalimbali yenye kuleta msongo wa mawazo kwa walimu na kuwafanya washindwe kufundisha vyema,” amesema Dk Sima.

Ili kubaliana na baadhi ya changamoto hizo, Chahita kimependekeza kuwapo kwa malipo ya ziada kwa walimu wa somo la hisabati, ili kuwatia moyo kutokana na mzigo mkubwa wa ufundishaji waliokuwa nao na kuwasaidia kuepuka mikopo itakayowafanya waingie kwenye msongo wa mawazo.

“Pia ni vyema kuwapo kwa takwimu sahihi za walimu na masomo yao, zitumike katika kubuni mpango maalumu wa kuwatumia walimu hao kufundisha,” amesema Dk Sima.

Pia, Chahita kimetaka somo la hisabati liwe kigezo kimojawapo cha ufaulu kwa daraja la kwanza na pili katika matokeo ya kitaifa ya kidato cha nne, ili kusaidia wanafunzi kufanya juhudi na kujituma.

“Pia, Chahita ipewe jukumu la kuratibu, kuhamasisha na kuendesha mafunzo ya hisabati kwa kila halmashauri za wilaya na manispaa kwa ufadhili wa Serikali,” amesema.

Pia, ili kupunguza tatizo la ushiriki hafifu katika mafunzo ya kitaifa, Chahita kimeitaka Serikali kupitia kila halmashauri au wilaya kila mwaka kugharamia mafunzo ya washiriki kumi, ambapo saba ni wa sekondari na wengine watatu wa shule za msingi, na wengine walipiwe na shule zao.


Maeneo mengine ya kuangaliwa

Kwa upande wake, Dk Said Sima amesema ili kuhakikisha haya yanafanikiwa, Serikali iendelee kuajiri walimu wa kutosha, kuboresha maslahi kulingana na mzigo wa ufundishaji kwa walimu wa hisabati.

Pia amesema ni vyema kuongeza upatikanaji wa vitabu na nyenzo za ufundishaji na kuhakikisha zinafika katika kila shule, hasa za vijijini.

“Ni muhimu sana shule hizi ambako kwa ujumla ufaulu wa shule huwa ni wa chini kidogo ukilinganisha na shule za mijini. Tunaunga mkono juhudi za Serikali katika kampeni za ‘kitabu kimoja mwanafunzi moja,’ lakini ni vyema ifanyike kwa usawa,” amesema Dk Sima.

Dk Sima pia ametaka kuongezwa kwa juhudi zaidi katika somo la hisabati kwa kushirikiana na Chahita na wadau wengine ili kuweka mikakati ya kuboresha uelewa na hatimaye kuongeza ufaulu.

“Ufaulu wa hisabati kutoka asilimia 20 hadi asilimia 25 ni hatua kubwa. Hata hivyo, bado hatujafikia kiwango cha chini cha hitajio la ufaulu wa dunia, ambacho ni asilimia 31 kilichowekwa na Benki ya Dunia. Hivyo tunahitaji mikakati imara ili kuweza kusonga mbele kwa lengo la kusaidia taifa letu,” amesema.

Katika hatua nyingine, wametaka kutolewa kipaumbele kwa somo la hisabati kwa wanafunzi kuongeza juhudi kutokana na uhitajio wake, ikiwemo Akili Mnemba (AI) ambayo ni matunda ya hisabati.

Matumizi ya Tehama nayo hayajaachwa nyuma, imeshauriwa kuongezwa kwa vifaa na elimu ya Tehama katika shule ili kupunguza baadhi ya changamoto na kuendana na hitajio la ulimwengu wa sasa.


Wasemavyo wadau

Akizungumza na Mwananchi, mmoja wa walimu wa somo hilo ametaka idadi yao iongezewe ili kupunguza mzigo wa ufundishwaji.

“Unaweza kuongeza hela kama motisha ndiyo walimu wakahamasika, lakini namna gani unaweza kufikisha yale maarifa sehemu husudiwa? Mtu una mikondo saba kwa siku; ni ngumu kufundisha kwa ufanisi,” amesema mwalimu huyo.

Mwalimu huyo anasema shule za mijini ndiyo za kuangaliwa zaidi kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi waliopo, huku walimu wengi wakiwa ni wa masomo tofauti na hisabati.

Uongezaji wa walimu liliungwa mkono na Vecensia Mnubi, ambaye ni mwalimu mstaafu, anakiri kuwapo kwa uhaba wa walimu katika shule nyingi.

“Ajira zinatangazwa ndiyo, lakini wanachukuliwa walimu wa masomo gani? Nafikiri ipo haja ya kuitisha sensa ya walimu wa hisabati waliopo nchini ili wote waajiriwe kuziba pengo lililopo,” amesema.