Mafuriko na ukame yanahitaji mipango kuepuka baa la njaa

Muktasari:
- Benki hiyo inasema watu wanaoishi chini ya Dola 1.25 za Marekani (takribani Sh3,000) kwa siku wataathirika zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Inasema, nchi saba kati ya 10 zilizo kwenye hatari zaidi duniani zinapatikana Afrika.
Tangu mwaka 1970, Afrika imekumbwa na zaidi ya majanga 2,000 yaliyoathiri zaidi ya watu milioni 460 na kuwajeruhi zaidi ya 880,000 na ifikapo mwaka 2030 takriban maskini milioni 118 watakuwa wameathiriwa na ukame, mafuriko, maporomoko ya ardhi na dhoruba, Benki ya Dunia inasema.
Benki hiyo inasema watu wanaoishi chini ya Dola 1.25 za Marekani (takribani Sh3,000) kwa siku wataathirika zaidi kutokana na mabadiliko ya tabianchi. Inasema, nchi saba kati ya 10 zilizo kwenye hatari zaidi duniani zinapatikana Afrika.
Nchi hizo ni Sierra Leone, Sudan Kusini, Nigeria, Chad, Ethiopia, Jamuhuri ya Afrika ya Kati na Eritrea. Chad imeanza kushuhudia athari hizo kwenye Ziwa Chad. Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) linasema ukubwa wa ziwa hilo umekuwa ukipungua kadri siku zinavyoenda.
Ziwa Chad lilikuwa na eneo lenye ukubwa wa takriban kilomita za mraba 25,000 mwaka 1963 lakini kwa sasa ni chini ya kilomita 2,500 jambo linaloathiri maisha ya watu zaidi ya milioni 50 ambao wanatarajiwa kuongezeka zaidi ya mara mbili ifikapo mwaka 2030.
Kwenye ripoti ya vipaumbele vya Afrika mwaka 2017 iliyotolewa na taasisi ya Brookings ya Marekani, mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa masuala yaliyopewa kipaumbele.
Taasisi hiyo inabainisha kwamba uhaba wa chakula ni miongoni mwa athari ambazo zitashuhudiwa kwa wananchi wengi hivyo kutaka jitihada za makusudi zichukuliwe kupunguza madhara yake.
Ripoti inaeleza, mpaka mwaka 2020 sekta ya kilimo ambayo inategemea mvua itaathirika hivyo kuathiri upatikanaji wa chakula kwa takriban asilimia 50. Asilimia 94 ya kilimo cha Afrika kinategemea mvua.
Takwimu za Shirika la Afya zinaonyesha kilimo kinazalisha chakula cha watu bilioni 7.3 duaniani kote ingawa takriban milioni 800 hawapati lishe inayokidhi mahitaji ya mwili.
Ndani ya muda huo, kati ya watu milioni 90 mpaka 220 watakumbwa na uhaba wa maji kutokana na kupungua kwa vyanzo vya maji. Zitakuwapo athari za kiafya pia. Magonjwa ya mlipuko yatatokea na kuathiri mamilioni ya Waafrika.
Kuongezeka kwa kina cha bahari ni miongoni mwa athari nyingine ambazo licha ya kuingilia shughuli za uvuvi, usafirishaji na miundombinu iliyopo kutakuwa na madhara kwa wananchi wanaoishi kwenye miji iliyo pwani.
Afrika inatarajiwa kushuhudia ongezeko la kina cha bahari kuliko wastani wa dunia hivyo kuathiri uchumi wa mataifa kadhaa hasa yaliyo magharibi ambayo asilimia 56 ya Pato la Taifa (GDP) linatoka ufukweni.
Walau miji minane iliyopo ufukweni mwa bahari inapaswa kujipanga kukabiliana na kuongezeka kwa kina. Shirika la Makazi la Umoja wa Mataifa (UN-Habitat) linaitaja miji hiyo kuwa ni Abidjan, Accra, Alexandria, Algiers, Cape Town, Casablanca, Dakar, Dar es Salaam, Djibouti, Durban, Freetown, Lagos, Libreville, Lome, Luanda, Maputo, Mombasa, Port Louis na Tunis. “Kati ya miji hii, Lagos ndiyo mkubwa zaidi ukiwa na zaidi ya watu milioni 10 ukifuatiwa na Dar es Salaam unaokua kwa kasi,” linasema shirika hilo.
Wananchi wengi watashuhudia kupanda kwa gharama za maisha ambazo, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kunatumia walau asilimia 1.4 la GDP za mataifa mengi na zitaongezeka mpaka asilimia tatu mwaka 2030.
Majanga ya asili yataongezeka. Benki ya Dunia inasema, kati ya mwaka 1995 na 2015 kulikuwa na ukame mara 136 barani kote, 77 ukitokea Afrika Mashariki. Niger, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC), Madagascar, Angola na Malawi zilikumbwa na mafuriko.
Matukio haya, kwa namna moja au nyingine, yanatarajiwa kupandisha bei za vyakula Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara ambako Tanzania inapatikana.
Tayari kuna zaidi ya watu milioni 20, benki hiyo inasema wanahitaji chakula cha msaada huko Malawi, Zimbabwe, Msumbiji, Madagascar, Lesotho na Swaziland.
Hakuna mamlaka iliyotangaza uwapo wa janga la njaa nchini lakini hiyo haiondoi haja ya kuweka mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa upana wake. Ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa Desemba mwaka jana inaonyesha mfumuko wa bei uliongezeka hadi asilimia 5.0 kutoka 4.8 zilizokuwapo Novemba na kuelezwa kwamba ulitokana na kuongezeka kwa gharama za vyakula.
Mabadiliko ya tabianchi ni changamoto ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa nchi nyingi za Afrika. Brookings inasema kati ya mataifa 30 ya bara hili yaliyofanyiwa utafiti, theluthi mbili zinashuhudia ongezeko la juu la joto kuliko wastani wa dunia hivyo kuhitaji maandalizi ya mapema.
Mkataba wa Mazingira wa Paris uliosainiwa mwaka juzi na kuanza kutekelezwa Novemba mwaka jana unalenga kupunguza ongezeko la joto walau liwe linapanda chini ya sentigredi mbili kwa mwaka.
Mtaalam Mazingira na Mabadiliko ya Tabianchi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), Abbas Kitogo anasema anasema ipo haja ya kubadili kilimo kinachotegemea mvua ambacho wananchi wengi wanajishughulisha nacho ili kuweza kukabili uhaba unaoweza kujitokeza.
“Mvua hazinyeshi kwa muda kama ilivyozoeleka hata zikinyesha ama huwa chini au zaidi ya wastani ambayo siyo nzuri,” anasema Abbas na kuongea:
“Mbinu bora ni kuwa na kilimo kinachoendana na mabadiliko ya hali ya hewa aidha kwa kupanda vyakula vinavyostahimili ukame au kilimo cha umwagiliaji.”
Licha ya kilimo cha kisasa, Abbas anaishauri jamii kulinda misitu ili kuongeza mvua na kuhifadhi ardhi dhidi ya mmomonyoko ambao madhara yake makubwa.
Licha ya wingi wa madhara ya mabadiliko ya tabia nchi, athari za uhaba wa chakula huwagusa wananchi wengi hasa maskini hivyo uchumi wa mataifa husika. Takwimu zinaonyesha kilimo kinaajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania huku kikifanya izuri kuliingizia taifa fedha za kigeni.
Wataalamu wa mazingira wanatahadharisha kupungua kwa kasi ya maendeleo iwapo hatua za makusudi za kupambana na uharibifu wa mazingira hazitachukuliwa.
Kujiandaa vyema na mabadiliko yanatabiriwa na taasisi za kimataifa, wananchi wanapaswa kujengewa uwezo na kuwezeshwa kufanya kilimo kinachoenda sawa na mabadiliko haya.
Ofisa Mazingira wa Kanda ya Mashariki wa Baraza la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Jafari Chegenge anasema: “Kilimo cha matuta kinapofanywa eneo la mlima husababisha mmonyoko wa ardhi hivyo kupoteza rutuba wakati mwingine kuchangia mafuriko ambayo matokeo yake ni uharibifu wa miundombinu.”
Hata kutumia dawa za kukinga mazao dhidi ya magonjwa na wadudu kusipofanyika kwa utaalamu kuna madhara ya kimazingira kwa shamba lililonyunyuziwa dawa.
“Endapo dawa itatiririka mpaka kwenye vyanzo vya maji inaweza kuua wadudu na wanyama wengine ambao ni muhimu kwa ikolojia,” anasema.
Kupotea kwa uoto wa asili ni suala jingine muhimu kwa mazingira. Mtaalamu wa Mazingira Mfuko wa Hifadhi ya Mazingira (WWF), Edga Kipoki anasema kilimo hasa cha kuhamahama kinasababisha upotevu wa uoto huo kutoka na kuhusisha maeneo makubwa.
“Ukilima kisasa unaweza kupata mavumo mengi kwenye eneo dogo lakini kinyume chake ni kusababisha jangwa litakaloharibu makazi ya viumbehai tofauti,” anasema Edga.
Ushirikiano wa Serikali na wananchi unahitajika ili kuboresha kilimo na kuongeza uzalishaji. Kuheshimu na kufuata sheria za mazingira pamoja na kuzilinda kuanzia kwa wachimbaji wa madini, wavunaji wa misitu, wafugaji na wakulima ni suala lisiloepukika.
Taasisi za umma, mashirika ya ndani na kimataifa pamoja na wanaharakati wa mazingira wanapaswa kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya utunzaji wa mazingira na faida zake ili kuchochea maendeleo.
Hifadhi ya mazingira ni ajenda ya Dunia, na Tanzania hushirikiana na nchi nyingine katika usimamizi wa mazingira.
Mpango wa Kitaifa wa Matumizi ya Ardhi wa mwaka 2011-2031 ni muhimu utekelezwe ili kuhakikisha mipango sahihi ya matumizi ya ardhi na usimamizi madhubuti wa mazingira nchini.
Ili kuleta mabadiliko chanya, uendelevu wa sera hizi ni muhimu kuzingatiwa.
Aidha, maendeleo ya kiuchumi ni lazima yazingatie uhifadhi ya mazingira kuupata uzalisha wenye tija na endelevu.
Kwa muktadha huo, kuna haja ya kuhakikisha mipango na mikakati iliyopo ni jumuishi na inatengewa fedha za kutosha za utekelezaji.