Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Neema inapomjia mstaafu jioni akielekea Kinondoni

Wakati mstaafu wetu ametumia nusu ya miaka yake 66 kupambana ili Mungu bariki awe mmoja wa wale ambao wamefanikiwa kufanya hela ijenge kibanda kwao na hajafanikiwa, anashtuka na kufarijika kwamba kibubu chake kimefanya utaratibu wa yeye hatimaye kuwa ‘kamilionea’ fulani hivi atakapokuwa tayari ameisharudi mavumbini alikotoka. Yeye na wastaafu wenzake wa kima cha chini wanakipongeza mno kibubu chao kwa hili.

Ndiyo, wakati mstaafu wetu akiomba Mungu ili waheshimiwa wafanye kila wawezalo ili ile nyongeza ya pensheni yao ya shilingi elfu hamsini ianze kuwa kwenye mshahara huu wa Desemba, waweze kujipongeza kwa hatimaye kilio chao kusikika pamoja na kuwa siyo kama walivyotegemea, anaomba sana nyongeza hiyo kuwa mfukoni mwezi huu wa ‘Feliz Navidad’ ili wafurahie na familia zao na hayo ya ‘Njaanuari’ watajua wenyewe pa kupita, kama ilivyo miaka yote.

Mstaafu wetu ameisoma mara mbilimbili moja ya kanuni iliyotolewa na Kibubu chao katika kile kinachoelezwa kuwa ni kujali na kuboresha maisha ya mstaafu huyu wa Taifa wa kima cha chini, kama siyo cha chizi. Amejikuta akiamini na kufarijika kuwa kwa pensheni yake hii ya ‘laki moja na elfu hamsini kuanzia mwezi ‘Njaanuari’ Kibubu chake kinamfanya ‘kamilionea’ fulani, japo akiwa tayari yupo mavumbini Kinondoni.

Ni jambo jema sana linalostahili Kibubu kupongezwa. Inaelezwa kwamba mstaafu anayepokea pensheni anapofariki Kibubu kinatoa shilingi laki tano ambazo ni nyingi kuliko pensheni yake ya shilingi laki moja na nusu, kuisaidia familia yake gharama za mazishi yake. Ndiyo, wakati huu wa binadamu kushikana mashati kwanza ili kumzika ndugu yao, hili la Kibubu kutoa laki tano linaleta faraja.

Baada ya mazishi yake, Kibubu kinatoa pensheni yake ya mwezi ya shilingi laki moja na elfu hamsini aliyokuwa anapata mstaafu aliyefariki na kuizidisha mara 36, yaani miaka mitatu, ambazo ni shilingi milioni tano na laki nne na kumkabidhi yule ambaye mstaafu alimuandika kuwa ndio mrithi wake ambaye inategemewa awe mwenza wake au watoto wake. Ndio wanaopaswa kula jasho lake la miaka 40 kwenye ajira ya baba au mama yao.

Mstaafu wetu anaamini kuwa kanuni hii itaondoa kawaida iliyopo kwenye familia zetu za Kiafrika ya wajomba, mashangazi, baba na mama wakubwa na wadogo kuibuka wakati wa misiba ili kupata gawio la mshiko ulioachwa na marehemu ili kurithi mali badala ya watoto. Kwa kanuni hii ya Kibubu inayoweka wazi kwamba shilingi milioni tano na laki nne zinakwenda kwa warithi alioandika mstaafu, japo zitawatia kimuhemuhe.

Mstaafu wetu sasa anafarijika kuwa ataweza kurudi mavumbini akiwa na amani na faraja kwa kuweza kuiachia familia yake japo shilingi milioni tano na laki nne za kumudu maisha yeye akiwa tayari yupo mavumbini Kinondoni au Lubengera! Hatimaye Kibubu chake kinamuwezesha kuwa ‘kamilionea’ ka aina fulani, japo akiwa tayari yupo Kinondoni. Kibubu kinastahili pongezi kwa hili.

Mstaafu wetu sasa anakiomba Kibubu chake kifanye mengine ya muhimu ya ziada ili kasi ya kutoa milioni tano na laki nne kwa wastaafu ziongezeke na isibaki kwenye maandishi tu. Kibubu kizungumze na Siri-kali ili mstaafu aweze kupata matibabu ya bure kutibu maradhi yake ya kiutu uzima yasioambukiza ya kiharusi, shinikizo la juu na la chini la damu na kisukari (mstaafu hajui hata kwa nini gonjwa baya hili tumeliita kisukari wakati halina utamu wowote bali machungu tu).

Kibubu kizungumze na Siri-kali kuwa kama imeshindwa kuwapa wastaafu wachache tu waliobaki wa Taifa hili matibabu ya bure, basi Kibubu kichukue jukumu la kuwalipia bima za afya kwa hela yao ambayo Kibubu kinaitunza na inakiwezesha kujenga maghorofa ya kupanga na kuuza. Kibubu kinaweza kuwalipia wastaafu bima ya afya yao ili kialfu hamsini chao walichoongezwa kiisishie kwenya matibabu yao ya uzeeni. Linawezekana hili, ni utashi tu.

Kuna hili la Kibubu kuanzisha benki ndogo ya kutoa mikopo nafuu kwa wastaafu inayoweza kutoa riba na tozo nafuu kwa wastaafu hao. Hela za wastaafu ziko huko na Kibubu hakishindwi hili. Ni utashi tu kuliko kuwaacha wastaafu ambao hela zao ziko kibubuni wakibamizwa na mikopo ya hizi benki za dotcom ambazo haziangalii makunyanzi bali riba ya mikopo yao yote ni moja tu, mkopaji awe mstaafu au mfanyabiashara.

Kibubu kianzishe benki ndogo ya kukopesha wastaafu. Kama wananchi wa kawaida wanaweza kuanzisha na kuendeleza Vikoba vya kukopa huko mitaani mradi wana ‘kijumbe’ tu, hiki Kibubu cha wastaafu kinashindwa nini kuanzisha benki ya kukopesha wastaafu wakati kinaweza kukopesha hata Siri-kali kujenga madaraja au viongozi wa Kibubu kununulia magari. Ni utashi tu kama ule wa milioni tano na laki nne kwa mstaafu wa Kinondoni!

Na hapa pa benki, hizi benki zetu za dotcom ambazo zimetukopesha zisiitolee macho ile milioni tano ya mstaafu wa Kinondoni inayotolewa na Kibubu. Haiwahusu kabisa. Ni ya mstaafu aliyepo Kinondoni. Mkopo wenu unakuwa ‘imetoka hiyo, ikirudi ni Kinondoni’ msije mkafanya makato yenu hata kama mmemkopesha mstaafu wiki iliyopita na bahati mbaya akawa mkazi wa Kinondoni wiki hii. Kubalini maumivu, milioni tano ni za warithi wa mstaafu.