Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Aisha Ramadhani: Hekaheka za mfanyakazi wa ndani hadi dereva lori

Waswahili wanasema kila binadamu ana ‘kitabu’ chenye kurasa za simulizi ya maisha yake.

Hivyo ndivyo ilivyo kwa Aisha Ramadhani, dereva wa lori la mafuta katika Kampuni ya Lake Oil.

Hadi amefikia kufanya kazi hiyo, amepitia mambo mengi, aliyomsimulia mwandishi wa Jarida la Familia katika mahojiano maalumu yaliyofanyika ndani ya lori wakati wakitoka jijini Dar es Salaam kwenda wilayani Kahama, mkoani Shinyanga.

Mwaka 1999 baada ya Aisha kumaliza darasa la saba, maisha yake yalikuwa magumu na kushindwa kuendelea na shule kutokana na wazazi wake kufariki dunia kwa nyakati tofauti.

Akisimulia, anasema akiwa na miaka 10, baba yake alifariki dunia, hivyo bibi yake akawa mlezi wake mkuu na hakuwa akijua kama mama yake yupo hai au la kwa kuwa alikatishwa mawasiliano naye.

 “Nakumbuka baba alifariki dunia nikiwa na miaka 10 na ndiye nilikuwa nikiishi naye baada ya kutengana na mama yangu tangu nikiwa mdogo, nilijikuta nalelewa na bibi ambaye baadaye alifariki dunia nikiwa darasa la tano,” anasema Aisha.

Anasema bibi yake aliacha wosia akifariki dunia aende kuishi kwa kaka yake wilayani Same, mkoani Kilimanjaro.

“Nilihamishiwa darasa la tano Same, nilipofika darasa la sita nilisoma kwa manyanyaso ya kufanyishwa kazi nyingi, sikuwa nahudumiwa hata viatu vya shule.

“Kwa kifupi kwa kaka niligeuzwa mfanyakazi wa nyumbani, hata muda wa kujisomea nikawa sina, nilipomaliza darasa la saba mwaka 1999 niliondoka kwenda kwa shangazi yangu aliyekuwa akiishi Mlola, Lushoto.

“Kwa bahati mbaya sana nilipofika kwake alinifukuza kwa kumhofia kaka kwa kuwa sikumuaga,” anasema Aisha.


Hekaheka za kazi za ndani

Baada ya kuona mambo sio mazuri, Aisha aliamua kwenda kutafuta kazi za ndani Lushoto Mjini na alikuwa akilipwa Sh5,000 kwa mwezi.

Hata hivyo, majibu ya darasa la saba yalipotoka, alifaulu lakini hakukuwa na mtu wa kumsomesha, hivyo aliendelea kufanya kazi za ndani.

Akiwa kwa mwajiri wake wa kwanza anasema manyanyaso yalizidi, hakukuwa na kizuri alichoona anafanya huku kazi zikiwa nyingi, ikiwamo kwenda kutafuta kuni.

Anasema hakuona tofauti na alivyokuwa kijijini kwao, hivyo aliamua kurudi tena kwa shangazi yake, lakini naye alimkataa tena.

“Niliamua kwenda Arusha kutafuta kazi kwingine na nilipata nikawa nalipwa Sh7000, lakini kulitokea ugomvi wa mabosi zangu (mke na mume), baadaye mwanamke akaamua kuondoka, hivyo baba mwenye nyumba akataka kunigeuza mke, nikaamua niondoke zangu,” anasema Aisha.

Siku hiyo alikwenda kulala stendi ya Arusha na alikaa kama abiria aliyekuwa anasubiri basi.

Akiwa stendi hapo, kuna kaka alikuwa anafanya biashara ya kuuza biskuti, ilipofika jioni ya siku ya pili alimuuliza kulikoni na kumwelezea yote yaliyomkuta.

“Kaka yule baada ya kusikia mkasa wangu, aliniuliza kama nataka tena kazi au kurudi nyumbani, nilimjibu nataka kazi.

“Aliniambia tuongozane, japokuwa moyo ulikuwa ukinidunda na kujiuliza kama naye ataniacha salama au la,” anasema Aisha.

“Kwa kuwa ilikuwa imeshaingia usiku yule kama aliniambia nitalala kwake halafu asubuhi atanipeleka mahali nikaanze kufanya kazi.”

Aisha anasema alikuwa akiwaza mengi, njaa ilikuwa pia ikimuuma kwa kuwa ni siku ya pili hajatia chakula mdomoni.

Walipofika nyumbani, yule kaka alimuacha na kumwambia kuna mahali anakwenda atarudi usiku, huku akimsihi asimfungulie mtu yeyote mlango mpaka atakaporudi.

“Kweli nilifuata maelekezo ya yule kaka, ambaye baada ya kuondoka alirudi saa moja asubuhi na kutaka kujua nilivyolala, kisha akanielekeza vitu vilipo ili nipike chai.”

Baada ya kunywa chai anasema alimpeleka kwa mwajiri mpya, aliyekuwa mwalimu mkuu huku mumewe akiwa ni askari wa Tanapa.

“Yule mwalimu alivyoniona tu, akasema huyu aisee simuachi, akae hapa na mwanangu, akanikabidhi mtoto wake mdogo na kunielezea chakula chake kilipo, akisema yeye atarudi mchana kumnyonyesha,” anasema Aisha.

Hata hivyo, anasema hakuishi zaidi ya miezi saba kwa kuwa katika familia hiyo kulikuwa na ugomvi wa mara kwa mara wa mabosi zake (mume na mke), kutokana na mwajiri wake kupigwa hadi kuzimia.

Baada ya kuona hayo, anasema alimuomba mwajiri wake aende nyumbani kuna shida kidogo imetokea na alivyoruhusiwa ndio ikawa tiketi yake ya kuondoka kwenye nyumba hiyo.

Aisha anasema baada ya kutoka huko alifikiria kurudi kwa shangazi yake, lakini alikumbuka kila akienda huwa anamfukuza na kuamua kwenda Tanga Mjini kusaka kazi kwa mwajiri mwingine.

Mwajiri aliyempata safari hii, alikuwa na duka, hivyo alikuwa akifanya kazi za dukani na nyumbani kwa wakati mmoja, lakini kwa bahati mbaya naye mume wake ikafika mahali akawa anamtaka kimapenzi, hivyo hakumaliza hata mwezi akaondoka zake.

“Nashukuru kipindi hicho kulikuwa na dada tunayefahamiana anaishi Lushoto, nilimwelezea yaliyonikuta akanitafutia kazi Dar es Saalam ya kuuza mgahawa na kunisisitiza niende kwa kuwa ni kama kupanda daraja kutoka kazi za ndani hadi kuuza mgahawa,” anasema Aisha.

Alipofika Dar es Salaam, anasema mwajiri wake huyo mpya alionekana kumpenda na alimwambia atakuwa msimamizi wa wafanyakazi wenzake na kusimamia mauzo yote katika mgahawa huo uliokuwa maeneo ya Kariakoo.

Hata hivyo, anasema katika kufanya kazi kwake huko, alikuwa akishuhudia wafanyakazi walivyokuwa wananyanyaswa na bosi wake, mambo yaliyokuwa hayampendezi.

“Sipendi kuona mtu akinyanyaswa na kuonewa, ilifika mahali wakaniona kama mimi ni mtoto wa bosi wa kuzaliwa kwa namna alivyokuwa ananichukulia,” anasema Aisha.

Kutokana na hayo mara kwa mara anasema aliomba kuacha kazi ikiwa ameshafikisha takribani mwaka mmoja na nusu, lakini bosi wake huyo alimkatalia.

“Hata hivyo, siku moja nilipata sababu ya kuiacha kazi baada ya kutokea wizi wa fedha kwenye droo nililokuwa nimeliacha wazi na kwenda kujisaidia.”

Anasema fedha hizo Sh20,000 ziliibwa na mmoja wa wafanyakazi hao, lakini zilipatikana.

 Aisha anasema aliomba kuacha kazi akaenda kwa shangazi yake ambaye safari hii alipokewa vizuri kwa kuwa alikuwa na pesa.

Alikaa kwa shangazi yake wiki mbili, baada ya hapo alikwenda Kibaha mkoani Pwani, alipopata kazi ya kuuza bar.

Akiwa huko kwa bahati mbaya alipata mimba, iliyogunduliwa na bosi wake wa kike na kumhakikishia kwa kumpima mkojo.

“Enzi hizo nilikuwa sijui mimba inapimwaje, lakini yeye akasoma majibu ya kile kifaa cha kupimia kikasoma mistari miwili, ndio akaniambia kuwa nina mimba tena kubwa tu,” anasema Aisha.

Wakati wakiwa katika taharuki hiyo ya mimba, kesho yake mume wa bosi wake alipata ajali ya gari na kufariki dunia papo hapo.

Baada ya hapo maisha ya yule mama yalibadilika, akasema hawezi kulipa mfanyakazi kwa kuwa ana familia kubwa inayomtegemea, hivyo akampa rafiki yake aliyekuwa na shida ya mfanyakazi.

Kwa kuwa rafiki yule alikuwa anafahamu vema uchapakazi wa Aisha haikuwa shida kukubali kumchukua hata pale alipoambiwa kuwa ni mjamzito.

“Moja ya kitu alichotaka rafiki huyu ni kumuonyesha mwanamume aliyenipa mimba, lakini nilipompeleka alinikana,” anasema Aisha.

Anasema alikaa kwa bosi huyo kama mtoto wa nyumbani hadi alipojifungua, “nilifikiria siku huyu mama akafariki nikatimuliwa na watoto wake kwenye nyumba, nitaishije na mtoto wangu, hivyo nikaona nianze kujitafuta mapema, alinikubalia na kunitaka nimuachie mtoto.”

Katika kutafuta kazi hiyo, alipata tena kazi ya hoteli, akawa akipata hela anaenda kumsalimia mtoto na kurudi kazini.

Anasema akiwa anaendelea na kazi hiyo, alijifungua mtoto wa pili na mwanamume mwingine ambaye walikuwa wakiishi Kiwalani, Dar es Salaam, lakini waliachana baadaye.

Anasema alimpeleka mtoto kwa shangazi yake, baada ya yeye kupata kazi ya kuzunguka kusajili namba za simu na alikuwa amepangisha chumba maeneo ya Tabata, jijini Dar es Salaam.

Katika harakati hizo alikutana na mwanamume mwingine ambaye alimpa ujauzito wa mtoto wake wa mwisho.

“Alikuwa ni mume wa mtu ingawa alinidanganya kuwa hana mke, jambo lililofanya nikatishe mawasiliano,” anasema Aisha.

Kutokana na hali hiyo, aliamua kurudi Same kwa mama yake mkubwa kujiajiri kwa kuwa fundi wa kushona nguo.


Kazi ya kuendesha bodaboda, lori

Anasema katika maisha yake ndoto yake ilikuwa kufanya kazi mbili, udereva wa magari makubwa au kuwa mwanajeshi.

Lakini akaanza kuendesha bodaboda, japokuwa mama yake mkubwa alikuwa hapendi na kufikia hatua ya kumwekea watu wakimuona wamwambie.

Anasema alijua kuendesha bodaboda kwa kujifunza kupitia pikipiki za wenzake.

Anasema mama yake mkubwa alipomkuta alikuwa akimgombeza sana na kumnyang’anya pikipiki, lakini mwisho wa siku alikuja kuikubali na akawa msaada kwake, ikiwamo kumpeleka hospitali, shambani na maeneo mengine.

Mwaka 2016, akiwa anapitia mtandao wa kijamii wa Facebook, aliona mtu ameandika katika mtandao huo kuwa anatafuta utingo amfundishe kazi.

Mmoja akatoa maoni yake chini ya ujumbe huo kuwa yeye anamtafuta wa kike kwa lengo la kuwainua wanawake.

Anasema baadhi yao walimbeza na kusema, “unataka aje umfanye shemeji.”

Yeye (Aisha) akaandika kuwa anatamani kuwa dereva wa lori, baadhi walimwendea ‘inbox’ atume namba ya simu, huku wengine wakamdhihaki kuwa akienda labda ageuke kuwa mke.

“Wengine waliniambia kuwa mwanamke na lori wapi na wapi, labda kama nataka kwenda kwenye kazi hiyo kwa ajili ya kujiuza.

“Ni maneno yaliyokuwa yanakatisha tamaa kweli, japo nilisubiria tu neema ya Mungu ishuke,” anasema Aisha.

Kwa kuwa alikuwa akiwaambia bodaboda wenzake kijiweni ndoto zake ni kuja kuendesha gari, ikatokea kaka mmoja waliyekuwa naye kijiweni aliyehamia kuendesha teksi akampa funguo aendeshe.

Aisha anasema hajui kilitokea nini, bali alichukua funguo akaingia ndani ya gari na kuliendesha.

“Sikujua hata niliwezaje, sijawahi kuendesha gari katika maisha yangu, ukiacha kuzunguka njia za ndani, nilitoka barabara kuu, kwa kuwa boda wenzangu walikuwa hawaniamini, walinifuata nyuma kwa kuhisi ningepata ajali, lakini haikuwa hivyo,” anasema.

Anasema ili kuhakikisha wenzake wanapigania ndoto za Aisha, kuna bodaboda alimwombea kusafiri na kaka aliyekuwa anapeleka mafuta ya gari vijijini kwa kuyabeba kwenye mapipa.

“Kaka huyo alinihoji maswali kama nipo serious kufanya kazi hiyo na kuahidi kunipitia siku inayofuata saa kumi jioni, tulipokuwa njiani akawa ananifundisha namna ya kuendesha.

“Hata hivyo ilipofika kwenda safari ya pili, sikuweza kwa kuwa, awali tulipokuwa njiani tunarudi alionyesha dalili za kunitaka kimapenzi,” anasema Aisha.

Ni kipindi hicho cha mwaka 2016 mwishoni, kaka Gabriel maarufu ‘Gadi’ aliyekuwa akifanya kazi Kampuni ya Petro Afrika alimpigia simu na kumuuliza kama yupo tayari kusafiri naye.

“Huyu Gadi ndio yule aliyesema anatafuta madereva wanawake kwenye Facebook awafundishe kazi na kukosolewa vikali.

“Gadi alitaka nipande gari kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza kusafiri naye, nilipofika Dar es Salaam alinitahadharisha kuwa angependa mtu anayependa kweli kujifunza tena kwa muda mfupi, nikamwambia usiwe na wasiwasi,” anasema.

Pikipiki ile alimwachia mtu akawa anapeleka hesabu kwa dada yake kwa ajili ya kununulia watoto mahitaji.


Asubiri gari kwa saa nane getini

“Kweli nilifika Dar es Salaam, nikakutana na Gadi, akiwa anapakia mafuta depo na nilisubiri saa nane na alipomaliza tulianza safari ya kuelekea jijini Mwanza.

“Tulipofika sehemu akanipa gari na kuanza kunielekeza namna ya kuendesha, ikiwa ni mara ya pili kuendesha tangu nilipoendesha teksi Same.

 “Wakati huo wote nilikuwa nina wasiwasi asije kunitaka kimapenzi kama yule wa kwanza, kwa bahati mbaya huyu kaka (Gadi) alikuja kufariki dunia, ndiye aliyekuwa sababu ya mimi kupata kazi kwenye kampuni mbalimbali hadi kufika hapa Lake Oil,” anasema Aisha.

Kipindi hicho anajifunza ndipo alipoamua kwenda kupata mafuzo ya udereva katika Chuo cha Ufundi Stadi (Veta).

Aisha anasema wakiwa na Gadi walikuwa wakisafiri kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza.

“Pia, Gadi akawa analeta wanafunzi wa kike nikawa ndio nawafundisha, hivyo nikageuka kuwa mwalimu baadaye, lakini pia aliniambia safari hiyo anataka iwe ya mwisho kwangu.

Safari ya tano alienda kama kumsindikiza kwa kuwa alikuwa hayuko sawa kiafya na alikuwa na wanafunzi wanne wakati huo anataka awafundishe.

“Tukiwa njiani tulikutana na lori lenye namba za Rwanda, akaniambia huyu mtu wangu anaitwa Hamza, anaweza kukusaidia ukapata kazi, akataka tumfuate nyuma ili waweze kuonana naye kumweleza hilo.

“Wakati huo Gadi akampigia simu Hamza kumwambia asimame,” anasema Aisha.

“Hamza alionyesha wasiwasi na kuuliza kama kweli ni dereva, Gadi alimwaminisha na kumwambia kama haamini anipe gari niendeshe hadi Kahama.”

Anasema walivyompa gari alionyesha ujuzi wake wa kuendesha na saa hiyo ilikuwa saa nne usiku wakielekea Kahama.

“Niliendesha mwendo wa zaidi ya kilomita 100, Hamza kuanzia hapo alinikubali kweli kuwa ni dereva na akasema ataenda kuongea bosi wake kuhusu jambo langu na ataniletea majibu.”

Wakati anasubiria hilo, Gadi alikuwa akiendelea kumtafutia kazi maeneo mengine, akamwambia ana rafiki yake anakwenda DRC Congo, hivyo ni vema akaenda naye ili akajifunze na safari za nje.

Anasema kaka huyo alimsumbua sana njiani kwa kumtaka kimapenzi na alipomkataa alimnyanyasa na kujikuta wanarudi barabara nzima wamenuniana na waliporejea nchini hakusafiri naye tena.

Hata hivyo, wakati akiwa nyumbani anasubiria jibu la Hamza, dereva wa kampuni ya magari ya Rwanda akampigia kuwa ajiandae waondoke naye safari hii na ahakikishe amebeba hati ya kusafiria.

Gari la huyo kaka lilikuwa likibeba makaa ya mawe kutoka Songea kwenda Rwanda, hivyo bosi wake akataka achukuliwe video akiwa anaendesha.

Hivyo alitangulia Songea kumsubiri, kwa kuwa alimwambia tangu mwanzo kuwa saa ya kwenda Rwanda yeye ndio ataendesha, gari hilo lilikuwa mali ya Kampuni ya Yusa.

Anasema alipofika Rwanda alikaa miezi minne akisubiri apewe gari lake na kipindi chote hicho alikuwa akilipwa posho na bosi wa kampuni hiyo na madereva wenzake wa Tanzania walikuwa wakimsaidia hela ndogondogo.

“Kiukweli madereva wa Tanzania tukiwa nje ya nchi, tunapendana sana, kwa hilo nashukuru,” anasema.

Fedha hizo Aisha anasema nyingine alikuwa akizitumia na nyingine alikuwa akituma Tanzania kwa ajili ya watoto.

Huko alikuwa anakaa kwa dada aliyefahamiana na Hamza nyumbani kwao na baada ya kufika miezi hiyo minne, bosi wa kampuni alimpigia simu ya kwenda kumkabidhi gari lake lililokuwa likienda kubeba saruji katika Kiwanda cha Wazo jijini Dar es Saalam na kupeleka Kigali, Rwanda.

Hivyo kuanzia hapo ndio ikawa safari yake ya kwanza kusafiri mwenyewe na lori kwenda kuchukua mzigo.

Anasema aliungwa mkono na madereva wenzake, ikiwamo kuongozana nao na hata Hamza aliposikia amepata gari, alifurahi na kumshukuru kwa uvumilivu wake, huku akimpa nasaha kuhusu mambo ya barabarani.


Alivyopokewa kazini

Anasema anashukuru alipokewa vizuri kazini na kuna wakati alikuwa akipewa nafasi ya upendeleo wa kutoka kwenye foleni.

Pia, madereva wenzake walikuwa wakitaka kujua kila alipofika ili kufahamu kama yupo salama.

Katika ufanyaji kazi huo, Aisha anasema ndani ya mwezi mmoja alijikuta akisafiri safari tano.

Alifanya kazi katika kampuni hiyo ya Rwanda takribani miaka miwili (yaani 2017 hadi 2019).

Kwa ufanyaji kazi huo, kampuni nyingine zikaanza kumhitaji, ikiwamo TransAfrika kulikokuwa na madereva wanawake wawili, mmoja wa Tanzania na mmoja wa Rwanda.

Walikuwa wakibeba makaa ya mawe kutoka Songea kwenda Rwanda na wakati mwingine kwenda Nairobi.

Julai 2019, aliachana na Kampuni ya Yusa akajaribu kuomba kazi Kampuni ya Trans Afrika na kupitishwa kupitia fundi aliyekwenda kutengeneza gari lake lililoharibika katika kampuni aliyokuwa akifanya nayo kazi awali.

 Mwishoni mwa mwaka 2021 akaacha kazi TransAfrika na kwenda Kampuni ya Twalibu Logistic na kumpa ruti za kwenda Congo, lakini baadaye aliomba kusafiri ndani ya nchi.

“Kwa kwenda Congo ruti hizo mbili, nilitumia miezi mitano, na kule kwenye ile nchi hakuna vyakula ni gharama sana kuishi, hapo bado familia inanisubiri, nikaona sitaweza,” anasema Aisha.

Anasema alipewa kazi ya kusafiri Mwanza kwenda Dar es Salaam, wakati mwingine Songea kubeba makaa ya mawe kupeleka kiwanda cha saruji Dangote.

Baadaye aliacha kazi Twalib Oktoba mwaka jana na Novemba mwaka huo akapata kazi Lake Oil.


Changamoto

Anasema moja ya changamoto inayowakumba wanawake madereva kupata kazi ni kutoaminiwa na baadhi ya waajiri.

Pia, anasema jamii mtaani inaona mwanamke anayefanya kazi hiyo ni yule aliyeshindikana, huku baadhi ya madereva wanaume wakiwavunja moyo, japo anakiri siku hizi wanaenda wakibadilika na ndio maana kuna madereva wanawake wengi sasa wa malori.

Jingine anasema wanawake wenyewe wanaopata nafasi hizo za madereva hufanya mambo ndivyo sivyo, hivyo kuwachafulia wale walio na kiu ya kweli ya kazi hizo.

Hana mpango wa utingo

Tofauti na madereva wengine, Aisha anasema huwa hatembei na utingo barabarani kwa kuwa wana kero zao.

Anasema ikitokea gari limeharibika ana uwezo wa kushuka na kutengeneza hata kama akiwa porini, kwa kuwa anashukuru alipata mafuzo Chuo cha Ufundi Stadi (Veta), hivyo anajua a, b, c za ufundi katika gari.


Madereva wenzake wanamzungumziaje

Dereva Francis Benedicto, anasema Aisha ni mwanamke mpambanaji kwa kuwa kuna mambo anayoyafanya hata madereva wanaume hawamuwezi.

“Kiutendaji Aisha ni mwanamke anayefanya vizuri, ni mtu anayeipenda, kuijali na kuifurahia kazi yake ndio maana anaifanya vizuri,” anasema Benedicto.

Francis anamuombea Mungu Aisha kuendelea kuwa hivyo na kueleza kuwa ni zaidi ya mama kwa namna anavyomuona.

“Hata madereva watano wa kike waliokuwepo kwenye Kampuni ya Lake Oil, hakuna unayeweza kumfananisha na Aisha kwa uchapa kazi wake,” anasema Benedicto.

Leila Hassan, mmoja wa madereva wa kike katika lori kwenye Kampuni ya TransAfrika, anasema Aisha ni bonge la mama, na huwa hataki utani linapokuja suala la kazi.

Usikose kufuatilia simulizi ya Aisha na saa 48 barabarani kutoka Dar es Salaam hadi Shinyanga Jumapili ijayo.