Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wenye miaka 40 hatarini matumizi ya uzazi wa mpango

Muktasari:

  • Makundi mengine yaliyotajwa ni pamoja na wanawake wenye michirizi nyuma ya mapaja, kifafa, wanaoumwa kichwa na kipanda uso, huku hatari zinazotajwa ni pamoja na kupata kiharusi, kuganda kwa damu na magonjwa ya moyo.

Dar es Salaam. Baadhi ya wanawake wamekuwa wakitumia njia za uzazi wa mpango bila kuzingatia hali zao, hivyo kujiweka kwenye hatari ya kupata magonjwa sugu.

Hata hivyo madaktari wanashauri kabla ya kutumia njia yoyote ya uzazi wa mpango, ni vema mwanamke akakutaka na mtaalamu wa magonjwa ya kinamama apate ushauri na vipimo kabla ya kufanya uamuzi.

Wanawake wenye umri wa zaidi ya miaka 40, wametajwa kuwa katika hatari pindi watumiapo njia za uzazi wa mpango kwa kuwa huchangia kuganda kwa damu kwenye mishipa na kiharusi, hali inayosababishwa na mabadiliko ya homoni za estrojeni na progesterone mwilini.

Neema Sanga (46), ni miongoni mwa wanawake walioweka vitanzi, lakini walivitoa kutokana na changamoto baada ya kufika umri wa miaka 41.

“Niliweka nikiwa na miaka 38 wakati huo nilikuwa nimejifungua mwanangu wa mwisho, nilikaa na kitanzi mpaka nilipofikisha umri wa miaka 41 sababu nilianza kupata changamoto ya maambukizi, baadaye nikapata shida ya kuganda kwa damu,” amesema.

Sambamba na hao, wale wenye michirizi nyuma ya mapaja au miguu, pia hawashauriwi kutumia njia zozote za uzazi wa mpango.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi, wataalamu wa magonjwa ya kinamama na uzazi wamesema kuna hatari za moja kwa moja kwa makundi hayo kutumia dawa za homoni na badala yake hushauriwa kutumia kondomu na njia za asili.

Daktari bingwa wa magonjwa ya kinamama na uzazi kutoka Hospitali ya Salamaani, Abdul Mkeyenge amesema mwanamke aliyefikisha umri wa miaka 40, tayari homoni zake huwa zimeanza kushuka na hata mzunguko wake wa damu huwa mdogo.

“Tunashauri mwanamke aliyetimiza umri wa miaka 40 akabaki kutumia njia nyingine za uzazi wa mpango kama kondomu na zile za asili.

“Akitumia vidonge, vitanzi na hata vijiti na zingine za homoni anaweza kupata athari ya damu kuganda, kupata changamoto ya homoni kwa kusikia baridi sana au joto kali hasa nyakati za usiku, mwili unaongezeka na homa kali,” amesema.

Daktari bingwa wa magonjwa ya uzazi, Dk Isaya Mhando amesema wanawake wenye miaka 40 na kuendelea hawatakiwi kabisa kutumia kwa sababu ya kutengeneza mgando wa damu kwenye mishipa na kiharusi.

Kwa mujibu wa Dk Mhando, homoni zilizopo kwenye njia hizo, huongeza hatari  ya kutengeneza mgando wa damu kwenye mishipa ya damu kwa kuwa mwanamke akifika zaidi ya miaka 40 ile mishipa yake huanza kusinyaa, homoni ya progesterone inavyopungua.

“Wengi tunawatibu wameshapata haya madhara, unaweza kumtibu kwa etrogeni lakini zinakwenda kwa muda mfupi sana. Kila mwanamke anayekuja anakuwa ameathirika na hilo, na ndiyo maana hata hawa wengine kuna kiduara huwa tunakizungusha kinakupa mwelekeo utumie njia gani,” amesema Dk Mhando.

Pamoja na hao, anawataja wanawake wenye kifafa na wanaoumwa sana kichwa au kipanda uso, kuwa hao wote hawatakiwi kutumia njia za homoni, ambao mara nyingi hushauriwa kutumia lupu isiyo na homoni au kalenda.

“Ukimfundisha anaweza kujua namna atakavyotakiwa kuishi, akiujua mzunguko wake wa hedhi siku za hatari akatumia kondom au njia ya kutoa nje manii kwa mwanaume, ambayo hata hivyo ina hatari kama mume ni mlevi na changamoto nyingine anaweza kutoa wakati tayari kuna mbegu zingine zilishaachiliwa ndani,” amesema.

Kwa mujibu wa Dk Mhando kuna makundi manne ya kinamama ambayo hupatikana baada ya vipimo.

“Kundi la kwanza mama anakuja anataka kutumia vipandikizi yupo kwenye ndoa yake, nyuma ya mapaja anakuwa na michirizi, huyu hafai kutumia njia yoyote anatakiwa atumie kondom.

“Michirizi inaashiria ana homoni ya progesterone nyingi kwa hiyo ukimuongezea homoni nyingine anakuwa mbioni kupata magonjwa ya moyo, na itasababisha mishipa ya damu itanuke zaidi damu inaweza ikawa inabaki huko zaidi kuliko kurudi kwenye moyo,” amesema.

Dk Mhando amesema makundi mengine ni wanawake ambao wanakubali homoni zote mbili zilizo katika njia za uzazi wa mpango, na kundi jingine linakubali homoni mojawapo pekee.

“Mama anachagua baada ya kumpima kwamba mwili wake unaendana na hiyo njia? Huyu amechagua kitanzi lakini kama ana wapenzi wenzi, tunamshauri abadili njia kwa sababu ile kamba inayobaki nje huwa na tabia ya kupitisha maambukizi mwishowe anapata PID,” amesema.