Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanawake wenye ndevu wanavutia machoni, katika hisia

Ndevu

Muktasari:

Zipo sababu nyingi za wanawake kuota ndevu. Hali hiyo bado haiwazuii kutekeleza majukumu yao.

Katika hali ya kawaida msichana au mwanamke hatazamiwi kuwa na ndevu kwenye kidevu, juu ya mdomo, kifuani, tumboni na mgongoni.

Kwa kawaida mwanamke huwa na vinyweleo vilaini, ambavyo jamii imezoea kuviita ‘malaika’.

Wanaume kwa kawaida huwa na ndevu ambazo huzitofautisha na vinyweleo kwa rangi nyeusi iliyokolea na huwa vigumu tofauti na vya wanawake ambavyo huwa vilaini.

Mwanamke anapokuwa na nywele nyingi sehemu hizo humaanisha kuwapo kwa hitilafu za kijenetiki au dosari za ulinganifu wa vichocheo vya jinsi mwilini mwake.

Wasichana wengine kutokana na urithi wa vinasaba, wanaweza kuwa na nywele nyingi sehemu mbalimbali za mwili. Hali hii kitabibu hujulikana kwa jina la ‘hypertrichosis’.

Mitazamo ya kijamii

Wanawake wanapoota ndevu nyingi hukabiliwa na changamoto za kisaikolojia kutokana na kuwa na mwonekano kama wa wanaume.

Mitazamo na mila nyingi za kijamii katika Bara la Afrika, bado zinakumbatia unyanyapaa wa wazi au wa kificho kwa wasichana wanaoota ndevu nyingi.

Msichana mwenye ndevu nyingi, anavuta hisia na macho ya wanaume na wanawake wenzake pia kiasi kwamba, anatazamwa kwa namna ambayo wakati mwingine inamnyima raha.

Wapo wanaume wanaoangalia wanawake wa namna hiyo kwa mtazamo hasi na wengine chanya. Ziko imani potofu miongoni mwa jamii kuwa wanawake wa namna hiyo wanaashiria kuwa na fedha, wengine wakiamini huwa wanawapiga waume zao na hata wengine kuamini kuwa hawana hisia za kike.

Ukweli ni kwamba wanawake wengi wenye ndevu huweza kuwa na hisia za kike kama wengine na hata kupata watoto licha ya mwonekano wa nje.

Wakati mwingine wanaume hawapendi kuoa wasichana au wanawake wenye ndevu nyingi kutokana na mwonekano unaowafanya wasichana hao kuwa kama wanaume.

Sababu za ndevu

Moja ya sababu za wanawake wengi kuota ndevu ni dosari za ulinganifu katika mfumo wa vichocheo vya mwili hasa vile vinavyoamua kutokea kwa mabadiliko ya ukuzi wa kijinsia.

Dosari za ulinganifu wa vichocheo vya kijinsia kwa wasichana zinaweza kusababishwa na mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuzalishwa kwa wingi kwa vichocheo vya ujinsia kutoka katika mifuko ya mayai na uvimbe katika mifuko ya mayai.

Uvimbe wa tezi ya Adrenali iliyo juu ya figo pia unaweza kusababisha tatizo hili kutokana na kuzalisha kwa wingi kichocheo cha Dehydroepiandrosterone (DHEA).

Wakati mwingine kunakuwepo na hali ya ulinganifu wa vichocheo vya ujinsia mwilini kama kawaida, lakini tatizo likawa ni mwitikio wa hali ya juu wa nywele kwa kiasi kidogo na cha kawaida cha kichocheo cha kiume kilichoko mwilini mwa msichana.

Katika hali hii, msichana pia anaweza kuwa na nywele nyingi sehemu mbalimbali za mwili wake.

Katika utafiti uliowahusisha wanawake 102 wanaokabiliwa na tatizo la kushindwa kutunga mimba waliohudhuria katika kliniki ya magonjwa ya wanawake, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) kati ya Septemba 2006 na Februari 2007, ilibainika miongoni mwao, asilimia 32, walikuwa na uvimbe katika mifuko ya mayai.

Asilimia 56.3 ya wanawake wote wenye uvimbe huo, walikuwa na tatizo la kuwa na nywele nyingi mwilini ikiwa ni pamoja na kuota ndevu.

Hii ni kwa mujibu wa utafiti wa Dk Pembe AB na Abeid MS wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba cha Muhimbili (Muhas), uliochapishwa katika Jarida la Kisayansi la Tanzania, Journal of Health Research la Oktoba 2009.

Utafiti ulibaini kuwa mambo mengine yanayochangia kutokea kwa tatizo hili ni matumizi ya dawa za hospitalini na vipodozi vyenye viambata vya dawa kama testosterone na steroid.

Ikaonekana kuwa hayo ni matokeo ya matumizi ya muda mrefu ya kutumia vipodozi hivyo kwa muda mrefu bila kupata ushauri wa afya.

Matumizi makubwa na holela ya baadhi ya dawa zenye kemikali kama vile Danazol, Cyclosporin na nyingine pia yanahusika kusababisha tatizo hili.

Shirika la Habari la China (Xinhua), limewahi kuripoti taarifa ya mwanadada mwenye umri wa miaka 16 aliyejulikana kwa jina moja la Nana kuwa aliota ndevu nyingi baada ya kupewa matibabu ya hospitalini kwa kupandikizwa mafuta yanayopatikana ndani ya mfupa (uloto).

Mwanadada huyo alipewa matibabu hayo baada ya kupata tatizo la kupungukiwa damu mara kwa mara lijulikanalo kama Aplasticanaemia.

Wataalamu wa sayansi ya afya ya jamii pia wanauhusisha unene wa kupindukia kwa wasichana na kutokea kwa tatizo la kuota ndevu.

Unene wa kupindukia unaweza kusababisha ongezeko kubwa la kichocheo cha kiume kijulikanacho kwa jina la Androgen ndani ya mwili.

Hali hiyo hutokana na nyama zenye mafuta mengi kugeuza kichocheo cha kike cha estrogen kuwa kichocheo cha kiume cha androgen.

Androgen inapokuwa nyingi mwilini husababisha msichana kuwa na tabia za kiume ikiwa ni pamoja na kuota ndevu na kuwa na sauti nzito.

Daktari Adam Nyalandu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), amewahi kunukuliwa kwenye gazeti moja la hapa nchini akisema kuwa tatizo la wanawake kuota ndevu linaweza kutokana na sababu nyingi ikiwamo matumizi ya vyakula vya kusindika vinavyotengenezwa kwa kutumia kemikali nyingi.

“Mfano ulikuwa huli nyama za kopo au vyakula vya kusindika ambavyo kemikali inatumika kuvisindika sasa unakula, vinaweza kusababisha tatizo hilo kwa kiwango kikubwa,” anasema Dk Nyalandu.

Wanawake wenye ndevu mara nyingi hukabiliwa na dalili kadhaa zinazowafanya watafute msaada wa kitabibu mara kwa mara. Baadhi ya dalili hizo ni kama vile kuota chunusi nyingi, kutokupata hedhi kama kawaida. Wakati mwingine msichana hupata damu pungufu wakati wa hedhi au kutoiona kabisa. Wataalamu wanasema wakati mwingine wanawake wa namna hiyo hupata hedhi isiyo na mpangilio.

Wanawake wenye tatizo hili pia wanakabiliwa na uwezekano wa kupata magonjwa sugu ya muda mrefu.

“Kama utafanya mahesabu, utagundua kwamba angalau nusu ya wanawake wenye tatizo la kuwa na nywele nyingi mwilini, wanakabiliwa na hatari kubwa ya kupata magonjwa ya kisukari na moyo,” anasema.

Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa vichocheo vinavyohusiana na mfumo wa uzazi mwilini na Rais wa Chuo Kikuu cha Sayansi za Afya cha Georgia, Dk Ricardo Azziz akielezea umuhimu wa utafiti alioufanya kwa kushirikiana na Vituo vya Afya vya Heather Cook na Kathleen Brennan, anasema matatizo mengine yanayosababisha ndevu kuota kwa wingi pia yanaweza kumfanya mwanamke kuwa mgumba.

Hali hiyo pia huweza kuandamana na kusinyaa kwa matiti na mfuko wa mji wa mimba. Athari nyingine ni pamoja na kututumuka isivyo kawaida kwa maumbile ya via vya uzazi na kuwa na sauti nzito na wakati mwingine kisanduku cha sauti hunenepa kama cha wanaume.

Mtawanyiko wa nywele mwilini huwa kama wa kiume. Pamoja na ndevu msichana huota nywele kifuani, tumboni, mapajani, mgongoni, miguuni na mikononi kwa wingi.

Epuka atahari kisaikolojia

Ili kuepuka athari za kisaikolojia zinazoweza kutokana na hali hii, msichana anashauriwa kuelewa kuwa kuota ndevu siyo dhambi na wala kosa.

Anapaswa kufahamu kwamba ndevu hazipaswi kuwa chanzo cha msongo wa mawazo kwani hali hiyo inaweza kuathiri afya ya mwili na akili.

Pia, ndevu zisiachwe zikawa ndefu kama za wanaume kwani zinavuta hisia za watu kumwangalia mwanamke au msichana kiasi kwamba hali hiyo inaweza kusababisha matatizo ya kisaikolojia.

Ndevu zikatwe na kuwa fupi kadri inavyowezekana wakati wote. Mkasi au cream ya kuondoa nywele inaweza kutumika kwa lengo hili. Ile dhana ya wanawake wengi kwamba ndevu zikinyolewa zinaongezeka maradufu haina ukweli wowote wa kisayansi.

Ndevu zising’olewe kwa vidole. Hii inaweza kusababisha uambukizo wa bakteria katika ngozi kwa urahisi na kuleta matatizo makubwa ya kiafya.

Njia nyingine iliyo bora kwa wasichana kujiepusha na tatizo la kuota ndevu ni kuachana na matumizi ya vipodozi vyenye viambata vya steroidi vinavyoleta weupe bandia wa ngozi.

Kufanya mazoezi ya mwili na kudhibiti unene wa mwili kwa njia ya lishe bora pia ni mkakati mwingine unaosaidia kupambana na tatizo hili.

Endapo nywele zimetapakaa kwa wingi miguuni na mikononi na kuleta mwonekano wa kiume, ni bora kuvaa nguo ndefu zinazofunika mwili vizuri ili kuepuka msongo wa kisaikolojia ambao unaweza kutokea kutokana na mtazamo hasi wa kijamii.