Utumiaji tumbaku unavyopunguza umri wa kuishi

Mbeya. Licha ya elimu kuhusu madhara ya matumizi ya tumbaku kuendelea kutolewa, bado watu wanaendelea kuitumia, hivyo kuhatarisha afya zao.
Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa matumizi yoyote ya tumbaku iwe kuvuta kama msokoto/kiko, kunusa na kutafuna/ugoro, bidhaa za tumbaku za kisasa kama sigara na shisha zite zina madhara sawa kwa kuwa mtumiaji huingiza sumu mwilini.
Moshi wa sigara huwadhuru pia wengine wasiovuta kwa sababu una kemikali zote anazopata mvutaji na hakuna kiwango salama kisichosababisha madhara.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), wastani wa watu milioni sita kila mwaka hupoteza maisha kutokana na uvutaji tumbaku, huku watu 900,000 hupoteza maisha kutokana na kuvuta hewa ya moshi katika mikusanyiko ya watu.
Mkurugenzi wa udhibiti wa dawa za binadamu na mifugo kutoka Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Dk Yonah Mwalwisi anasema takwimu hizo zilifanyiwa utafiti na WHO mwaka 2019.
Dk Mwalwisi anasema matumizi ya tumbaku hufupisha muda wa kuishi kwa binadamu kwa wastani wa miaka 20 hadi 25, huku wavutaji 7 mpaka 10 wanaanza kutumia wakiwa na umri mdogo.
Inaelezwa nusu ya watumiaji wa tumbaku kwa muda mrefu hufa kutokana na madhara yake, nusu ya vifo hivyo vikiwa chini ya miaka 70.
Anasema takwimu zinaonyesha matumizi ya tumbaku kwa nchi maskini yako juu tofauti na mataifa mengine, huku ikionyesha kati ya asilimia 100, asilimia 80 ya wavutaji ni katika nchi zenye kipato cha chini na kati.
“Watumiaji wa tumbaku bilioni 1.3 wanaishi katika nchi zenye kipato cha chini na kati, huku katika nchi zilizoendelea wanatumia dola trilioni 1.4 kugharimia magonjwa yanayotokana na matumizi ya tumbaku,” anasema.

Madhara ya matumizi ya tumbaku
Dk Mwalwisi anasema kuna athari kubwa za kiafya kwa mtumiaji anayetumia mifumo ya bomba au shisha kwa saa moja, kwani anavuta wastani wa sumu ambayo imezalishwa kwenye sigara 100.
“Bidhaa ya tumbaku ina kemikali zaidi ya 4,000, huku hatarishi zikiwa 40 ambazo zimethibitishwa kusababisha athari ya magonjwa ya saratani kwa wanawake na wanaume wanaotumia kuvuta kama kionjo.
Kwa upande wa wanawake, anasema madhara yanayotokana na kuvuta tumbaku ni kupata saratani ya mfuko wa uzazi inayosababisha kushindwa kupata ujauzito.
Athari nyingine kwa wanawake ni kuharibika kwa mimba pamoja na mtoto anayezaliwa kupoteza maisha au kulizaliwa na uzito usio wa kawaida pamoja na kupata utasa.
“Kwa wanaume hupata changamoto ya upungufu wa nguvu za kiume kutokana na mzunguko wa damu na kuharibika kwa mbegu za kiume,” anasema.
Hatua zilizochukuliwa
Anasema hatua zinazochukuliwa ni kutoa elimu kwa jamii, ikiwa ni pamoja na kuelezea athari za matumizi ya tumbaku, hususan kwa watoto wenye umri chini ya miaka 18.
“Pia kuna jitihada mbalimbali zinafanywa kuhakikisha jamii inaelimishwa juu ya hatari ya matumizi ya bidhaa za tumbaku ili kupunguza madhara kwa kiwango kinachowezekana,” anasema. Dk Mwalwisi anasema mikakati mingine ni kuweka mazingira yatakayochangia kuondoa uvutaji na utumiaji wa tumbaku pamoja na kuunda kamati za kitaifa kusimamia udhibiti wa bidhaa hizo katika nyanja zote za maisha.
Anasema hatua nyingine ni kuandaa mfumo na taratibu za kupokea maombi ya usajili wa bidhaa za tumbaku kupitia teknolojia za kisasa za mifumo ya Tehama (online) na kutoa elimu kwa umma kuhusiana na sheria ya udhibiti na madhara yake
Lengo la udhibiti
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), Adam Fimbo anasema kama mamlaka wanakusanya taarifa za bidhaa ya tumbaku zilizopo sokoni na usajili wa maeneo ya kibiashara, hususan katika maeneo ya mipakani.
“Changamoto za matumizi ya tumbaku ni kubwa kwenye jamii yetu, ni vema wadau wakashirikiana na TMDA kutoa elimu kwa jamii, ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari kuandika habari za kuelimisha jamii,” anasema.
Mganga Mkuu Mkoa wa Mbeya, Dk Salum Manyata anasema athari za matumizi ya tumbaku ni kubwa, hivyo wameweka mikakati kwa kushirikiana na TMDA kutoa elimu na kuyafikia makundi mengi zaidi.
“Kuna mikakati mbalimbali tunaifanya ili kuhakikisha jamii inaachana na matumizi ya tumbaku pamoja na kujikinga kuvuta hewa ya moshi ambayo ina madhara pia,” anasema.
Kauli ya Serikali
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera anasema kuna kila sababu ushirikino uwe mkubwa kwenye jamii, ili kunusuru kundi kubwa la wazee, vijana, watoto ambalo linaonekana kuathirika na matumizi ya tumbaku kama takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO zinavyoonyesha.