Utafiti wabaini asilimia 75 ya vyakula vilivyosindikwa havina ubora

Dar es Salaam. Asilimia 75 katika vyakula 400 vya kusindikwa vilivyofanyiwa utafiti vinavyouzwa hapa nchini vimebainika kutokuwa na ubora wa kiafya katika matumizi yake.
Hayo yamesemwa Juni 25, 2025 katika utoaji wa matokeo ya tathimini ya utafiti yaliyofanywa na taasisi inajishughulisha na kuangalia ubora wa uchakataji wa bidhaa za kusindika ya ATNI.
Mtafiti Mwandamizi, Kaitlyn Elavaza amesema katika utafiti huo wamefanya kwa kampuni 21 na kuzihusisha bidhaa 483 ambapo matokeo yameonyesha kuwa ni asilimia 25 kwa bidhaa zote hizo ndio zina ubora wa afya.
"Moja ya vitu tulivyokuwa tunaangalia katika utafiti huu ni pamoja na maandishi nyuma ya bidhaa kwamba kuna viungo vinapatikana ndani ya bidhaa husika lakini baada ya kutafiti unagundua ukweli ni kwamba havipo na pia kwa vile ambavyo wanasema vipo kwa kiwango fulani utakuta vinazidi.
"Katika hilo mfano kuna vitu ambavyo sio vizuri kwa afya ukivitumia kama mafuta, chumvi, sukari ambavyo vinachangia magonjwa yasiyoambukiza, unaweza kuambiwa vipo kwa asilimia ndogo lakini ukichunguza kiundani vimepitiliza hali inayohatarisha afya ya mlaji.
Katika ushauri wao, Meneja Mradi wa utafiti, Bo-jane Woods amesema kuna haja kampuni zinazotengeneza bidhaa husika kuangalia namna ya kuondoa vitu ambavyo siyo bora kwa afya na kuangalia mbadala wake.
Pia, Bo-jane amesema kama taifa kuna haja ya kuboresha mifumo ya sera na kisheria ili kuweza kuhakikisha vyakula vyote vinavozalishwa nchini na vinavyotoka nje ya nchi vinakuwa na ubora wa afya na pia vinalinda uhai pamoja na usalama wa chakula.
Mkurugenzi wa Taasisi na Lishe, Germana Leyna amesema utafiti huo umekuja wakati mwafaka ukizingatia kuanzia mwaka 2021 Serikali inatekeleza mpango wa kisekta wa lishe na moja ya watu iliyopanga kuwashirikisha ni sekta binafsi.
Amesema hii ni kutokana na kuona sekta binafsi ipo tayari katika kujadili namna bora ya kuweza kuzalisha bidhaa zao ili waweze kusaidia hali ya lishe nchini lakini na wao kuweza kupata kipato.
"Kwa hiyo kupitia tafiti kama hizi tumepata eneo ambalo tutashirikiana na sekta binafsi ili kuhakikisha kwamba huko kuzuri wanakofanya huko duniani inaweza kufanyika na hapa nchini pia," amesema Germana.
Kuhusu bidhaa zisizokidhi viwango vya afya, Leyna amesema inachangiwa na mambo kadhaa ikiwemo maendeleo ya kidunia ambapo nchi zilizoendelea wameanza kuwa na viwanda muda mrefu, wameshatengeneza sera zao na miongozo mbalimbali na wameshajizatiti namna ya kusimamia uzalishaji wa viwanda vyao.
Kama haitoshi athari zinazotokana na lishe duni wao wameshaanza kuzipitia kwa muda mrefu hususani unene uliozidi au kiriba tumbo.
"Kwa hiyo kutokana na kuwa wenzetu hawa wameendelea na kutokana na mambo ya kibiashara inawezekana wengine wakatafuta penye unafuu wa kuweza kuuza bidhaa zao hizo.
"Kingine kinachochangiwa ni mazingira watu waliolelewa kwani unapolelea kwenye mazingira ya chakula cha ladha fulani basi kuibadilisha hiyo haiba ni ngumu lakini kama taasisi tutaendelea kuwaelimisha watanzania hadi waelewe madhara ya utumiaji wa vyakula hivyo kwa afya zao na kusisitiza ukaji wa vyakula vya asili,"amesema.
Mkurugenzi huyo
Aidha amesema kama nchi kuna kujiuliza hiyo ladha ya sukari nyingi tufanyaje na kuanza mjadala namna gani inaweza kupunguzwa au kukatafutwa vyanzo mbadala vya hiyo ladha ya sukari.
Mbunge Viti Maalumu kupitia CCM, Neema Lugangira amesema akiwa mdau wa lishe wa miaka mingi na amekuwa akisema ni lazma Serikali ihakikishe jukumu na mamlaka ya kusimamia chakula linarudishwa kwa Wizara ya Afya.
"Katika utafiti huo umeonyesha hata kwa vyakula vya watoto vya kusindikwa kuwa asilimia tisa ndio inaenda na viwango vilivyowekwa kwa vyakula vya watoto na Shirika la Watoto la Duniani (Unicef) pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO).
"Kwa hiyo hii inaendelea kuweka msukumo kwa nini kuna haja ya suala la usalama wa chakula litoke Wizara ya Viwanda na Biashara na kuwa chini ya Wizara ya Afya kwa sababu kimsingi wizara hiyo ndio yenye dhamana ya kuhakikisha kwamba inalinda usalama na afya za Watanzania," amesema Neema.
Ameongeza kuwa kubwa zaidi ni kuwepo kwa ongezeko la magonjwa yasiyiambukiza ikiwemo shinikizo la damu, sukari na magonjwa mbalimbali ya saratani ambapo vyakula hivyo hivyo vinachangia.
Kama haitoshi amesema pia asilimia 70 ya gharama za kuendesha Mfuko wa Taifa Bima ya Afya (NHIF) ni kwa sababu ya magonjwa hayo yasiyoambukizwa ambapo anaona namna gani vinashahabiana na wizara hiyo ya afya.