Usiruhusu simu kudhuru maisha yako

Muktasari:
- Hata hivyo, matumizi yake yasiyo sahihi yanatajwa na wataalamu wa afya kuwa na hatari kubwa kwa afya ya binadamu, ikiwa ni pamoja na kuhusishwa na magonjwa yasiyoambukiza kama vile saratani ya ubongo, ngozi, kupungua kwa uwezo wa uzalishaji wa mbegu za kiume, na wanawake kupoteza hamu ya tendo la ndoa.
Simu za mkononi zimekuwa sehemu muhimu ya maisha ya kila siku, zikitumika kama nyenzo rahisi ya mawasiliano pamoja na kuongeza ufanisi katika shughuli mbalimbali za kijamii na kiuchumi
Hata hivyo, matumizi yake yasiyo sahihi yanatajwa na wataalamu wa afya kuwa na hatari kubwa kwa afya ya binadamu, ikiwa ni pamoja na kuhusishwa na magonjwa yasiyoambukiza kama vile saratani ya ubongo, ngozi, kupungua kwa uwezo wa uzalishaji wa mbegu za kiume, na wanawake kupoteza hamu ya tendo la ndoa.
Ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya mwaka 2024 inaonyesha ongezeko la matumizi ya simu ambapo laini ziliongezeka kutoka milioni 76.66 hadi milioni 86.84 kati ya mwezi Juni hadi Septemba mwaka huo. Ongezeko hili linadhihirisha utegemezi mkubwa wa wananchi kwa mawasiliano ya simu, lakini pia linachochea mjadala kuhusu usalama wa kiafya wa matumizi hayo.
Wataalamu wa afya, wakiwemo madaktari bingwa wa ubongo na mishipa ya fahamu, wameonya dhidi ya tabia ya kulala karibu na simu au kuiweka chini ya mto wakati wa kulala, wakieleza kuwa kunaweza kusababisha aina fulani ya saratani kutokana na mionzi inayotolewa na vifaa hivyo.
Aidha, Shirika la Afya Duniani (WHO) katika utafiti wake wa mwaka 2011 lilieleza kuwa kuna hatari ya asilimia 40 zaidi ya kupata saratani ya ubongo (glioma) kwa mtu anayetumia simu kwa zaidi ya dakika 30 kila siku kwa muda wa miaka kumi.
Baadhi ya wanawake wamekuwa na tabia ya kubeba simu ndani ya sidiria, jambo ambalo linaelezwa kuwa hatari na linaloweza kuongeza uwezekano wa kupata saratani ya matiti au kuathiri homoni za uzazi.
Hata hivyo, Taasisi ya Afya ya Marekani (NHI) iliwahi kufanya utafiti uliohusisha zaidi ya watu 420,000 na kubaini kuwa hakuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya kuweka simu kwenye sidiria na ugonjwa wa saratani ya matiti. Pamoja na ni muhimu kwa wanawake kubadili mtindo huu uwekaji wa simu.
Watafiti pia wameonya kuhusu tabia ya baadhi ya madereva, wakiwemo waendesha pikipiki, kuzungumza na simu wakati wa kuendesha vyombo vya moto, wakisema kuwa ni tabia hatarishi inayoathiri uwezo wa kuzingatia hali ya barabarani na kusababisha ajali.
Vilevile, utafiti wa Chuo Kikuu cha Exeter nchini Uingereza mwaka 2014 ulieleza kuwa kuweka simu mfukoni kunaweza kuathiri ubora wa mbegu za kiume, ingawa haukutoa ushahidi wa moja kwa moja kuthibitisha madai hayo.
WHO liliwahi kutoa takwimu mwaka 2020 kwamba wanawake 685,000 walifariki kwa saratani ya matiti duniani kote, huku robo ya vifo hivyo vikirekodiwa Marekani.
Matumizi ya vifaa vya sauti kama 'earphones' pia yamekuwa kwenye mjadala, ambapo madaktari wameonya kuhusu hatari ya kupata uziwi na saratani kwa matumizi yasiyo salama ya vifaa hivyo.
Hali hiyo imefanya wataalamu kupendekeza matumizi ya muda mfupi wa vipokea sauti, si zaidi ya dakika 90 kwa mara moja, huku sauti ikipunguzwa hadi kiwango kisichozidi asilimia 80 ya sauti ya juu.
Takwimu za Wizara ya Afya zilitolewa Juni 19, 2019 na aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, zikionyesha kuwa asilimia 3 ya wanafunzi nchini wana matatizo ya usikivu na kati ya watu 100 wenye magonjwa yasiyoambukiza, watu 24 wana matatizo ya usikivu.
Aidha, WHO katika taarifa yake ya Februari 2015 ilisema kuwa vijana wapatao bilioni 1.1 duniani wako hatarini kupata matatizo ya usikivu kutokana na matumizi ya vifaa vya sauti visivyo salama.
Hali hii inaonyesha kuwa ingawa teknolojia ya simu za mkononi ni ya manufaa makubwa, bado ni muhimu kwa watumiaji kuwa waangalifu na kuzingatia usalama wa kiafya kwa kuacha tabia zinazoweza kusababisha madhara ya muda mrefu kwa afya yao.
Salim Mohammed ni mwanahabari anayeishi mkoani Tanga. 0655 902929