TMDA watakiwa kufika vijijini

Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki, Agrey Muhabuki akizungumza katika kikao kazi kati ya wamiliki wa maduka ya dawa muhimu na famasi mjini Bariadi. Picha na Samwel Mwanga
Muktasari:
- TMDA ifike maeneo ya vijijini na kutoa elimu, ukaguzi na kuhakikisha maduka ya dawa muhimu yana wahudumu wenye sifa, ili wananchi wawe na uhakika na dawa wanazonunua.
Simiyu. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imetakiwa kufika katika maeneo ya vijijini ili kutoa elimu kwa wauzaji na wamiliki wa maduka ya dawa muhimu kuhusu sheria, taratibu na vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa katika uendeshaji wa maduka hayo, kwani imebainika kuwa wauzaji wengi hawana sifa stahiki.
Hayo yameelezwa leo Juni 27, 2025 mjini Bariadi katika kikao kazi kilichowakutanisha TMDA na wamiliki wa famasi na maduka ya dawa muhimu katika halmashauri ya mji wa Bariadi mkoani hapa.
Robert Mayongelo ni mmiliki wa duka la dawa muhimu mjini Bariadi amesema kuwa wamiliki wengi wa maduka ya dawa katika maeneo ya vijijini hawajui matakwa ya kisheria, jambo linalohatarisha afya za wananchi.
“Mfamasia aliyeidhinishwa ni nadra kupatikana huku vijijini na maduka mengi yanaendeshwa na watu wasio na taaluma, TMDA iende kutoa mafunzo na kusimamia utekelezaji wa sheria ya dawa na vifaa tiba ya mwaka 2019,” amesema.
Rose Makenge ni mmiliki wa Famasi iliyoko mjini Bariadi amesema kuwa kuna umuhimu wa mamlaka hiyo kufika maeneo ya vijijini mara kwa mara na kutoa elimu juu ya matumizi sahihi ya dawa.
“Tunaiomba TMDA ifike huko maeneo ya vijijini na kutoa elimu, ukaguzi na kuhakikisha maduka ya dawa muhimu yana wahudumu wenye sifa, ili wananchi wawe na uhakika na dawa wanazonunua,” amesema.
Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki, Agrey Muhabuki amesema mamlaka hiyo imejipanga kuendelea kutoa elimu na kuhakikisha wamiliki wanazingatia matakwa ya kisheria.
“TMDA inatambua changamoto ya upatikanaji wa maduka yenye wataalamu maeneo ya vijijini. Hivyo tunatoa wito kwa wamiliki kushirikiana nasi kupata elimu ya kisheria na tutazidi kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kulinda afya za wananchi,” amesema.
TMDA pia imesisitiza wamiliki wa maduka ya dawa wafuate Sheria ya dawa na vifaa tiba ya mwaka 2019, huku ikihimiza wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona maduka yanayoendeshwa kinyume na taratibu.
Akifungua kikao hicho Katibu wa Afya Mkoa wa Simiyu, Aziza Hamis amesema kuwa wafanyabiashara hao wamepewa dhamana na Serikali juu ya maisha ya wananchi hivyo ni vizuri kuifanya kwa kufuata misingi ya sheria, kanuni, miongozo na usimamizi wa maduka ya dawa pamoja na famasi.
“Zimekuwepo changamoto mbalimbali zinazotokea katika maeneo yenu ya kazi, kwa baadhi ya maduka ya wenzetu si wote wanafanya kazi kinyume na taratibu ziliozowekwa za kuendesha biashara zenu kwa kulaza wagonjwa,kuchoma sindano, kufanya tohara mambo ambayo ni kinyume na kanuni za uendeshaji wa biashara zenu,”amesema.