Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tanzania kuanza kudhibiti sukari, chumvi na mafuta kwenye vyakula

Muktasari:

  • Hatua hiyo pia itaweka msingi wa kuanzishwa kwa alama za tahadhari kwenye vifungashio vya vyakula, kudhibiti matangazo ya vyakula visivyo na afya, hususan yale yanayowalenga watoto, pamoja na kuboresha mazingira ya lishe shuleni.



Dar es Salaam. Tanzania ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha miongozo itakayowezesha kuanza kutekelezwa kwa sera mpya za lishe zinazolenga kudhibiti kiwango cha sukari, chumvi na mafuta katika vyakula vilivyosindikwa.

Hatua hiyo inalenga kupunguza ongezeko la unene uliopitiliza, kiribatumbo na magonjwa yasiyoambukiza, huku ikiboresha afya ya wananchi.

Hatua hiyo pia itaweka msingi wa kuanzishwa kwa alama za tahadhari kwenye vifungashio vya vyakula, kudhibiti matangazo ya vyakula visivyo na afya, hususan yale yanayowalenga watoto, pamoja na kuboresha mazingira ya lishe shuleni.

Akizungumza Julai 17, 2026, wakati wa Kongamano la Kimataifa la Unene (ICO) linalofanyika nchini Mexico, Mkurugenzi Msaidizi wa Huduma za Lishe katika Wizara ya Afya, Dk Neema Mwampili, amesema Serikali imefikia hatua za mwisho za kukamilisha mwongozo wa utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Lishe, utakaoweka msingi wa utekelezaji wa afua mbalimbali za kuboresha lishe nchini.

Amesema mwongozo huo utasaidia kudhibiti kiwango cha sukari, chumvi na mafuta katika vyakula vilivyosindikwa, hatua inayolenga kulinda afya ya walaji na kupunguza mzigo wa magonjwa yasiyoambukiza yanayochangiwa na lishe duni.

"Hatua hizi zinalenga kujenga mazingira yanayowezesha wananchi kufanya uchaguzi wa vyakula vyenye afya na kupunguza vihatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza," amesema Dk Mwampili.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Grace Magembe amesema Tanzania imeandaa Mfumo wa Kitaifa wa Kutathmini Ubora wa Virutubisho kwenye vyakula na kushiriki katika kuandaa mfumo wa pamoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), utakaotumika kuweka viwango vya ubora wa lishe wa vyakula katika nchi wanachama.

Dk Magembe amesema mfumo huo utasaidia kuanzishwa kwa alama za tahadhari kwenye vifungashio vya bidhaa za chakula, kudhibiti matangazo ya vyakula vyenye kiwango kikubwa cha sukari, chumvi na mafuta, pamoja na kuimarisha sera za lishe mashuleni.

Mtaalamu wa Afya ya Jamii, Dk Ali Mzige amesema bila hatua hizo kuchukuliwa, Serikali italazimika kutumia fedha nyingi zaidi kutibu magonjwa hayo badala ya kuwekeza katika huduma nyingine za afya.

“Watu wanaougua magonjwa yasiyoambukiza hupunguza tija kazini kutokana na ugonjwa, ulemavu au vifo vya mapema, hali inayoweza kuathiri uchumi wa Taifa,” amesema.

Amesema mfumo wa afya utakabiliwa na mzigo mkubwa zaidi wa huduma za muda mrefu kwa wagonjwa wa kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.

“Hali hiyo ndiyo sababu ya Serikali kuanza kuandaa sera za kudhibiti kiwango cha sukari, chumvi na mafuta kwenye vyakula vilivyosindikwa pamoja na kuweka alama za tahadhari kwenye vifungashio vya bidhaa za chakula,” amesema Dk Mzige.

Takwimu

Hatua hizo zinakuja wakati takwimu za Utafiti wa Taifa wa Vihatarishi vya Magonjwa Yasiyoambukiza (STEPS) wa mwaka 2023 zikionesha kuwa, mtu mmoja kati ya watatu nchini (asilimia 31.1) ana uzito uliozidi au unene uliopitiliza, hali inayoongeza hatari ya kupata kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na baadhi ya aina za saratani.

Takwimu zinaonesha kuwa asilimia 20.9 ya Watanzania wenye umri wa miaka 18 hadi 69 wana uzito uliozidi (overweight), huku asilimia 10.2 wakiwa na unene uliopitiliza (obesity). Kwa jumla, takribani asilimia 31.1 ya watu wazima nchini wana uzito uliozidi au unene uliopitiliza.

Takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa wanawake wanaathirika zaidi kuliko wanaume, huku tatizo hilo likiongezeka kadri umri unavyosonga.

Kwa mfano, katika kundi la watu wenye umri wa miaka 46 hadi 69, zaidi ya asilimia 36 wana uzito uliozidi au unene uliopitiliza. Kwa wanawake wa kundi hilo, kiwango hicho hufikia asilimia 46.1.

Aidha, kwa wanawake wenye umri wa miaka 20 hadi 49, takwimu za Utafiti wa Demografia na Afya Tanzania (TDHS) wa mwaka 2022 zinaonesha kuwa asilimia 22 wana uzito uliozidi, huku asilimia 14 wakiwa na unene uliopitiliza.

Hivyo, kwa jumla, asilimia 36 ya wanawake wenye umri wa miaka 20 hadi 49 wana uzito uliozidi au unene uliopitiliza, huku Dar es Salaam ikiwa miongoni mwa maeneo yenye viwango vya juu zaidi.

Hivi karibuni, Dk Magembe aliwasilisha mafanikio ya Tanzania katika kuandaa na kutekeleza sera za lishe zinazotegemea ushahidi wa kisayansi, pamoja na mikakati ya kudhibiti unene uliopitiliza na kiribatumbo.

Amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika tafiti na tathmini mbalimbali zinazosaidia kufanya uamuzi wa kisera, ikiwamo Tathmini ya Kitaifa ya Uwekezaji katika Kuzuia Uzito Uliozidi na Unene Uliopitiliza, pamoja na uchambuzi wa ubora wa lishe wa vyakula vilivyofungashwa vinavyouzwa sokoni.


Aidha, amesema tafiti zimefanyika ili kupima uelewa wa watumiaji kuhusu taarifa za lishe zinazowekwa kwenye vifungashio vya bidhaa, hatua inayolenga kuboresha mfumo wa utoaji wa taarifa kwa walaji.

"Tanzania imejenga msingi wa kisera unaotegemea ushahidi wa kisayansi. Ushirikiano kati ya Serikali, taasisi za utafiti, vyuo vikuu, asasi za kiraia na washirika wa maendeleo, umewezesha kufikiwa kwa hatua hizi," amesema Dk Magembe.

Mbali na hatua hizo, Serikali imeendelea kuhamasisha wananchi kubadili mtindo wa maisha kupitia Kampeni ya Zijue Namba Zako, inayowahimiza kupima mara kwa mara shinikizo la damu, kiwango cha sukari kwenye damu, uzito, urefu na mzunguko wa kiuno ili kubaini mapema vihatarishi vya magonjwa yasiyoambukiza.

Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Kinga, Wizara ya Afya, Dk Otilia Gowelle amesema Serikali inaendelea kuimarisha miongozo ya kuzuia na kudhibiti unene uliopitiliza na kiribatumbo ili kuongeza ufanisi wa afua za kinga na kuhimiza mabadiliko ya mtindo wa maisha.

Tanzania imetumia jukwaa hilo kuonesha hatua ilizopiga katika kujenga sera za lishe zinazolenga kulinda afya ya wananchi na kupunguza mzigo wa magonjwa hayo.