Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Haya hapa wanayopitia wenye unene wa kupindukia

Muktasari:

  • Unene wa kupindukia ni hali ya kiafya inayotokea pale mwili unapokuwa na mafuta mengi kupita kiasi, kiasi cha kuathiri afya ya mtu.

Dar es Salaam. Katika kona moja ya Stendi ya Mabasi ya Mbezi, jijini Dar es Salaam, anaonekana mwanamke mwenye umri wa makamo aliyesimama pembeni huku akihema kwa nguvu.

Jua la mchana lilikuwa kali, lakini jasho lililomtoka halikutokana na hali ya hewa pekee. Alikuwa ametembea umbali mfupi kutoka kwenye daladala hadi eneo la kusubiria usafiri mwingine, safari ambayo kwa wengi huonekana ya kawaida, lakini kwake ilikuwa kama kupanda mlima mrefu.

Hayo ndiyo maisha ya kila siku kwa baadhi ya watu wenye unene wa kupindukia, maisha yaliyojaa maumivu yasiyoonekana kwa macho ya wengi.

Nyuma ya miili hiyo kuna simulizi nzito za fedheha, upweke, magonjwa na mapambano ya kimya kimya.

Unene wa kupindukia ni hali ya kiafya inayotokea pale mwili unapokuwa na mafuta mengi kupita kiasi, kiasi cha kuathiri afya ya mtu.

Katika baadhi ya jamii za Kiafrika miaka ya nyuma, unene uliwahi kuonekana kama alama ya mafanikio au maisha mazuri, lakini sasa mambo yamebadilika kadri elimu ya lishe na afya bora inavyozidi kuenea na kuwafikia watu wengi, hasa kupitia mitandao ya kijamii, watu wamebadili mtazamo na kuuchukulia kama changamoto ya kiafya.


Simulizi zao

Akizungumza na Mwananchi, Neema Shabani, anayepitia changamoto hiyo ya kuwa na unene wa kupindukia, amesema wakati mwingine analazimika kulipia siti mbili katika daladala au kukodi bajaji ili aweze kufika katika shughuli zake za kila siku, jambo linalomuumiza kiuchumi.

“Bila kufanya hivyo sikai kwa amani katika daladala, kondakta atalalamika nimechukua nafasi kubwa, au abiria anaweza kulalamika unambana. Ili kuepusha shari, ninalipia tu siti ya watu wawili.

“Watu wanakucheka kwenye daladala, wengine hawataki ukae pembeni yao kwa sababu unachukua nafasi kubwa,” amesema Neema.

Neema anaongeza kuwa pamoja na changamoto hiyo anapopanda vyombo vya usafiri, mwili wake humfanya atumie muda mrefu kufanya shughuli zake mbalimbali kutokana na kuchoka haraka.

“Naweza kufua nguo chache tu nikawa tayari nimeshachoka, napumzika kidogo ndipo naendelea. Kutokana na hilo najikuta natumia muda mrefu kufanya kazi moja. Hii inanitesa sana,” ameeleza Neema.

Mwajuma Saidi (25), ambaye naye anapitia changamoto hiyo, amesema anapata changamoto hasa wakati wa kuchagua nguo za kuvaa, kwani huhisi hazimpendezi kutokana na muonekano wa mwili wake.

Pia amesema hata anapopiga picha za kumbukumbu mbalimbali za maisha yake huingiwa na hofu ya kupata ‘comment’ mbaya kutokana na muonekano wa mwili wake atakapozipakia katika mitandao ya kijamii.

“Hiyo ndiyo sababu hata ukipita katika kurasa zangu za mitandao ya kijamii huwezi kukuta nimepakia picha yangu hata moja, kutokana na hofu ya kushambuliwa mitandaoni kutokana na muonekano wangu,” amesema Mwajuma.

Kwa upande wake, Noel John amesema amekuwa akiudhiwa na baadhi ya watu wake wa karibu kumuita majina ambayo yeye binafsi hapendezwi nayo, ambayo yamesababishwa na namna anavyoonekana.

Baadhi ya majina ambayo Noel Ngaya amedai kumchukiza ni pamoja na bonge nyanya, kipipa, kibakuli, kaka bonge na mengineyo.

Pia amedai unene huo kupindukia umewahi kumfanya kukataliwa na mwanamke aliyempenda, akidai kuwa havutii.

“Iliniuma sana awali, lakini baadaye nilijifunza kujikubali huku nikiendelea kupambana kufanya mazoezi na kufuata ushauri wa wataalamu wa lishe ili nipunguze uzito,” amesema.


Kitaalamu imekaaje?

Akizungumza na Mwananchi, mtaalamu wa lishe kutoka Shirika la World Vision, Dk Daud Gambo, ameasema unene wa kupindukia ni hali ya mwili kuwa na mafuta mengi kuliko kiwango kinachotakiwa kiafya. Tatizo hilo limekuwa likiathiri watu wa rika zote, kuanzia watoto hadi watu wazima.

Amesema hali hiyo huweza kusababishwa na mambo mbalimbali, ikiwemo mfumo mbovu wa chakula, changamoto za homoni na mtindo usiofaa wa maisha.

“Ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, sukari nyingi, ni chanzo kikubwa cha ongezeko la uzito. Vilevile, matumizi ya vinywaji vyenye sukari nyingi kama soda na juisi za viwandani yamechangia kuongezeka kwa tatizo hilo,” amesema Gambo na kuongeza;

“Mbali na lishe, ukosefu wa mazoezi ya mwili pia umetajwa kuwa sababu nyingine. Watu wengi hutumia muda mwingi kukaa maofisini, kutazama televisheni au kutumia simu bila kufanya shughuli za mwili zinazosaidia kuchoma mafuta.”

Ameongeza kuwa baadhi ya watu hupata unene kutokana na matatizo ya homoni au msongo wa mawazo ambao wakati mwingine husababisha mtu kula sana bila kuzingatia mpangilio sahihi.

Gambo amesema unene wa kupindukia unaweza kusababisha magonjwa mbalimbali yasiyoambukiza, yakiwemo shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya moyo pamoja na matatizo ya kupumua.

Pia, watu wenye uzito mkubwa hukumbwa na maumivu ya viungo kutokana na mwili kubeba uzito mkubwa kupita kawaida. Kwa wanawake, unene unaweza kuathiri mfumo wa uzazi na kuongeza changamoto wakati wa ujauzito.

Mbali na athari za kiafya, tatizo hilo pia lina madhara ya kisaikolojia. Baadhi ya watu wenye unene hupitia unyanyapaa, kubezwa au kukosa kujiamini katika jamii kutokana na mwonekano wao.


Nini kifanyike

Gambo ameshauri watu wanaopitia changamoto hiyo kufika hospitalini ili wafanyiwe uchunguzi wa kitaalamu utakaosaidia kubaini chanzo halisi cha tatizo hilo.

Pia amesisitiza kuzingatia ulaji bora kwa kula matunda, mboga za majani na vyakula vyenye virutubisho muhimu huku wakiepuka mafuta na sukari nyingi.

“Mazoezi ya mwili nayo ni muhimu katika kudhibiti uzito. Kufanya mazoezi kwa angalau dakika 30 kila siku kunaweza kusaidia kupunguza mafuta mwilini,” ameeleza.

Amesisitiza kuwa kupunguza uzito si jambo la siku moja, bali linahitaji nidhamu, uvumilivu na mabadiliko ya maisha ya kila siku.