Siri za kuimarisha afya ya akili
Muktasari:
- Katika kuadhimisha Siku ya Afya ya Akili Duniani, wataalamu wa afya wanakubaliana kuwa, kulinda na kuboresha afya ya akili si jambo la hiari tena, bali ni hitaji la msingi kwa kila mtu.
Dar es Salaam. Katika dunia ya sasa yenye kasi kubwa na msongamano wa majukumu, changamoto za maisha zimeendelea kuathiri siyo miili yetu pekee, bali pia afya ya akili kwa kiwango kikubwa.
Kila siku watu hukumbana na presha kazini, changamoto za kifamilia, uhusiano wa kijamii na hali ngumu ya kiuchumi.
Mambo haya husababisha msongo wa mawazo, huzuni, wasiwasi, au hata kupoteza motisha ya kuendelea na shughuli za kila siku.
Katika kuadhimisha Siku ya Afya ya Akili Duniani, wataalamu wa afya wanakubaliana kuwa, kulinda na kuboresha afya ya akili si jambo la hiari tena, bali ni hitaji la msingi kwa kila mtu.
Mtaalamu wa saikolojia tiba kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Isaack Lema, anasema mtu anaweza kuchukua hatua mbalimbali katika maisha ya kila siku kulinda afya yake ya akili.
Anasema ni muhimu kila mtu kujiuliza namna anavyokabiliana na changamoto za kila siku, jinsi anavyotambua na kuonesha hisia zake, na kama ana uwezo wa kujizuia kutoa kauli hasi au kukasirika kwa wepesi.
Anasisitiza umuhimu wa ukakamavu wa kimwili na kihisia, kufanya mazoezi ya mwili na ya kiakili, kuwa na ujuzi wa kutatua matatizo, kujumuika na watu wengine, pamoja na kupata muda wa kupumzika na kulala vizuri. Haya yote ni mambo yanayosaidia ubongo kubaki katika hali nzuri ya utendaji kazi.
Daktari bingwa wa magonjwa ya akili kutoka Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili – Mirembe, Dk Godfrey Mkama, anaongeza kuwa mtu anapaswa kuwa wazi kuhusu hisia zake, kupata usingizi wa kutosha, kula mlo kamili, kushughulisha mwili, kuishi kwa kuzingatia wakati uliopo na kufurahia kile kinachotokea katika maisha yake kwa sasa.
Anasisitiza kuwa kushirikiana na watu wenye mitazamo chanya, kujali wengine, kuboresha uhusiano wa kifamilia, kuondoa kinyongo na kujitolea, ni njia muhimu za kuimarisha afya ya akili.
Aidha, anakumbusha umuhimu wa kukabiliana mapema na msongo wa mawazo au matatizo ya akili, na kutafuta msaada ili kuendelea kuwa mtu tegemeo katika jamii.
‘’Kula mlo kamili, shughulisha mwili, zingatia kikamilifu wakati uliopo kifikra na ufurahie kinachotokea,’’ anasema.
Kwa upande mwingine, Muuguzi bingwa wa afya ya akili kutoka Hospitali ya Muhimbili-Mloganzila, Shamila Mwanga, anasema kadri tunavyopambana kulinda afya ya mwili, vivyo hivyo tunapaswa kulinda afya ya akili.
Anaeleza kuwa kujitunza binafsi ni hatua ya kwanza muhimu, kulala vizuri, kula vyema vyakula sahihi, kufanya mazoezi, na kuchagua kile unachokiruhusu katika maisha yako.
Anaonya juu ya tabia ya watu kukubali kila kazi au ombi kwa kuhofia kuwakasirisha wengine, akisema hiyo ni njia ya kujitengenezea matatizo ya afya ya akili.
‘’Mtu anapojitahidi kuwaridhisha wengine kupita kiasi bila kuangalia uwezo wake au hali yake, huishia kwenye msongo wa mawazo unaoweza kumsababishia matatizo makubwa ya akili,’’ anaeleza.
Anashauri mtu aweke vipaumbele, ajue ni nini anapaswa kufanya na nini anaweza kuahirisha, na kujifunza kusema ‘hapana’ pale anapozidiwa.
Vilevile, anaeleza umuhimu wa kutambua shughuli unazozipenda kama kusali, kuimba, au kutafakari, ambazo zinaweza kusaidia kupunguza msongo wa mawazo na kuweka akili katika hali nzuri.
Aidha, Shamila anashauri watu kupunguza matumizi ya vilevi kwani huchangia kuyumbisha akili na hata kuongeza hatari ya kujiua.
Anashauri mtu ahakikishe anazungukwa na uhusiano mzuri, watu wanaoweza kumwelewa na kumtia moyo. ‘’Kuwa mtu wa shukrani na kudumisha maombi au ibada kulingana na imani yako, ni mambo yanayosaidia kuweka akili katika utulivu,’’ anasisitiza.
Wanaume hatarini
Wataalamu pia wamebaini kuwa wanaume wako katika hatari zaidi ya kupata matatizo ya afya ya akili kuliko wanawake.
Mtaalamu wa saikolojia, Saldin Kimangale, anasema mara nyingi wanaume hukosa fursa ya kuzungumza waziwazi kuhusu hisia zao kwa hofu ya kuhukumiwa kuwa ni dhaifu, jambo linalochochewa na mitazamo ya kijamii.
Anasema wanaume wengi hujenga ukuta na kuwa wagumu kutafuta msaada mapema, tofauti na wanawake, hali inayowasababishia matatizo makubwa zaidi kama Bipolar, Schizophrenia, na magonjwa ya wasiwasi.
Dk. Praxeda Swai, Mkuu wa Kitengo cha Magonjwa ya Akili Muhimbili, anasema ingawa wanawake wameonekana kuongoza kwa idadi ya wagonjwa wa nje wanaohudhuria kliniki, wanaume wanaongoza kwa kulazwa hospitalini kwa matatizo ya afya ya akili. Anasema jumla ya watu wazima wanaopata huduma za nje kwa mwaka ni 18,000, huku watoto wakiwa ni 1,400, na jumla ya wanaolazwa ni 1,500.
Pia anaeleza kuwa kumekuwa na ongezeko la wastani wa asilimia 4.8 la wagonjwa wanaofika kliniki kila mwaka tangu 2023.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2023, ilionyesha kuwa changamoto za afya ya akili zilichangia asilimia 8.15 ya vifo vya kujinyonga kwa kila watu 100,000.
Aidha, ripoti ya Wizara ya Afya ya mwaka 2022 ilieleza kuwa idadi ya wagonjwa wa afya ya akili iliongezeka kutoka 386,358 mwaka 2012 hadi 2,102,726 mwaka 2021 sawa na ongezeko la asilimia 82.
Kati ya Julai 2023 hadi Machi 2024, watu 293,952 walihudhuria vituo vya kutolea huduma za afya kwa ajili ya matatizo ya akili, ikilinganishwa na 246,544 kwa kipindi cha mwaka 2022/23.
Katika kipindi hicho, wagonjwa 19,506 walilazwa hospitalini kwa matatizo ya afya ya akili, ikilinganishwa na 13,262 mwaka uliotangulia.
Jitihada za Serikali
Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali imechukua hatua mbalimbali ili kuboresha huduma za afya ya akili nchini.
Mkurugenzi wa Huduma za Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dk Hamad Nyembea, anasema afya ya akili ni eneo la kimkakati linalopewa kipaumbele kikubwa. Anasema hospitali zote za rufaa za mikoa, zimeanzisha kliniki za kuhudumia watu wenye changamoto za afya ya akili, na kila hospitali ina watumishi waliopatiwa mafunzo ya kutoa huduma hizo.
Aidha, Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe imeanzisha utaratibu wa kufanya kambi katika hospitali za mikoa ili kuwahudumia wagonjwa pamoja na kuwajengea uwezo watumishi wa afya.
Dk Nyembea anasema lengo la muda wa kati na mrefu ni kuhakikisha kila hospitali ya mkoa ina daktari bingwa wa afya ya akili, na tayari hospitali za mikoa minne zina mabingwa hao, huku hospitali nyingine sita watumishi wake wakiwa masomoni.
Serikali pia inaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu afya ya akili na umuhimu wa kutafuta huduma mapema.
‘’Hali ya sasa inaonesha wazi kuwa matatizo ya afya ya akili yanaongezeka, na Serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha changamoto hiyo inakabiliwa kwa ufanisi,’’ anasema Dk Nyembea.