Serikali yaweka mkakati kukabili changamoto ya upatikanaji wa dawa
Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa wakati akizungumza katika kikao kazi cha kutathimini hali ya upatikanaji wa dawa cha waziri huyo na wadau wa afya kilichofanyika Aprili 2, 2026 katika makao makuu ya Bohari ya Dawa (MSD), Keko jinini Dar es Salaam.
Muktasari:
- Ni utekelezaji wa mfumo wa utoaji dawa kwa njia ya kielektroniki (e-Prescription), mfumo utakaotumika katika ngazi mbalimbali za utoaji huduma, ukiwa na lengo la kuunganisha huduma za kliniki, famasia, stoo pamoja na takwimu za matumizi ya dawa.
Dar es Salaam. Waziri wa Afya, Mohamed Mchengerwa, ametangaza mkakati mpya wa Serikali wa kuanzisha mfumo wa kielektroniki wa uandishi na utoaji wa dawa (e-Prescription), hatua inayolenga kukabiliana na changamoto sugu ya upatikanaji wa dawa nchini.
Hatua hiyo imekuja kutokana na malalamiko ya wananchi kuhusu uhaba wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya, zikiwemo zahanati, vituo vya afya na hospitali za rufaa.
Baadhi ya wagonjwa wamelalamika kuandikiwa dawa zisizopatikana katika vituo wanavyohudumiwa, hali inayowalazimu kununua dawa hizo katika maduka binafsi kwa gharama kubwa au kukosa tiba stahiki.
Akizungumza mwishoni mwa wiki, Mchengerwa amesema Serikali imeanza mchakato wa kuunganisha huduma za kliniki, famasia, stoo na mifumo ya takwimu kupitia teknolojia hiyo mpya.
Mchengerwa amesema kuwa e-Prescription itamwezesha mhudumu wa afya kuona kwa wakati halisi upatikanaji wa dawa na mbadala wake, hivyo kuandika dawa kwa kuzingatia hali halisi ya stoo na miongozo ya tiba.
“Hatutaruhusu tena mgonjwa kuandikiwa dawa ambayo haipo wakati kuna mbadala wenye kiambato kilekile,” amesisitiza.
Amesema mfumo huo utasaidia kudhibiti tabia ya baadhi ya wahudumu kuandika dawa kwa majina ya kibiashara badala ya majina ya kitaalamu, hali inayochangia ongezeko la gharama na mkanganyiko kwa wagonjwa.
Kwa mujibu wa waziri huyo, e-Prescription pia itakuwa nyenzo muhimu ya ukusanyaji wa takwimu sahihi kuhusu matumizi ya dawa, zitakazosaidia kuboresha upangaji wa mahitaji, bajeti na uagizaji.
Amebainisha kuwa mfumo huo utaongeza uwazi na uwajibikaji kwa kuwezesha ufuatiliaji wa nani ameandika dawa, lini na mgonjwa amepewa nini.
Sambamba na hilo, Mchengerwa ameelekeza maboresho ya haraka katika usimamizi wa dawa, ikiwamo kupitia upya mfumo wa upimaji wa upatikanaji wake ili kuzingatia utoshelevu kulingana na mahitaji halisi ya vituo.
Kilichobainika
Mchengerwa pia amekiri kuwepo kwa pengo kati ya takwimu rasmi za upatikanaji wa dawa na hali halisi inayowakumba wananchi wanapofika katika vituo vya kutolea huduma, akisisitiza kuwa Serikali haitaridhika na takwimu nzuri pekee huku malalamiko yakiendelea.
Amesema Serikali inalipa suala hilo uzito kwa kuhakikisha taarifa zinazotumika katika kufanya maamuzi zinaakisi uhalisia wa huduma, badala ya kuonesha mafanikio ya kinadharia yasiyoendana na hali ya vituoni.
Kwa mujibu wa waziri huyo, tathmini ya hivi karibuni imebainisha udhaifu katika maeneo kadhaa, ikiwamo uandishi wa dawa usiozingatia miongozo ya tiba, upangaji usio sahihi wa mahitaji, usimamizi dhaifu wa stoo na matumizi yasiyo sahihi ya rasilimali fedha.
Amesema changamoto hizo husababisha dawa kukosekana kwa wakati, kuisha mapema au kuagizwa kwa wingi usioendana na mahitaji halisi.
Pia, amebainisha wasiwasi kuhusu baadhi ya maduka ya dawa ndani ya vituo vya afya, yakidaiwa kuuza dawa zinazopaswa kutolewa bure, kinyume na dhamira ya kuanzishwa kwake.
Mchengerwa amesisitiza umuhimu wa kuwashirikisha wafamasia katika menejimenti ya vituo vya afya, akieleza kuwa ni wadau muhimu katika usimamizi wa dawa na upangaji wa mahitaji.
Pia, taasisi zenye madeni zimetakiwa kuwasiliana na Bohari ya Dawa (MSD) kupanga ulipaji, huku viongozi wa afya wakitakiwa kusimamia matumizi sahihi ya fedha na mifumo ya takwimu.
Amesisitiza uwajibikaji, akionya dhidi ya uchepushaji wa dawa na kusisitiza utekelezaji badala ya maneno.