Prime
PIRAMIDI YA AFYA: Haya yanasababisha kujifungua mtoto njiti

Jumatatu Aprili 7, 2025 ilikuwa ni Siku ya Afya Duniani. Chini ya mwavuli wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Tanzania iliungana na nchi nyingine kuadhimisha siku hii ya kimataifa.
Katika kuunga kampeni ya mwaka huu iliyoangazia afya ya uzazi na mtoto, leo tutapata ufahamu kuhusu watoto njiti ambao kitabibu ni hali ya mtoto kuzaliwa chini ya wiki ya 37.
Mara nyingi kujifungua mtoto njiti kunaweza kutokea kwa njia ya kawaida au kufanyiwa upasuaji, kabla ya muda kutimia kutokana na uwepo wa tishio la afya.
Takwimu za WHO zinaonyesha mwaka 2020 watoto milioni 13.4 walizaliwa njiti. Hiyo ni zaidi ya mtoto mmoja kati ya 10.
Vile vile mwaka 2019 takriban watoto 900,000 walifariki kutokana na matatizo ya kuzaliwa njiti.
Tatizo hili linaongoza kusababisha vifo vingi kwa watoto chini ya miaka mitano, hivyo kuwa ni tatizo la kiulimwengu.
Kuumwa sana na kufariki ni kutokana na watoto njiti kuwa na kinga dhaifum hivyo kuwa rahisi kuvamiwa na vimelea, kushindwa kulinda joto la mwili kutokana na ngozi kuwa changa na kukosa mafuta na kushindwa kujitegemea kula au kunyonya.
Mtoto kuzaliwa njiti sababu zinaweza kuwa matatizo upande wa mama au kichanga kilichopo nyumba ya uzazi, au wote wawili.
Inakadiriwa karibu asilimia 50 ya watoto njiti sababu za kuzaliwa hivyo hazijulikani.
Matatizo yanayoweza kuwa hatarishi ni pamoja na tishio la kifafa cha mimba kabla ya muda, ukuaji hafifu wa mtoto katika nyumba ya uzazi, uambukizi ikiwamo UTI na STI, mshtuko, ugonjwa mkali.
Mengine ni kuwa na historia ya kujifungua njiti na uchungu kabla muda kutimia, kondo la nyuma kujipachika vibaya au kukwanyuka kabla ya wakati.
Pia maji ya nyumba ya uzazi kuwa mengi, dosari za kimaumbile katika nyumba ya uzazi, kutokwa damu njia ya uzazi, udhaifu mlango wa nyumba ya uzazi, kuwa na mimba pacha au zaidi na mvurugiko wa vichochezi.
Vilevile uwepo wa kisukari cha ujauzito, shinikizo la juu wakati wa ujauzito na chupa kuvunjika kabla ya wakati, shambulizi la tando katika kondo la nyuma.
Mambo mengine ni pamoja na shinikizo la akili au msongo wa mawazo, kufanya kazi ngumu za kuchosha mwili, kuwa na uzito mdogo wakati wa ujauzito na upungufu wa damu mwilini.
Pia matumizi ya pombe, tumbaku na dawa za kulevya, umri chini ya miaka 17 au zaidi ya miaka 40 na matumizi holela ya dawa.
Muhimu kuviepuka vihatarishi vyote vilivyo ndani ya uwezo wako. Hudhuria kliniki ya ujauzito na fika mapema pale unapopata dalili za magonjwa.
Endapo vihatarishi vitabainika mapema hatua zinaweza kuchukuliwa ili kudhibiti, kutibu au ushauri. Vilevile ni muhimu kula lishe bora, mazoezi, kuepuka matumizi ya vilevi na tumbaku.
Baadhi ya vihatarishi ni vigumu kuepukika, ila vinaweza kupunguzwa makali katika huduma za afya.
Ni kweli baadhi ya familia zilizowahi kupata watoto njiti huwa na hofu kuhusu mustakabali wa afya hapo baadaye.
Kutokana na juhudi kubwa zinazoendelea katika mifumo ya afya hivi sasa, maeneo mengi yanatoa huduma bora kwa watoto njiti kwa kuzingatia miongozo ya WHO.