Ngono kwa vijana inavyochangia saratani kwenye umri mdogo -5

Dar es Salaam. Kutokana na baadhi ya vijana kuanza kujamiiana katika umri mdogo, imebainika wapo wanaopata saratani na hasa za kizazi na koo.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, aina hiyo ya saratani imeanza kujitokeza kwa vijana chini ya miaka 30, ikilinganishwa na awali maradhi hayo yalipowakabili zaidi watu wazima wenye umri kati ya miaka 50 na kuendelea.

Inaelezwa na wataalamu maambukizi ya kirusi cha Human Pappiloma Virus (HPV) ni miongoni mwa sababu za vijana hao kupata saratani za kizazi kwa wasichana na ya koo kwa wavulana.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Kinga katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk Crispin Kahesa anasema:

"Kitaalamu, tunasema angalau binti aanze kushiriki tendo la ndoa katika umri ambao ni wa mtu mzima, kuanzia miaka 18.
"Anapofanya tendo hilo katika umri mdogo ni wazi maumbile yake yanakuwa hayajakomaa, hivyo ni rahisi kupata michubuko na maambukizi,” anasema Dk Kahesa.

Anasema akipata maambukizi katika umri mdogo, mabadiliko hutokea mapema tofauti na mtu mzima.

Pasipo kutaja takwimu za idadi ya vijana walioathiriwa, Dk Kahesa anasema ni ngumu kufahamu kwa sababu mara nyingi saratani haina dalili na hutokea baadaye.

Saratani ya koo huwapata zaidi vijana wa kiume kama anavyoeleza daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Emmanuel Lugina.

Anasema inaweza kugawanywa katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni lile linalohusishwa na kirusi cha HPV na la pili ni lile ambalo haina uhusiano na kirusi hicho.

Anasema saratani ya koo inayohusishwa na HPV inatokea zaidi kwa vijana, kirusi kikisambazwa kutokana na aina ya matendo katika kutenda tendo la ndoa.

Kwa upande wake, daktari bingwa wa magonjwa ya saratani katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, Irene Nguma anasema wapo wanaopata saratani katika umri mdogo kutokana na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU).

Anasema kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania ikiwamo maambukizi yapo kwa kiwango cha juu, hivyo hupata katika umri mdogo.

Akizungumzia saratani ya kizazi, anasema wapo wanaopata katika umri wa chini ya miaka 30, akifafanua baadhi ni waliojihusisha na vitendo vya kushiriki ngono katika umri mdogo na baada ya miaka kadhaa ndipo saratani hujitokeza.

“Mtu akipata maambukizi ya kirusi siyo keshokutwa unapata saratani, inakupa madhara mbele na ndiyo maana tunatoa chanjo kwa mabinti wadogo,” anasema Dk Nguma.

Amesema iwapo wasichana watajiepusha na ngono na kuwa na wapenzi wengi wataepuka saratani hiyo katika umri mdogo.
Mwaka 2018 Serikali ya Tanzania ilianza kutoa chanjo kwa wasichana 614,734 wenye umri wa miaka 14 kuwakinga na saratani ya shingo ya kizazi, wasichana hawa kwa sasa wana umri wa miaka 20.


Augua akiwa na miaka 19

Msichana (jina linahifadhiwa) ni miongoni mwa wenye saratani ya kizazi aliyeipata katika umri mdogo ambaye ameshapatiwa matibabu ya tiba-kemikali kwa mizunguko ya dozi 12.

Ni binti wa miaka 19, mzaliwa wa Kijiji cha Kishangazi, kata ya Mtae wilayani Lushoto.

Akizungumza na Mwananchi, anasema baada ya vipimo madaktari wamemthibitishia anaweza kupona, ingawa anahitaji dozi kadhaa kumalizia matibabu.

Msichana huyo aliyezaliwa Julai 17, 2004 na kuhitimu shule ya msingi Kishangazi, aliolewa na mimba mbili ziliharibika kutokana na kutokwa damu nyingi.

Kwa mujibu wa binti huyo, alianza kushiriki ngono akiwa na miaka 14.

“Sijazaa, nilikuwa nikishika ujauzito mimba zinatoka, hivyo hospitali nilikuwa nikichomwa sindano damu inakata. Baadaye hali hiyo ilijitokeza tena na haikukata,” anaeleza.

“Hospitali ngazi za chini walikuwa wananichoma sindano damu ikate lakini iliendelea. Baadaye hali ikawa mbaya sikuweza kutembea. Sikuwa napata maumivu yoyote,” anasimulia.

Anasema zahanati ya Mshangazi ilimpa rufaa kwenda Hospitali ya Bombo ambako pia alitakiwa kwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili alikobainika kuwa na saratani ya kizazi, hivyo alitakiwa kwenda Ocean Road.

“Baada ya kupatiwa dripu la kwanza la dawa, damu ilikata na wakati huo maumivu yalishaanza nayo yakakata. Nilipopata kemo (tiba-kemikali) ya pili niliweza kusimama na damu haikutoka tena,” anasema.

Anasema tiba-kemikali kwa mzunguko wa kwanza alipata Novemba, 2023 na baada ya wiki mbili akapata nyingine.


Matibabu yake

Anasema, “Mwanzo niliishiwa kabisa damu. Nakumbuka nilikuwa na hali mbaya mpaka nililazwa ICU, ndugu na marafiki walijua nitakufa na hata baadhi ya ndugu wa mbali walishauri niachwe wasipoteze fedha. Hata mimi nilikata tamaa,” anasimulia.

Anasema alipozungumza na daktari wake alimweleza ugonjwa huo haupo katika hatua ya juu, hivyo atahitaji dozi ya tiba-kemikali na atapona.

“Alinishauri siyo vizuri kupigwa mionzi kwa kuwa mimi bado mdogo, nilimsikiliza. Nikaanza tiba-kemikali na kila ninapopokea tiba hiyo hulazwa wodini kwa siku nne,” anasema.

Mei 3, 2024 akizungumza na Mwananchi akiwa kwa baba yake eneo la Vikindu, mkoani Dar es Salaam alisema: “Madaktari wamenihakikishia kwamba saratani imeisha.”

Dada wa binti huyo (jina linahifadhiwa) anaelezea changamoto hiyo, akisema mdogo wake alianza kuumwa ghafla mwaka 2023 akiwa kwa mume wake mkoani Tanga.

“Alishaolewa kwa mume wake, akawa anaugua huko. Akampeleka Bombo, walipofika huko wakaona havieleweki akaja Muhimbili. Huku baada ya kupima ndiyo ikabainika saratani, hali ilikuwa mbaya, alikuwa anamwaga sana damu,” anasimulia.

“Alikuwa na hali mbaya, alikuwa anatokwa mabonge makubwa ya damu. Walibaini ni saratani na tukaambiwa lazima aanzishiwe matibabu haraka, wakisema watatupunguzia na itatugharimu kulipia kuanzia Sh2 milioni na wakatusisitiza mtaweza,” anasema.

Anasema walikaa kikao cha familia, hivyo walianza mchakato kwa kila mwanafamilia kuchangia kiasi kidogo kwa ajili ya matibabu ya binti huyo.

“Walituambia fedha tutalipa kidogo kidogo. Kwa kifupi Serikali wametusaidia sababu walishasema nendeni ustawi wa jamii, mtoto apate matibabu. Madaktari walitusisitiza mtoto bado mdogo, jitahidini mumsaidie na sisi tukajitahidi Allah akafanya wepesi,” anasema.

Anasema kuna wakati alilazwa ICU, chakula alikuwa akinywa kijiko kimoja cha uji au viwili, mpaka daktari bingwa alipomtembelea aliagiza abadilishiwe, akapata nafuu na kurudishwa wodini.

Anasema walipopiga simu nyumbani kutoa taarifa kuhusu hali ya mgonjwa, kila mmoja alikata tamaa.

“Kila mtu anakwambia hatatoka, huko nyumbani Tanga walisema acheni kuhangaika hatapona, madaktari wanasema huyu atapona na wamejitahidi sana amepona kadiri ya uwezo wao, walishatutoa mashaka msijesema hatapona, lazima atapona mkitumia dawa kwa wakati,” anasema.


Kuhusu kirusi cha HPV

Wakati saratani ya shingo ya kizazi ikitajwa kuathiri wengi, aina hiyo imekuwa ikisababishwa na virusi vinavyoambukizwa kwa njia ya ngono, Kirusi cha Human Papilloma (HPV) ambacho husababisha saratani ya mlango wa kizazi.

Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani katika Hospitali ya Aga Khan, Aleesha Adatia anasema kila kirusi kina namba na vinagawanywa katika pande mbili, kwani vipo vyenye hatari zaidi na visivyo vya hatari.

Virusi visivyo na hatari vinaweza kusababisha maudhi madogo madogo kama vivimbe sehemu za siri, huku vile vyenye hatari vipatavyo 13 vikisababisha saratani.

Anapoulizwa iwapo matumizi ya kondomu yanaweza kusaidia mhusika kutokupata maambukizi ya virusi hivyo, Dk Aleesha anasema yanaweza kupunguza hatari za kupata maambukizi kwa kiasi fulani.

“Virusi hivi vinazunguka eneo lote la sehemu za siri au nyeti na si eneo ambalo kondomu inaweza kuvaliwa. Kwa wanaume virusi hivi hukaa sehemu yote ya ngozi inayoshikilia uume, korodani na sehemu ya haja kubwa,” anasema.

Anasema mwanamume akipata virusi hivi atamwambukiza kila mwanamke anayekutana naye kimwili na mwanamke akivipata huchukua kati ya miaka 15 hadi 20 kupata saratani ya shingo ya kizazi.

Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani Aga Khan, Harrison Chuwa anasema ili kujikinga na kirusi hicho ni muhimu kuepuka ngono katika umri mdogo, wapenzi wengi na mabinti wenye umri mdogo kupewa chanjo