Prime
Mazoezi yanavyoweza kuwa mbadala wa vipodozi
Muktasari:
- Mazoezi ya kawaida na mepesi yakifanyika mara kwa mara, huchangia kuboresha afya ya ngozi kwa kiwango kikubwa.
Dar es Salaam. Tangu zamani za kale, wanadamu wamekuwa na hulka ya kupenda kuwa na ngozi yenye afya, inayong'aa na kuvutia.
Hulka hii imeonekana zaidi miongoni mwa wanawake, jambo lililosababisha soko la bidhaa za urembo kukua kwa kasi duniani.
Miongoni mwa bidhaa zinazouzwa kwa wingi ni mafuta, sabuni, krimu na losheni mbalimbali za ngozi. Hata hivyo, si bidhaa zote ni salama.
Zipo zinazozalishwa kwa viwango vinavyokubalika, lakini pia zipo bidhaa bandia na nyingine ambazo zimepigwa marufuku, kutokana na kuwa na viambata hatari vinavyoweza kusababisha madhara makubwa kiafya, ikiwamo saratani.
Hata hivyo, si watu wengi wanaofahamu kuwa mazoezi ya mwili yanaweza kuwa mbadala salama na wa gharama nafuu wa matumizi ya vipodozi.
Mazoezi ya kawaida na mepesi yakifanyika mara kwa mara, huchangia kuboresha afya ya ngozi kwa kiwango kikubwa.
Mazoezi huifanya ngozi kuwa na afya njema kiasi cha kumfanya mtu mwenye umri wa miaka 50 kuonekana mchanga zaidi kuliko umri wake.
Hali kadhalika, mtu anayefanya mazoezi mara kwa mara huonekana kuchelewa kuzeeka kutokana na ngozi yake kubaki imara na yenye mvuto.
Wakati wa kufanya mazoezi, viungo mbalimbali vya mwili, hususan misuli, hufanya kazi kwa nguvu ili kuzalisha nishati.
Katika mchakato huo, misuli huvunja sukari (glucose) ili kupata nguvu, na moja ya matokeo ya mchakato huo ni kuzalishwa kwa joto.
Joto la mwili linapoongezeka, mwili hujirekebisha kwa kuongeza mzunguko wa damu na kuruhusu jasho kutoka ili kuupoza mwili na kudhibiti kiwango cha joto. Katika hatua hiyo, jasho hubeba pamoja nalo baadhi ya taka na uchafu uliopo mwilini.
Mchakato huu ni muhimu kwa afya ya ngozi kwa sababu pamoja na kuondoa joto, husaidia pia kusafisha ngozi. Sehemu ya mafuta yaliyokusanyika chini ya ngozi pamoja na taka nyingine hutolewa kupitia vitundu vya jasho, hivyo kuifanya ngozi kuwa safi na yenye afya.
Vilevile, wakati wa mazoezi, kutoka kwa jasho, huchangia kuondoa baadhi ya kemikali zenye madhara mwilini pamoja na kupunguza uwezekano wa baadhi ya vijidudu vinavyoweza kudhuru ngozi.
Hata hivyo, baada ya kufanya mazoezi ni muhimu kuoga. Kuoga husaidia kuondoa jasho, mafuta na taka zilizotolewa mwilini ambazo zinaweza kubaki juu ya ngozi na kusababisha madhara endapo hazitaondolewa.
Mbali na hilo, mazoezi husaidia kupunguza makunyanzi kwa kuimarisha tishu za ngozi. Kadiri tishu zinavyopata nguvu na kunyooka, ndivyo ngozi inavyokuwa imara zaidi na kupunguza dalili za kuzeeka mapema.
Mazoezi pia husaidia kupunguza kiwango cha kichochezi cha mwili (homoni) kinachoitwa cortisol, ambacho huongezeka mtu anapokuwa na msongo wa mawazo.
Kiwango kikubwa cha homoni hii kinaweza kuchochea kutokea kwa chunusi, vipele na hata kuharibu nyuzi za tishu za ngozi, hali inayochangia kutokea kwa makunyanzi.
Hii ndiyo sababu watu wanaopitia msongo mkubwa wa mawazo au maumivu ya kihisia, mara nyingi hupata vipele au chunusi nyingi zaidi, kutokana na kuongezeka kwa kiwango cha homoni hiyo mwilini.
Tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa mazoezi pia huongeza uwezo wa ngozi kujikarabati haraka baada ya kuumia au kuathirika, jambo linalosaidia kupunguza hatari ya baadhi ya magonjwa ya ngozi, ikiwamo saratani ya ngozi.
Kwa hiyo, ni vyema kufanya mazoezi mepesi kwa angalau dakika 30 kila siku kwa siku tano za wiki.