Kondomu: Wanaume wengi hawajui matumizi sahihi

Matumizi ya kondomu ni asilimia tano.
Muktasari:
- Kondomu zimekuwa zikitumika nchini kwa muda mrefu sasa, ambapo awali zilikuwa zikitumika kama njia ya kupanga uzazi, na baada ya kugundulika kwa VVU, zinatumika kuzuia maambukizi.
Ni asilimia tano pekee wanaojua namna ya kuzitumia kwa usahihi
Unapotembea mchana hasa mijini haikuchukui dakika tano kuweza kuona aina mbalimbali za mipira ya kiume (kondomu) katika maduka yakiwamo ya kawaida, pia yale ya dawa.
Kondomu hizo zimetengenezwa kwa sura na maumbile, rangi mbalimbali tofauti ambazo baadhi yake kwa hakika zinavutia kuzitazama.
Hadi sasa, zipo zenye harufu au marashi anuwai kama yale ya ndizi, zabibu, chokoleti na hata zile zenye harufu ya Big G.
Katika nchi zilizoendelea zikiwamo za Ulaya na Marekani, wataalamu wanaeleza kuwa zipo zile zenye mtetemo maalumu kwa ajili ya kuliongezea ladha tendo la ndoa.
Pia, zipo zenye majina ya watu maarufu kama vile, ‘Obama Condom’ ambayo ina picha ya rais huyo wa Marekani ikionyesha alama ya dole gumba na za Sir Richard.
Lakini, pamoja na kuwepo kwa kondomu zenye picha za watu maarufu kama Obama, utafiti umebaini kuwa ni asilimia tano tu ya wanaume duniani ndiyo hutumia mipira hiyo.
Utafiti huo uliochapishwa karibuni na Shirika la Afya Duniani (WHO) umebaini kuwa wanaume wengi duniani kote hawapendi kuvaa kondomu, hivyo kukinzana na hali halisi ya changamoto za afya duniani, ambapo watu milioni 2.5 huambukizwa Virusi Vya Ukimwi (VVU) kila mwaka, zaidi katika nchi za Afrika.
Nchini Marekani, Taasisi ya Bill na Melinda Gates imeandaa mashindano ya kutengeneza kondomu zitakazompa ladha ya kipekee mwanaume na mwanamke ili kuongeza matumizi ya kinga hiyo.
Lengo ni kuhakikisha kuwa mimba za utotoni pamoja na magonjwa ya zinaa hasa Ukimwi vinapungua.
“Kupungua kwa ladha ya tendo la ndoa ndicho chanzo cha watu kutopenda kuzitumia. Sasa tunafanya juhudi kuhakikisha zinatumiwa, ”anasema ofisa mipango wa taasisi hiyo, Steven Ward.
Mshauri wa Kiufundi wa Afya ya Uzazi wa Marekani, Jeff Spieler, anasema anatamani iwapo zingeundwa kondomu zinazoongeza raha ya tendo la ndoa na kulifanya tendo liwe bora zaidi kuliko bila kinga hiyo.
“Yaani, kondomu iwe nzuri zaidi kuliko kutenda tendo hilo bila kinga hiyo. Haitakuwa kama kuoga wakati umevaa koti la mvua,” anasema Spieler.
Taasisi hiyo imeahidi kutoa donge nono kwa kampuni au wabunifu binafsi watakaounda kondomu ambayo baada ya kufanyiwa majaribio itaonyesha kuwa na matokeo mazuri.
Hata hivyo, Spieler anasema, mchakato huo utakuwa mgumu kwani katika hali ya kawaida tendo lenyewe huweza kuwa baya kwa siku hiyo, hivyo kumfanya mtumiaji kuhisi kondomu hiyo haina ubora.
Hii si mara ya kwanza kwa kondomu kubuniwa kwani wataalamu wameshawahi kuunda mipira hiyo lukuki kama vilezile za Ice Cream na ‘Pleasure Plus, zenye plastiki nyembamba ambayo mtumiaji akivaa huwa ni kama hakuvaa chochote .
Hata hivyo, pamoja na aina hizo lukuki, bado watumiaji ni wachache na wanalalamika zina kasoro kadhaa kama kubana, kuunguza au kuchomoka wakati wa tendo.
Mapema mwaka jana, utafiti uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Tiba ya Kinsley ulibaini kuwa nusu ya wanaume duniani hawajui jinsi ya kuvaa mipira ya kiume (kondomu) hali inayochochea kuenea kwa maambukizi ya Ukimwi.
Ilibainika kuwa wengi huivaa vibaya kwa kuigeuza, kuivaa nusu, kuitoboa wakati wa kuvaa na kuitoa kabla ya wakati.
Mpaka sasa, aina mbili za kondomu, Morigami na ‘Pronto for Secs’, zipo katika majaribio ya kitabibu na kwa watumiaji wake.
Hata hivyo taasisi hiyo ilionyesha wasiwasi wa mafanikio ya uvumbuzi wa kondomu hizo katika nchi zilizoendelea ambazo zipo katika mrengo wa kitamaduni.
‘Katika nchi nyingine, mwanamke akibeba kondomu anaonekana kama ni kahaba, lakini kadiri maambukizi yanavyoongezeka nafikiri watajitambua,” alisema.
Hata nchini Tanzania, bado Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaidis) inashirikiana na kampuni katika kuzindua aina mbalimbali za kondomu ili kuzipa ubora na kuzifanya zipendwe na watumiaji.
Kwa mfano shirika linalotoa elimu ya afya nchini(PSI) liliwahi kuzindua kondomu yenye sura mpya yenye vidutu.
Mwenyekiti Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi nchini (Tacaids), Dk Fatma Mrisho anasema kondomu ni njia nzuri ya kuzuia maambukizi mapya iwapo hata hivyo itatumiwa ipasavyo.
Anasema Dk Mriasho kuwa kondomu zimekuwa zikitumika nchini kwa muda mrefu sasa, ambapo awali zilikuwa zikitumika kama njia ya kupanga uzazi, na baada ya kugundulika kwa VVU, zinatumika kuzuia maambukizi.
“Tafiti zilifanyika kitaifa na kimatifa na kama ilivyothibitishwa na WHO na UNAIDS ni kwamba kondomu zikitumiwa vizuri zina uwezo mkubwa wa kuzuia maambukizi ya VVU na magonjwa ya zinaa,” alisema Dk Mrisho.
Dhana potofu kuhusu kondomu
Katika nchi zinazoendelea mpaka sasa bado kuna changamoto kubwa kuhusu kondomu.
Kwa mfano wapo wanaodhani kuwa kutumia kondomu kunasababisha ugumba jambo linalosababisha wanaume kuacha kabisa kuzitumia.
Pia, zipo baadhi ya jamii ambazo watu huazimana kondomu kwa kudhani ni kitu kinachoweza kuazimwa.
Vilevile zipo jamii ambazo wanawake hukataa wanaume wanapotumia kondomu wakidhani kuwa wanaonekana wao ni makahaba. Wapo watu wanaovaa mipira hii miwili wakati wa tendo moja, jambo ambalo ni kosa na linaweza kusababisha maambukizi.
Wengine hudhani kuwa kondomu hubana na hivyo kuzuia damu kusafiri katika sehemu ya mbele ya mwanaume.
Wataalamu wanaeleza kuwa jambo ambalo si kweli kwani mipira hiyo hutanuka kwa zaidi ya inchi nane.