Kazi zinavyowakwamisha kinamama kunyonyesha

Stella Mutta (30), amekaa ofisini kwake akiendelea kuweka mahesabu sawa kwenye vitabu vyake.
Mutta alianza kutoelewana na mwajiri wake baada ya kupata ujauzito ikiwa hajamaliza mwaka mmoja tangu aanze kutekeleza mkataba wake wa kazi.
“(Kazini) walianza kutonijali na wakaamua kutonilipa mshahara wangu nilipokwenda likizo ya uzazi,” alieleza Mutta wakati akizungumza na mwandishi wa makala haya alipotembelea ofisini kwake eneo la Mtaa wa Uhuru jijini Mwanza.
Kwa bahati nzuri, Mutta alikuwa akijua haki zake na ndipo alipoamua kwenda kushtaki katika Mahakama ya Kazi ambayo iliamuru mwajiri huyo kumlipa stahiki zake (mshahara).
Kutokana na hali hiyo, Mutta aliongezewa mzigo wa kazi na kumsababishia iwe vigumu kupata muda wa kupumzika jambo ambalo ni kinyume na Sheria ya Kazi.
Hata hivyo, aliamua kutumia njia mbadala ya kuacha maziwa nyumbani lakini, dada wa kazi hakuwa na ujuzi wa kuyahifadhi.
Matokeo yake mtoto alikuwa akinywa maziwa ya baridi hali iliyomsababishia apate tatizo la mafindofindo.
Ilipofikia hatua ya mtoto kupata mafindofindo, Mutta aliamua kuacha kazi ili apate muda wa kumlea wake.
Hata hivyo, changamoto ya Mutta ni tofauti na Monica Shabani (28), ambaye ni mama wa mtoto wa mwaka mmoja.
Mama huyu anayefanya kazi Dar es Salaam ambaye ni daktari, anasema alikumbana na changamoto ya unyonyeshaji aliporejea kazini baada ya kumaliza likizo yake ya uzazi.
Anasema jirani na kazini kwake kulikuwa hakuna shule ya chekechea ambayo ingekuwa rahisi kwake kumwacha mwanaye na baada ya muda kurejea kwa ajili ya kumnyonyesha.
“Unajua naishi Tabata Kinyerezi, lakini ninakofanyia kazi ni mjini. Ilikuwa changamoto kubwa kumnyonyesha mwanangu. Pia, siwezi kukamua maziwa kwa vile hakuna sehemu ya kuyahifadhi.
“Hakuna kabisa chumba kilichotengwa kwa ajili ya faragha kama ya unyonyeshaji. Hivyo, ninapokuwa zamu kazini kwa saa 12 mtoto hanyonyi kabisa,” anaeleza.
Hali hii iliyowakumba Mutta na Shabani, siyo jambo la kushangaza.
Hiyo inatokana na kwamba kina mama wengi wanaofanya kazi wamekuwa wakikabiliwa na vikwazo vya kuratibu vyema muda wao, kupanga namna ya kunyonyesha na wakati huohuo kutimiza wajibu wao kazini.
Shirika la Afya Duniani (WHO), linasisitiza umuhimu wa mtoto kupewa maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo.
Hii inamaanisha kuwa mtoto hapaswi kupewa kitu kingine chochote zaidi ya kunyonya maziwa ya mama pekee.
Tanzania ina sheria zinazotoa mazingira rafiki kwa kinamama kupata muda wa kuwanyonyesha watoto wao lakini hata hivyo, baadhi ya waajiri hawazingatii hilo, hivyo kuathiri afya za watoto.
Kwa mujibu wa ripoti ya Utafiti wa Watu na Afya ya mwaka 2016, Tanzania imefanikiwa kupiga hatua kwa kuhakikisha idadi kubwa ya watoto wananyonya maziwa ya mama zao.
Utafiti huo unaonyesha kuwa mafanikio hayo yamefikia asilimia 59.2 lakini hali hiyo inamaanisha kuwa asilimia nyingine iliyosalia inaashiria bado hawanyonyi maziwa ya mama.
Pia, kina mama ambao wanakabiliwa na changamoto ya kupata muda wa kunyonyesha wakiwa kazini wanalazimika kuchukua uamuzi mwingine ikiwamo kuwapa maziwa ya kopo kabla hawajawaachisha kunyonya maziwa.
Kama unyonyeshaji ukizingatiwa, kuna uwezekano wa kupunguza vifo vya watoto 823,000 walioko chini ya miaka mitano kwa mwaka.
Hata hivyo, Taifa linapaswa kuweka msukumo ili kuhakikisha kina mama wanawanyonyesha watoto wao.
Dk Daniel Safi wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza, anaeleza kuwa unyonyeshaji una faidi kubwa kwa mtoto ikiwamo kumwongezea ufahamu, kukuza hisia zake pamoja na kuwa na makuzi mazuri kisaikolojia.
Pia, wanawake wanaonyonyesha wanaripotiwa kuwa na kiwango kidogo cha msongo wa mawazo hali inayowasaidia kuimarisha afya pindi wanapotoka kujifungua.
Kunyonyesha pia, kunawasaidia kuondokana na hatari ya kunenepa na kukumbwa na matatizo mengine kama vile saratani.
Kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya mwaka 2014, mama anayejifungua ana haki ya kunyonyesha mtoto wake kwa saa mbili kwa siku katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo.
Hata hivyo, ufuatiliaji uliofanywa na mwandishi wa makala haya katika makundi mawili ya kina mama jijini Dar es Salaam na Mwanza, unaonyesha kuwa waajiri wengi wanavunja sheria hiyo.
Mmoja wa kina mama hao, anasema kazini kwake hakuna sehemu ya faragha inayomwezesha mama anayenyonyesha kutimiza wajibu wake.
Kutokana na hali hiyo analazimika kujificha chini ya meza ili kukamua maziwa na baadaye kuyahifadhi kwenye chombo alichokwenda nacho kazini. Licha ya mwajiri wake kumuahidi angefanya kazi kwa nusu siku, hakumpunguzia kazi jambo analodai lilikuwa ni ahadi hewa.
Mradi huu maalumu umetekelezwa kwa msaada kutoka Kituo cha Kimataifa cha Waandishi wa Habari (ICFJ)
Kituo cha kimataifa cha waandishi (ICFJ) Mradi maalum