Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

CAG abaini uhifadhi usio salama dawa za asili

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa CAG, uhifadhi wa dawa za asili haukufuata viwango vya usafi kama inavyotakiwa na kifungu 4.7.2 cha Mwongozo wa Viwango kwa Vituo vya Tiba Asili na Tiba Mbadala wa mwaka 2007

Dar es Salaam. Ziara zilizofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere katika maeneo ya waganga wa tiba asili (vilinge), zimebaini uhifadhi usio wa usafi wa dawa za asili, huku wataalamu wa dawa wakieleza madhara yake.

Kwa mujibu wa CAG, uhifadhi wa dawa za asili haukufuata viwango vya usafi kama inavyotakiwa na kifungu 4.7.2 cha Mwongozo wa Viwango kwa Vituo vya Tiba Asili na Tiba Mbadala wa mwaka 2007.

CAG, Charles Kichere amebainisha hayo katika ripoti yake ya Udhibiti wa Tiba za Asili kwa mwaka wa fedha 2023/24 aliyoiwasilisha bungeni Aprili 16, 2025.

Kichere amesema mwongozo unazitaka dawa za asili zihifadhiwe kwenye vyombo visivyopenyeza unyevu na hewa, viwekwe sehemu zisizofikiwa na watoto na viwe vya plastiki au glasi ya kahawia ili kuzuia mwanga na kulinda viambata vinavyoathirika na mwanga.

“Hata hivyo, ukaguzi ulibaini kuwa dawa zimehifadhiwa kwenye vyombo visivyo na uwezo wa kufunga kwa hewa au unyevu, karibu na maeneo yenye unyevu na pasipo udhibiti wa halijoto na unyevu.

“Kulikuwa pia na viashiria vya uchafuzi kutokana na vumbi na wadudu kwa kukosekana kwa uingizaji hewa wa kutosha, kama inavyoonekana kwenye picha nilizoambatanisha,” amesema Kichere.

Picha zilizoambatanishwa na CAG zilionyesha dawa zimewekwa sakafuni kwenye mazingira yenye unyevu mwingi.

Picha hiyo ilipigwa na wakaguzi huko Buza, Dar es Salaam, Septemba 14 2024.

Katika picha nyingine ilionyesha dawa zimehifadhiwa kwenye vyombo visivyofungwa vizuri karibu na bati la paa (eneo lenye unyevu mwingi). Picha ilipigwa na wakaguzi huko Dutwa, mkoani Simiyu, Septemba 18, 2024.

CAG Kichere amesema masuala ya kawaida yanayotokana na uhifadhi usiofaa wa dawa za asili ni pamoja na kupungua kwa nguvu ya tiba kutokana na joto, mwanga au hewa.

Uchafuzi wa dawa kutokana na ukungu unaotokana na unyevu na uzalishaji wa viambata vyenye sumu kutoka kwa dawa zilizoharibika.

“Hii huathiri zaidi mitishamba iliyokaushwa, unga, mafuta yenye viambata vya dawa, sharubati na dawa zilizochachushwa, hali inayoweza kusababisha mzio au madhara mengine ya kiafya kwa watumiaji,” amesema.

Ametaja sababu kubwa ya kuwepo kwa hali hizi ni ucheleweshwaji wa ukaguzi wa mara kwa mara ambao ungefanya waganga wafuate masharti yaliyowekwa.

Pia, imebainika kuwa, waganga hawajapewa mafunzo sahihi juu ya masharti ya uhifadhi wa dawa na hakuna miongozo rasmi ya kuhakikisha ubora wa muda mrefu wa dawa unahifadhiwa.

“Matendo haya ya uhifadhi usio wa usafi yalishuhudiwa katika mamlaka zote za Serikali za Mitaa (LGAs) zilizotembelewa katika mikoa yote ikiwa ni pamoja na Dodoma, Arusha, Simiyu na Dar es Salaam. Hali hii inaonesha haja ya kuimarisha uelewa juu ya utunzaji na upimaji wa dawa za asili, pamoja na kutoa elimu kwa jamii ili kuhakikisha usalama na ubora wa dawa za asili,” amesema.

CAG ameonya kuwa, hali hiyo ya uhifadhi usiofaa ni hatari kiafya kwa sababu inaweza kusababisha sumu au athari nyingine kwa wagonjwa, kutokana na matumizi ya dawa zisizo salama au zisizo na ufanisi, hivyo kuhatarisha maisha ya watu.

Wataalamu wa dawa wafunguka

Kwa mujibu wa wataalamu wa dawa, muda wa kuisha matumizi yake ama dawa kushuka uwezo wa kufanya kazi au kushuka kwa kiwango cha dawa kufanya kazi inategemea na uhifadhi, uandaaji.

Rais wa Chama cha Wafamasia Tanzania (PST) Fadhili Hezekiah amesema kama dawa inapaswa kuwa na miligramu 50 ule muda wake ukipita inaanza kupungua nguvu na itakapofika mwisho wa muda wa matumizi yake inaharibika au kiwango kilichobaki hakiwezi kutekeleza mahitaji lengwa.

Amesema dawa zinazotokana na mitishamba, huchukuliwa na kuongezwa kiambata na kupitishwa kwenye mchakato kutoka kwenye dawa za unga na kutengenezwa kuwa sindano au dawa ya kidonge.

“Inapokuwa kwenye mitishamba dawa inakuwa bado ipo katika mfumo ambao haujawekewa viambata vingine, vinavyotakiwa kuhifadhi inakaa muda mfupi zaidi, tofauti na hizi zilizochakatwa tuliongeza kitu gani uwezo wa kukaa muda mrefu unakuwepo.

“Hii mitishamba inaweza ikavutia ukuaji wa viumbe wengine hasa wa asili ya mba au fangasi kama haijahifadhiwa vizuri kuna vitu vingine vipo katika hiyo dawa,” amesema.

Amesema kwenye mti kuna kemikali zingine zinazotengenezwa, hivyo kutofunga vizuri vifungashio mara nyingi viumbe wanaota na dawa inaanza kupoteza nguvu yake, uhifadhi unabaki palepale inapofunikwa vizuri.

Mfamasia wa Tiba Asili kutoka Wizara ya Afya, Ndahani Msigwa amesema wamekuwa wakidhibiti dawa za asili kwa kufanya ufuatiliaji na kutoa elimu kwa waganga wa tiba asili.

“Dawa asili ubora wake unaanzia shambani kuanzia uvunaji, ivunwe sehemu safi na salama na kama ni majani yanavunwa ambayo hayajaathirika, zikaushwe sehemu ambayo imefunikwa ili isiingie uchafu.” 


Ongezeko matumizi bila udhibiti

Katika hatua nyingine, CAG amebaini matumizi yaliyoongezeka ya dawa za asili bila udhibiti, usimamizi na utafiti, akisema ni hatari kwa afya ya umma.

Amebainisha  dawa za asili zina mchango mkubwa katika mfumo wa afya nchini, zaidi ya asilimia 60 ya Watanzania hutumia dawa za asili kutibu magonjwa.

Amesema licha ya ongezeko hilo, kumekuwa na wasiwasi kuhusu ukosefu wa utafiti wa kisayansi kuhusu dawa hizo, baadhi ya watu huendelea kuzitumia bila uthibitisho wa kisayansi, jambo linaloongeza hatari ya madhara kiafya na upotoshaji wa matibabu.

“Kwa hiyo, kuna uhitaji mkubwa wa kuweka udhibiti, kuhakikisha ubora na kuwasaidia wataalamu wa dawa za asili ili kukabiliana na changamoto hizi na kupunguza madhara yasiyotegemewa kwa watumiaji,” amesema CAG Kichere.

Alipoulizwa Ndahani, amesema katika udhibiti wa dawa kuna hatua mbalimbali wanafanya ukaguzi zinakouzwa.

“Tunafanya ukaguzi na kuangalia ubora na ufanisi, zilizopo sokoni tunaenda wakati mwingine hatuendi kuwakagua, tunanunua na kwenda nazo maabara kuzifanyia uchunguzi tunajiridhisha. Pia tunafanya usajili, kufuatilia usajili wa maduka kama yana ubora na wataalamu husika,”amesema Ndahani.

Utegemezi, umbali wa vituo

Kutokana na ziara na majadiliano na wataalamu 20 wa tiba za kienyeji kutoka katika mikoa minne iliyotembelewa ya Arusha, Dodoma, Dar es Salaam na Simiyu, CAG amebainisha kuwa wagonjwa wengine, hasa wanaoishi maeneo ya vijijini, hupendelea kutibiwa kwa wataalamu wa tiba za kienyeji kwa imani matibabu ya kisasa ni ghali zaidi.

Amesema jamii nyingi, hasa vijijini au maeneo ya mbali, hukumbwa na changamoto ya kufikia vituo vya afya ya kisasa kutokana na jiografia yao.

Hivyo gharama ya muda na fedha inayotumika kufika kwenye vituo vya afya ya kisasa huwakatisha tamaa watu kutafuta matibabu ya kisasa, hasa pale tiba mbadala kama vile tiba za kienyeji zinapatikana kwa urahisi.