Akili unde kusaidia matibabu ya afya ya akili

Muktasari:
- Kupitia jukwaa hilo lililobuniwa na watu kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma, linawawezesha kubainika mapema kwa viashiria vya matatizo ya afya ya akili na kuwaelekeza watumiaji kupata msaada na kupona kwa wakati.
Dar es Salaam. Kutambua hatua za haraka ili kutibu tatizo linalokusumbua ni moja ya njia inayoweza kukusaidia kuwa salama.
Lakini baadhi ya magonjwa kama msongo wa mawazo, wasiwasi na matatizo ya kihisia wakati mwingine imekuwa vigumu kuyabaini mwanzoni, ndipo kikundi cha wabunifu vijana kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kilipokuja na suluhisho.
Kikundi hicho kinatumia jukwaa la akili unde (AI) linalosaidia kubaini mapema viashiria vya matatizo ya afya ya akili na kuwaelekeza watumiaji kupata msaada na kupona kwa wakati.
Kwa mujibu wa wataalamu, jukwaa hilo limeundwa baada ya kubaini kuwa wagonjwa wengi hulazwa katika vituo vya afya ya akili kwa sababu ya ukosefu wa zana za kupima kiwango cha msongo wa mawazo na kutoa msaada wa mapema kabla hali haijawa mbaya zaidi.
Akizungumza na Mwananchi leo, Julai 1, 2025 kwenye Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), Mtafiti mkuu, Kulwa Malyango, ameeleza kuwa mfumo huo wa AI unaojulikana kama ‘Akili Check’ uko kwenye hatua ya majaribio, ukifanyiwa majaribio katika hospitali nne za rufaa.
“Tulitengeneza jukwaa hili ili kushughulikia changamoto zinazoongezeka za afya ya akili katika jamii ambazo zimesababisha ongezeko la visa vya kujiua.
“Tuligundua kuwa watu wengi hufikia hatua ya juu ya matatizo ya akili kutokana na kukosekana kwa uchunguzi wa mapema na matibabu ya wakati. Lengo letu ni kupunguza mzigo wa afya ya akili nchini,” amesema.
Uhitaji wa haraka wa hatua za afya ya akili unaungwa mkono na takwimu kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO), linalokadiria kuwa zaidi ya Watanzania milioni nne wanakabiliwa na matatizo ya afya ya akili.
Hata hivyo, kesi nyingi hazitambuliwi kutokana na unyanyapaa, uhaba wa rasilimali, na upungufu wa wataalamu wa afya ya akili.
Ripoti ya 2023 kutoka Mental Health Tanzania Initiative pia ilionyesha ongezeko la asilimia 40 ya visa vya msongo wa mawazo na wasiwasi miongoni mwa wanafunzi ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Malyango amesisitiza kuwa ubunifu kama huu wa jukwaa la akili unde unaweza kuwa muhimu katika kuziba pengo la huduma ya afya ya akili nchini.
Jukwaa hili huwasaidia watumiaji kutathmini kiwango chao cha msongo wa mawazo na huwapa mwongozo juu ya namna ya kukabiliana nacho kabla hali haijawa mbaya zaidi.
Hadi sasa, mfumo huo umefanyiwa majaribio katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Hospitali ya Benjamin Mkapa, Hospitali ya Milembe na Hospitali ya Amana.
“Tangu tulipoanza, zaidi ya watu 200 wamegunduliwa na kutibiwa katika hospitali hizi. Maoni kutoka kwa taasisi hizi yamekuwa mazuri, yakionesha kuwa mfumo huu ni wa kiufanisi na rahisi kutumia,” amebainisha.
Mbali na kuwasaidia watu binafsi, jukwaa hili pia linawawezesha watoa huduma za afya kwa kutoa mapendekezo ya matibabu sahihi kulingana na hali ya afya ya akili ya mtumiaji.
Kwa sasa, mfumo huo unawalenga watumiaji wenye vifaa vya kompyuta na simu janja, lakini timu hiyo inapanga kuupanua zaidi ili ufanye kazi kwenye simu za kawaida, kuhakikisha upatikanaji mpana kote nchini Tanzania.
Katika hatua nyingine, mtafiti mwingine kutoka UDOM, Jospeter Jonathan, ametengeneza mfumo mwingine wa akili unde unaoweza kusaidia wanasayansi kutambua dawa bora kwa magonjwa yanayoibuka.
“Katika miaka ya hivi karibuni, tumeshuhudia milipuko kadhaa ya magonjwa, ikiwemo Uviko-19, ambayo ilidhihirisha ukosefu wetu wa miundombinu na maandalizi ya kiteknolojia ya kukabiliana na changamoto kwa haraka. Mwaka 2023, baada ya kutafakari hali hiyo, niliamua kutengeneza mfumo huu,” ameongeza.
Alitolea mfano nchi kama China, ambapo teknolojia za hali ya juu ziliruhusu maendeleo ya haraka ya chanjo wakati wa milipuko.
“Jukwaa hili linasaidia watafiti kubuni tiba kwa magonjwa mbalimbali kwa njia rahisi na yenye ufanisi.
“Kwa mfano, mtu anapotaka kubuni tiba kwa ugonjwa kama saratani, mchakato huo huwa mrefu na mgumu, lakini kwa kutumia AI, matokeo yanaweza kupatikana papo hapo,” ameongeza.