Chukua tahadhari dhidi ya homa ya ini

Virusi vya homa ya ini ni moja ya maambukizi yanayoshika kasi katika maeneo mengi duniani, ikikadiriwa idadi ya watu milioni 257 wanaishi na virusi hivyo duniani kote.

Kama ilivyo kwa Virusi vya Ukimwi (VVU), virusi vya hepatitis B (HBV) vinaenezwa kwa njia zinazofanana kila kitu na VVU, ikiwamo kugusana damu na maji maji ya mwilini ya mtu mwenye HBV.

Ripoti ya Shirika la Afya Duniani ya mwaka 2015 inaonyesha watu 887,000 walikufa kutokana na madhara ya virusi vya HBV, ikiwamo kuoza ini na saratani ya ini.

Virusi hivi huenezwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kwa njia ya kujamiiana bila kinga, kutumia vifaa vyenye ncha kali vilivyotumika na kuongezewa damu yenye maambukizi.

Njia nyingine zinazoweza kuchangia maambukizi ni kuchangia mashine za kusafishia figo, kutumia sindano za wanaojidunga dawa za kulevya na maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Ugonjwa huu unaweza kuwa wa kawaida na kwisha baada ya kipindi kifupi au ukawa sugu. Ni moja ya maradhi ya kuambukiza yanayotishia afya za wafanyakazi wa sekta ya afya.

Madhara mabaya ya maambukizi ya HBV ni pamoja na ini kuoza, kukakamaa, kuota vichuguu na kushindwa kufanya kazi. Pia tatizo hili likidumu muda mrefu linaweza kuwa chanzo cha saratani ya ini.

Ni kawaida kwa aina hii ya homa ya ini kudumu mwilini bila kuibua dalili zozote mpaka pale madhara makubwa yanapoibuka katika ini.

Viashiria na dalili vya ugonjwa huu ni pamoja na homa, uchovu, kutapika, kichefuchefu, kukosa hamu ya kula, rangi ya ngozi kubadilika na kupata manjano kwenye tando nyeupe ya macho na viganja vya mkono.

Vile vile maumivu ya misuli na viungo vya mwili, kuhisi ladha mbaya kinywani, kukojoa mkojo mweusi, kuwashwa na maumivu upande wa juu ya tumbo wa kulia.

Ugonjwa huu hauna tiba, ila mwili unapovamiwa na virusi hivi huweza kuvidhibiti na hujitengenezea kinga ya maisha, lakini pale unaposhindwa kuvidhibiti ndipo hushambulia ini na kuibua madhara mbalimbali.

Vipimo kadhaa vinaweza kufanyika kubaini uvamizi wa virusi hivi, ikiwamo vya maabara kubaini aina ya virusi vya homa ya ini, wingi wa virusi na kutazama utendaji kazi wa ini. Picha ya ultrasound kujua hali ya kimaumbile ya ini na pia picha ya MRI inaweza kufanyika pamoja na unyofozi wa sampuli ya tishu ya ini.

Baada ya kupata dalili au viashiria vya ugonjwa huu, fika mapema katika huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi, matibabu na ushauri.

Dawa za kufubaza makali ya virusi ARVs huweza kutolewa, ili kudhibiti kuongezeka kwa virusi pamoja na kuendelea kuathirika kwa ini, ingawa si wagonjwa wote wanaweza kunufaika na matibabu ya dawa.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza watoto wote wanaozaliwa kupatiwa chanjo ya HBV. Kuwa na mpenzi mmoja mwaminifu aliyepimwa na ukishindwa tumia kinga (kondomu).

Makundi ya walio hatarini kupata homa ya ini ni pamoja na watoa huduma za afya, wafungwa, wanajeshi, wenye wapenzi wengi na wanaosafiri maeneo mbalimbali. Hawa wapewe kipaumbele kupata chanjo.