Zitto: Miswada miwili ipelekwe mkutano mmoja wa bunge

Muktasari:
- Wadau wa siasa nchini wametaka miswada ya sheria ya mabadiliko ya Katiba na sheria ya uchaguzi iwasilishwe kwa wakati mmoja bungeni.
Dar es Salaam. Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amependekeza miswada ya sheria ya mabadiliko ya Katiba na ule wa sheria ya uchaguzi iwasilishwe kwa wakati mmoja kwenye mkutano mmoja cha Bunge.
Hatua hiyo, amesema itaharakisha mchakato wa mabadiliko ya Katiba na sheria hizo kabla ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Zitto ameyasema hayo jijini Dar es Salaam leo, Jumatano Agosti 23, 2023 alipochangia mada katika mkutano wa wadau wa Demokrasia ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).
Kulingana na Kabwe, uwezekano wa kulitekeleza hilo upo kwa kuwa si mara ya kwanza kuwahi kufanyika.
"Mwaka 1992 wakati wa mabadiliko ya Tanzania kutoka kwenye mfumo wa siasa ya chama kimoja kwenda vyama vingi, miswada miwili iliwasilishwa kwa pamoja katika mkutano mmoja wa Bunge” ameelezea Kabwe na kuongeza;
"Tukiruhusu kwenda na muswada mmoja kisha turudi kuja kuandika mwingine, tutachelewa."
Hata hivyo, Kabwe ambaye ni Kiongozi wa ACT Wazalendo, ameendeleza hoja ya chama chake kuhusu hatua ya kuanza na mabadiliko ya sheria za uchaguzi ili kuendea uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu iwapo Katiba Mpya haitakuwa imekamilika.
"Tunafahamu kwamba inawezekana mchakato wa Katiba ukawa mrefu na unaweza ukarefushwa ama na michakato yenyewe kisheria lakini na ile ya badala ya kuwa taifa la kujadiliana tumegeuka taifa la kuzomeana hiyo inaweza kurefusha mchakato huo," amesema.
Akifafanua kuhusu suluhu ya kupatikana tume huru ya uchaguzi, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza amesema kuna haja ya kuangalia demokrasia ndani ya vyama kabla ya kwenda nje.
"Hapa tunajikita sana kuangalia ushindani wa chama na chama tunasahau huku tunapoanzia ndani ya vyama, kama tukifundishana vema demokrasia ndani ya vyama na misingi yake na kufundishana msitoe rushwa, basi chaguzi hata za baadhi ya vyama zitakuwa nzuri," amesema.
Ametaka watu wasifikiri marekebisho ya uchaguzi lazima kukimbilia kwenye Katiba, ilhali kunahitajika kujirekebisha ndani ya vyama.